Daftari la Wapiga kura: Chadema kuchukua maamuzi magumu
Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene. Picha Na Immanuel Herman
Dar Es Salaam.Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC)
ikisisitiza kuwa ratiba ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga
kura itaenda kama ilivyopangwa, kamati kuu ya chama cha Demokrasi na
Maendeleo imesema itachukua maamuzi magumu endapo shughuli za uboreshaji
huo zitachelewa na kuharibu mchakato wa kura ya maoni.
Mkurugenzi
wa NEC, Julius Malaba alisema leo kuwa uboreshaji utaanza Februari 16
kama ilivyotangazwa awali na utamalizika kwa wakati ili kupisha ratiba
ya kura ya maoni.
“Ratiba inazingatiwa, vifaa vitafika kwa wakati na kuanza kazi kwa wakati,” alisema Malaba.
Akizungumza
wakati wa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chadema, Afisa Habari wa
Chadema, Tumaini Makene amesema chama hicho kimeitisha kikao hicho ili
kujadili hatma ya uboreshaji wa daftari hilo na muda uliobaki kabla ya
kupiga kura ya maoni Aprili 30, mwaka huu.
Pia Chadema
walisema kuwa watachukua hatua zaidi iwapo mashine za Biometric Voters
Registration(BVR) zitabainika kuwa na kasoro katika uboreshaji huo.
Zoezi
la kuandikisha Watanzania milioni 26 wenye sifa ya kupiga kura
lilitakiwa kuanza mwezi huu lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec)
imesema zoezi hilo litaanza Februari 16, mwaka huu kwa sababu bado
inasubiri mashine 7,750 za (BVR) kwa ajili ya kazi hiyo.
“Kwa
mazingira ya kawaida muda uliobaki kwa ajili ya kazi hiyo kubwa
hautoshi ndiyo maana kuitishwa kwa kikao cha dharura ili kufanya
uamuzi,”alisema Makene-