Waziri wa Fedha akiri udhaifu Bandari
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya akijibu hoja za taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyowasilishwa bungeni, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Waziri wa Fedha, Saada Mkuya amesema, Serikali itabadilisha kanuni kwa malengo mahususi ya kudhibiti misamaha ya kodi.
Waziri
Mkuya alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu hoja zilizowasilishwa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto
Kabwe kuhusu Ripoti ya Ukaguzi Maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema Serikali itapitia misamaha ili kuhakikisha ile isiyokuwa na tija inaondolewa.
Akizungumzia
suala la wafanyakazi wa Mamlaka Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
kujilipa posho za safari kiasi kikubwa, Mkuya alisema walikuwa
wakijilipa tangu Septemba mwaka 2009 bila kupata kibali cha Msajili wa
Hazina kitu ambacho ni kinyume na utaratibu.
“Hivi sasa tunaidhinisha sisi wenyewe na mashirika yote ya umma yanatakiwa kupata kibali cha Msajili wa Hazina,” alisema.
Waziri
Mkuya alisema ili kuhakikisha kunakuwapo na ufanisi katika hilo,
watendaji wote wa Msajili Hazina wataondolewa kwenye bodi za mashirika
ambako ni wajumbe ili kusiwe na mwingiliano wa kimasilahi.
Kuhusu
tatizo la mtaji katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), alisema
Serikali inalishughulikia na kwamba italipa deni la Sh22.5 bilioni
zilizoelezwa na kamati.
Kuhusu deni la mashirika ya
hifadhi za jamii ambalo Serikali inadaiwa, Waziri Mkuya alisema Serikali
ina mpango wa kuuza bondi zake ili iweze kulipa deni hilo lakini
akasema hiyo itakuwa baada ya kupeleka waraka wa kusudio hilo kwenye
Baraza la Mawaziri.
Serikali za Mitaa
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa
Ghasia akijibu hoja za Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)
alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa katika mikataba ambayo haina
masilahi kwa halmashauri.
Pia, alisema ili kudhibiti
ununuzi usiozingatia sheria katika halmashauri, Serikali imeandaa
mafunzo kwa wanunuzi wote ili wajue Sheria za Ununuzi na wale
wasiozingatia watachukuliwa hatua.
Alisema kutokana na
matatizo katika halmashauri mbalimbali nchini, Serikali imewavua
madaraka wakurugenzi 21, wakurugenzi watano wamefikishwa mahakamani, 27
wamepewa onyo, pia watumishi 233 wamefukuzwa kazi na 277 wamefikishwa
mahakamani, huku 10 kesi zao zimekwisha na wengine wamefungwa na wengine
kulipa faini.
Alisema kuhusu udhaifu mkubwa katika
ukusanyaji wa mapato wameanzisha utafiti wa vyanzo vipya kwa kuanzisha
kodi ya majengo katika halmashauri, ushuru wa nyumba za kulala wageni
ambao hapo nyuma haukuwapo.
Waziri Ghasia alisema
katika kuzingatia ununuzi wa umma, Serikali itaziwezesha sekretarieti za
mikoa kusimamia na kufuatilia miradi yote ili kuhakikishwa
inatekelezwa.
Kuhusu mishahara hewa, Waziri Ghasia
alisema sasa hivi suala hilo limedhibitiwa kwa kuwa mamlaka za Tamisemi
zinatakiwa kuwasilisha majina ya watumishi waliopo kila mwezi ili
watumiwe fedha zao moja kwa moja.
Baada ya majibu hayo,
Spika Anne Makinda alitoa nafasi ya kujadiliwa kwa ripoti hizo na kumpa
nafasi Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu ambaye alianza
kuzungumzia suala la TPA na kupongeza watu kupunguzwa vyeo na akaanza
kuzungumzia suala la Uda lakini alizuiwa na Spika kwa madai kwamba kuna
kesi mahakamani kuhusu shirika hilo.
Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG), George Masaju alishauri Bunge kutokujadili suala hilo
kwa kuwa kuna mashauri matatu mahakamani jambo lililomkera Mbunge wa
Kawe (Chadema), Halima Mdee ambaye alisimama na kupinga hoja ya AG.
Baada ya maelezo hayo Spika aliahirisha Bunge.