Kamati tatu za Bunge zamgomea Makinda
Spika wa Bunge, Anne Makinda (kulia) akiongoza kikao cha Kamati ya Uongozi kinachojumuisha wenyeviti wote wa Kamati za Bunge kilichokutana jana kupanga ratiba ya mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza vikao vyake Jumanne ijayo. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi Ndogo ya Bunge, Dar es Salaam. Picha na Owen Mwandubya.
Dar es Salaam. Danadana zimeendelea juu ya utekelezaji wa
azimio la tatu la Bunge kuhusu kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow
linaloagiza kuwajibika kwa wenyeviti wa kamati zake tatu za kudumu,
baada ya juzi Spika wa Bunge, Anne Makinda kukaririwa akisema
wameshajiuzulu, lakini wajumbe wake wameibuka jana na kusema hawatafanya
uchaguzi hadi watakapopata maelekezo kutoka Ofisi ya Spika.
Azimio
hilo ambalo ni moja ya manane ya Bunge hilo linasema: “Kamati husika za
Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya
Mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati
husika za kudumu za Bunge.”
Wenyeviti hao na kamati zao
katika mabano ni Victor Mwabalaswa (Nishati na Madini), Andrew Chenge
(Bajeti) na William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala).
Juzi,
Spika Makinda aliwaeleza waandishi wa habari kwamba wenyeviti
waliotakiwa kuvuliwa nyadhifa zao tayari wamejiuzulu na kamati husika
zinatakiwa kufanya uchaguzi kupata wengine wapya.
Hata
hivyo, jana, kwa nyakati tofauti Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati
na Madini, Jerome Bwanausi na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk
Festus Limbu walisema hawatafanya uchaguzi mpaka pale watakapopata
maelekezo kutoka Ofisi ya Spika, huku wajumbe wa kamati ya Katiba
wakieleza hivyohivyo.
Dk Limbu alisema: “Unajua Chenge
aliteuliwa na Spika Makinda kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti.
Tunachokisubiri ni ruhusa ya Spika ili tufanye uchaguzi, kama anateua
tena mwenyekiti basi tunasubiri uteuzi wake.”
Hata hivyo akizungumzia suala hilo la Chenge, Katibu wa
Bunge Dk Thomas Kashilillah alisema: “Chenge aliteuliwa katika kipindi
cha mpito ambacho kikiisha atachaguliwa mwenyekiti mwingine. Hivyo
alisema naye anaweza kuondolewa tu na wajumbe wa kamati.”
Kwa
upande wake, Bwanausi alisema: “Hatuwezi kufanya uchaguzi bila kupata
maelekezo kutoka Ofisi ya Spika. Tulichoamua kamati ni kumwondoa
Mwabalaswa katika nafasi yake ya uenyekiti, ila kama ni uchaguzi bado
hatujafanya.”
Jana, kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria
na Utawala kiliongozwa na Nyambari Nyangwine badala ya Ngeleja
aliyekiongoza juzi, licha ya kutotakiwa kufanya hivyo kulingana na
maazimio ya Bunge.
Wajumbe wa kamati hiyo waliozungumza
walieleza kuwa Nyangwine aliongoza badala ya Makamu Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Gosbert Blandes ambaye alikwenda kuhudhuria kikao cha
Kamati ya Uongozi.
Dk Kashilillah alisema jana kwamba tayari Spika ameshatoa maelekezo na kinachotakiwa kufuatwa na kamati hizo ni utekelezaji tu.
“Kauli
ya Spika kwamba wenyeviti wamejiuzulu na kuzitaka kamati husika kufanya
uchaguzi tayari ni maelekezo. Sasa hapo unataka tuseme kitu gani, labda
andikeni kuwa kamati zimekaidi agizo hilo,” alisema Kashilillah.