Aliyeua Uingereza apandishwa kortini

Dar es Salaam. Raia wa Marekani, Sammy Almahri anayedaiwa kumuua mpenzi wake Nadine Aburas nchini Uingereza kisha kumkimbia, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la mauaji.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila jana alidai kuwa mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo la mauaji Desemba 31 mwaka jana.
Wakili Mwangamila alidai kuwa mshtakiwa huyo ambaye alifanya mauaji hayo ndani ya Hoteli ya Curdiff South Wiles, alikimbilia Tanzania wakati akijua ni kinyume na sheria.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo hakuruhusiwa kuzungumza lolote mahakamani hapo kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kulisikiliza shauri hilo hadi Mahakama Kuu.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Wakili anayemtetea mshtakiwa huyo, Cuthbert Tenga aliieleza Mahakama kuwa mteja wake alipokonywa baadhi ya nyaraka zake muhimu na kwamba ana matatizo ya kiafya, pia akaunti zake za benki zimefungiwa.
Wakili Tenga aliiomba Mahakama itoe ruhusa ya kufunguliwa kwa akaunti ya mteja wake pamoja na kurudishiwa nyaraka zake alizopokonywa ili familia yake isiathirike.
Wakili Tenga aliiomba Mahakama imuonee huruma mteja wake huyo kwa madai kuwa anategemewa na familia yake na ameacha watoto wawili wanaomtegemea ambao ni wanafunzi huko Marekani.
“Almahri anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa daktari maalumu,” alisema Tenga.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwangamila aliieleza Mahakama hiyo kuwa hawakubaliani na hoja ambazo zimetolewa na upande wa utetezi. Alisema akaunti za benki zilizozuiwa kutumika zinafanyiwa upelelezi hadi hapo utakapokamilika.
Hakimu Janeth Kaluyenda baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alisema anashindwa kutoa uamuzi kuhusu matumizi ya nyaraka hizo kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo. Aliiahirisha kesi hadi Februari 15 mwaka huu.
Powered by Blogger.