Lipumba,wafuasi 32 wa CUF watiwa ndani Jijini Dar leo
Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahimu Lipumba akizozana na polisi muda mfupi kabla ya kukamatwa pamoja na wafuasi wengine 32 wa chama hicho jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam
limewakamata wananchama wa Chama cha Wananchi CUF 32 akiwemo Mwenyekiti
Taifa wa chama hicho,Profesa Ibrahim Lipumba kwa kufanya maandamano
ambayo si halali.
Awali polisi ilizuia maandamano
yaliyokuwa yamepangwa na chama hicho ya kuadhimisha kukumbuka ya miaka
14 tangu kufanyika kwa mauaji na mateso ya wananchi wa Zanzibar na Bara
yalifanywa na vyombo vya usalama.
Akizungumza leo Naibu
Kamishna wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam,Simon Siro alisema wanachama
waliokamatwa walikuwa 32 kati ya hao wawili ni wanawake na 30 ni wanaume
ambao wote kwa pamoja wanashikiliwa na jeshi hilo kwa ajili ya
mahojiano.
“Wanachama 32 akiwemo Profesa Lipumba
tunawashikilia katika kituo cha Polisi Kati kwa kufanya maandamano
ambayo hayana kibali, wote wapo hapa tunaendelea kuwahoji,”alisema Siro.
Siro
alisema walipewa taarifa ya maandamano hayo na viongozi wa chama hicho
hivyo jeshi hilo liliwaandikia barua ya kuzuia maandamano hayo kwa
kuhofia fujo kutokea.
Siro alisema sababu kubwa ya
kuzuia maandamano hayo yasifanyike kwa kuwa mwaka 2001 yalifanyika
maandamano batili yaliyosababisha baadhi ya polisi na wananchi kufa.
“Jeshi
la polisi likiruhusu hayo maandamano kuna uwezekano wa kutokea fujo na
hayo maandamano ya mwaka 2001 yalikuwa si halali na kwenye maandamano
hayo walikufa askari polisi,”alisema Siro.
Alisem
sababu nyingine ya kuzuia maandamano hayo ni kuwa hivi karibuni
walikamatwa watu wanaojihusisha na mambo ya ugaidi hivyo kutokana na
mazingira hayo jeshi la polisi linazuia mikusanyiko mikubwa kwa kuhofia
kutokea mambo mabaya.