Lipumba apandishwa kizimbani,augua ghafla
Wafuasi
wa CUF wakimuonyesha Mwenyekiti wao, Profesa Ibarahim Lipumba jeraha la
Abdul Kambaya alipokwenda kuripoti katika Kituo cha Kati Cha Polisi,
Dar es Salaam jana, Kambaya alijeruhiwa juzi wakati Polisi wakizuia
maandamano, Mtongani juzi. Picha na Anthony Siame
-
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
akikabiliwa na shtaka la kushawishi wafuasi wake kutenda kosa la jinai.
Wakimsomea
shtaka linalomkabili, mawakili wa Serikali Joseph Maugo na Hellen Moshi
walidai jana kuwa kati ya Januari 22 na 27 katika maeneo mbalimbali ya
Dar es Salaam aliwashawishi wafuasi wake kutenda kosa hilo kinyume cha
sheria.
Baada ya kusomewa, Profesa Lipumba ambaye
anatetewa na mawakili; Mohammed Tibanyendera, Peter Kibatala, Hashimu
Mziray, Fred Kiwelu na John Malya alikana shtaka hilo na kudai kuwa ni
la uongo.
Upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika na kuiomba ipange tarehe nyingine.
Mawakili
hao wa Profesa Lipumba waliiomba Mahakama impatie mteja wao masharti ya
dhamana yenye nafuu. Hakimu Mfawidhi, Isaya Arufani alimtaka Profesa
Lipumba kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika kila mmoja akiwa na barua
na kitambulisho kila mmoja kusaini hati ya dhamana ya maneno yenye
thamani ya Sh2 milioni.
Profesa Lipumba alikamilisha masharti hayo na kuachiwa huru saa 9:42 alasiri.
Baada
ya Lipumba ya kuachiwa huru, wafuasi wake waliokuwa wamefurika
mahakamani hapo walianza kuimba nyimbo za chama chao huku wakisema rais,
rais, rais. Akiwa nje ya viwanja vya Mahakama, Profesa Lipumba
aliwataka wafuasi hao kuondoka katika eneo hilo la Mahakama kwa
ustaarabu na kwamba Jumapili atatoa taarifa katika Viwanja vya Manzese
na kuwataka wananchi kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura.
Lipumba awasili polisi
Jana, saa 4.05
asubuhi, Profesa Lipumba aliliripoti katika Kituo cha Kikuu cha Polisi
Dar es Salaam, muda mfupi baada ya wafuasi wengine 32 wa chama hicho
kufika kituoni hapo kuhojiwa.
Kiongozi huyo na wafuasi hao walikamatwa na polisi juzi na baadaye kuachiwa huru na kutakiwa kuripoti jana.
Profesa
Lipumba alimaliza kuhojiwa saa 5:20 asubuhi na kutoka nje ya kituo
hicho na kuanza kuwaeleza wanahabari jinsi jinsi polisi walivyokiuka
taratibu kwa kumkamata na kumdhalilisha wakati alikuwa akiwazuia
wanachama wa CUF kutofanya maandamano.
Kitendo hicho
kiliwafanya polisi kumchukua kwa mahojiano zaidi, wakieleza kuwa kauli
zake zinaweza kuchangia kuvuruga upelelezi wa kesi inayomkabili.
Augua ghafla
Saa
7.00 mchana alitolewa kituoni hapo na kupelekwa katika Zahanati ya
Umoja wa Mataifa (UN), Kinondoni baada ya hali yake kubadilika ghafla
wakati akihojiwa.
Alikaa katika hospitalini kwa dakika 39 na kuchukuliwa moja kwa moja hadi katika Mahakama ya Kisutu.