Ndassa amrithi Mwambalaswa uenyekiti wa kamati


Mwenyekiti Mpya wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa (kushoto) akipongezana na Makamu wake, Jerome Bwanausi baada ya wajumbe wa kamati hiyo kuwachagua kuwa viongozi wa kamati hiyo katika uchaguzi uliofanyika Dodoma jana. Picha na Owen Mwandumbya
Dodoma. Kamati tatu za Bunge ambazo wenyeviti wake walitakiwa kuwajibika  kutokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, zimeanza kuchagua wenyeviti wapya huku ile na Nishati na Madini ikimchagua Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa kuwa mwenyekiti wake.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya vuta nikuvute tangu vilipoanza vikao vya kamati hizo, Januari 13 mwaka huu  kutokana na wajumbe wake kugoma kufanya uchaguzi kwa maelezo kuwa hawajapewa mwongozo kutoka ofisi ya Spika.
Hata hivyo, Januari 23 Spika wa Bunge, Anne Makinda alizitaka kamati hizo za Nishati na Madini, Bajeti na Katiba, Sheria na Utawala kufanya uchaguzi kabla ya kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge, kama linavyosema azimio la tatu la Bunge kuhusu kashfa ya escrow.
Katika Azimio lake la tatu kuhusu kashfa hiyo, kati ya maazimio manane, Bunge liliazimia: “Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za kudumu za Bunge.”
Ndassa amechukua nafasi ya Victor Mwambalaswa aliyejiuzulu kutokana na azimio hilo la Bunge.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kamati hiyo zinaeleza kuwa nafasi ya makamu mwenyekiti imebaki kwa Jerome Bwanausi ambaye ni Mbunge wa Lulindi.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kamati hiyo imefanya uchaguzi na kumchagua Ndassa kama mwenyekiti wao.
Alisema kuwa kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na ile ya Bajeti zitafanya uchaguzi kama ilivyoelekezwa.
Akizungumzia kuchaguliwa kwake, Ndassa alisema kamati hiyo ina mambo mengi na inasimamia wizara ambayo mawaziri na makatibu wakuu wengi wamekuwa wakiondolewa.
”Tutasimamia mikataba ya mafuta na gesi na kutaka iwe wazi, pia zabuni za utafutaji gesi na mafuta si vibaya wazawa nao wakahusishwa,” alisema.
Powered by Blogger.