Zitto: Nitamuunga mkono Mbowe
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amesema atamuunga mkono
HAKI SAWA: Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Zitto Kabwe wakiwasili kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara jana, ambako walihutubia mkutano wa hadhara. Picha na Ibrahimu Yamola
Mtwara. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe amesema atamuunga mkono Kiongozi
wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe pale atakapowasilisha hoja
yake bungeni kuhusu ufisadi wa zaidi ya Sh1 trilioni katika mradi wa
bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Zitto
aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja
wa Mashujaa mkoani hapa uliandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF)
kuwashukuru wakazi wa mkoa huo kwa kuwachagua viongozi wa chama hicho
katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Najua bado
mnalia kuhusu bomba la kupeleka gesi Dar es Salaam, machozi yenu
yatafutika kwani tayari habari za ufisadi mkubwa katika ujenzi wa bomba
hili zimeanza kuchomoza.
“Kiongozi wa Upinzani Bungeni
(Mbowe) ametamka mara kadhaa kuwa atatoa hoja kuhusu ufisadi katika
ujenzi wa bomba la gesi. Pale atakapohitaji msaada wetu tutamsaidia,
tunaamini gharama za mradi huu zimezidishwa mara mbili na inawezekana
kabisa kuwa zaidi ya Dola ya Marekani 600 milioni (zaidi ya Sh1
trilioni) zimegawanywa kwa watu kama rushwa kuanzia China mpaka hapa
Tanzania. Machozi yenu wana Mtwara yatafutwa kwa uwezo wa Mola,” alisema
Zitto.
Alisema katika miaka ya hivi karibuni Mkoa wa
Mtwara umechukua sura mpya kitaifa baada ya kugunduliwa kwa gesi na wao
(wananchi) wameonyesha kwamba wakiamua wanaweza kupigania masilahi ya
Taifa.
“Mmesimama kidete kuhakikisha utajiri huu
hauporwi na haturudii makosa yaliyofanyika Kanda ya Ziwa pale
tuliporuhusu madini kuporwa na mabeberu wa kimagharibi,” alisema.
Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwahutubia wakazi hao, aliwataka
viongozi wa Serikali za Mitaa waliochaguliwa kuongoza kwa misingi ya
chama ya haki sawa kwa wote.
“Profesa Muhongo (Waziri
wa Nishati na Madini, Sospeter) hana uwezo wa kuendelea kuwapo
madarakani na hapaswi kufumbiwa macho, wote waliohusika na sakata hili
lazima wachukuliwe hatua,” alisema.
Kuhusu uandikishaji
wa Daftari la Kudumu la Wapigakura alisema, “watakapokuja kuwaandikisha
jitokezeni hiyo ndiyo njia pekee ya kutafuta ukombozi wa pili wa Taifa
hili lakini msipofanya hivyo hatutawaondoa hawa CCM.”
Mapokezi yalivyokuwa
Pilika
pilika za mapokezi ya viongozi hao zilianza tangu asubuhi na ilipofika
saa 5.20 zaidi ya magari 40 yaliyopambwa kwa bendera za CUF, pikipiki
300 na bajaji 30 zilikusanyika katika daraja la Mikindani kuwapokea
viongozi hao.
Wakiwa wamevalia sare za chama chao,
wafuasi hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali ukiwamo wa “Tunataka
fedha zetu za escrow zirudi... mtumbwi wa Chenge umetoboka.’
ACT wapata kipigo
Wanachama
wa chama kipya cha ACT-Tanzania waliosafiri kutoka Dar es Salaam kwenda
Mtwara wakitumia basi dogo aina ya Coaster walikumbana na kipigo kutoka
kwa wafuasi wa CUF waliowazuia wakidai kuwa hawakualikwa.
Mmoja
wa wanachama wa ACT ambaye pia ni Mwenyeji wa Mkoa Kigoma anayeishi Dar
es Salaam, Monalisa Ndala alisema; “Tuliambiwa huu mkutano siyo wa
kwetu na ACT hawahusiki, ndipo walianza kutupiga wakitutaka kuvua sare
kama tunataka kuendelea na msafara.”