Mawaziri wapya watinga ofisini na rundo la ahadi
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage
Dar es Salaam. Mawaziri waliobadilishwa
wizara na Rais Jakaya Kikwete, wameingia ofisini na kuahidi kutumia muda
mfupi uliobaki kuendeleza yale yaliyoachwa na watangulizi wao.
Mabadiliko
hayo yalifanyika baada ya mawaziri wawili kujiuzulu kutokana na kashfa
ya akaunti ya Tegeta Escrow. Ni Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati na
Madini na Profesa Anna Tibaijuka wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Rais Kikwete alimteuwa George Simbachawene
aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchukua
nafasi ya Profesa Muhongo na Lukuvi aliyekuwa Waziri wa Sera, Uratibu na
Bunge akimrithi Profesa Tibaijuka.
Simbachawene
alifika wizarani hapo Saa tano asubuhi na kupokelewa na wafanyakazi wa
wizara hiyo waliojipanga katika mistari miwili, huku yeye akipita
katikati yao.
“Tutaendeleza pale walipoishia wenzetu,
tutahakikisha umeme unaendelea kusambazwa nchini kwa kutumia Wakala wa
Umeme Vijijini (Rea), mafuta nayo tutashirikiana na (Ewura) Mamlaka ya
Udhibiti wa Nishati na Maji kuona bei zinashuka kulingana na bei za soko
la dunia.”
Aliongeza: “Gesi nayo tutahakikisha
inatumika na kuwanufaisha Watanzania, hususan itakapoanza kutumika
kuzalisha umeme katika Kituo cha Kinyerezi.”
Naye
Mwijage alisema: “Nimeletwa katika wizara ambayo nina uzoefu nayo
kutokana na kuwa katika sekta ya nishati tangu mwaka 1984, hivyo kama ni
mchezo umepata mchezaji.”
Kwa upande wake Waziri wa
Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi, Lukuvi alisema: “Uamuzi ya kutatua
migogoro ya ardhi haihitaji fedha, hivyo watendaji wanatakiwa kutumia
akili ili mwananchi aweze kupata haki zao za msingi.”
Awali, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka amekabidhi ofisi kwa waziri Lukuvi, huku
akimkabidhi miradi ambayo hajaitekeleza katika kipindi chake cha
uongozi, ikiwamo mradi wa mpango mji wa Dar es Salaam.
Alisema
miradi hiyo ameitekeleza kwa kiasi kikubwa, huku mingine ikiwa na
changamoto na kumtaka waziri Lukuvi kutumia akili ya ziada kuikamilisha.
Hata hivyo, Tibaijuka alisema mipango miji haijapewa umuhimu na kuitaka Serikali kuangalia upya suala la upangaji miji.
Tibaijuka
aliitaja miradi mwingine ni mradi wa Mji wa Kigamboni unaohitaji Sh14.6
bilioni kukamilika, Sera ya Watumishi wa Sekta ya Ardhi na Sera ya ubia
na Serikali kumiliki mashamba makubwa.
Kwa upande
wake, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anna Kilango alisema
ingawa wizara hiyo ina changamoto zake, atahakikisha kuwa utekelezaji
unafanyika kwa kuzishirikisha sekta zote.
“Suala la elimu siyo la waziri pekee, kuna wadau wa elimu, taasisi, walimu wenyewe na wakurugenzi,” alisema.
Kilango alisema anafahamu changamoto za kada hiyo kwa sababu amewahi kufundisha na kuahidi kuzifanyia kazi.
Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Pamela Chilongola na Laura Paul