Hatima ya Muhongo ndani ya saa 48
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano kuanza mjini Dodoma, sasa hakuna shaka kwamba Rais
Jakaya Kikwete atafanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri wakati
wowote kuanzia leo na kabla ya Jumapili (saa 48) kutokana na kukabiliwa
na safari ya nje.
Rais anatarajiwa kufanya mabadiliko
hayo baada ya kumwondoa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji
fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kuingiziwa Sh1.6 bilioni
kwenye akaunti yake.
Mwingine ni Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye anatuhumiwa kutoshughulikia kwa
makini sakata hilo na kusababisha Serikali kupoteza fedha hivyo kuwapo
kwa uwezekano mkubwa wa kumvua uwaziri utakaomlazimu Rais kufanya
mabadiliko madogo kwenye baraza lake, ikiwa ni miezi isiyozidi mitano
kabla ya kuvunja Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Rais Kikwete anaweza kutangaza mabadiliko hayo wakati wowote kuanzia leo.
“Rais
anaondoka Jumapili kwenda Davos (Uswisi kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la
Kiuchumi la Dunia (WEF)), hivyo kwa jinsi yoyote ile ni lazima atangaze
baraza kesho (leo) au Jumamosi,” alisema mpashaji habari wetu.
“Hawezi
kutangaza baraza jipya akiwa nje ya nchi, hivyo ni lazima atangaze
kesho (leo) au ikishindikana Jumamosi ili Jumapili afanye shughuli
nyingine na kuondoka.”
Hata hivyo, mabadiliko ya mwisho
ya Baraza la Mawaziri yalitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni
Sefue ambaye pia anaweza kupewa kazi hiyo.
Baada ya
kujadili sakata la uchotwaji wa fedha hizo kwa takriban siku nne,
Novemba 28, mwaka jana Bunge lilifikia maazimio manane, likiwamo la
kutaka wote waliohusika kwenye kashfa hiyo wachukuliwe hatua na mamlaka
husika, akiwamo Profesa Muhongo ambaye Rais Kikwete alisema Novemba 22,
2014 kuwa amemuweka kiporo hadi baada ya “siku mbili au tatu” kusubiri
matokeo ya uchunguzi.
Hata hivyo, shinikizo
liliongezeka baada ya Kamati Kuu ya CCM, iliyokutana Zanzibar chini ya
uenyekiti wa Rais Kikwete, kuitaka Serikali iwe imetekeleza kwa vitendo
maazimio yote ya Bunge kuhusu sakata hilo kabla ya kikao cha Bunge
kitakachoanza Jumanne ijayo na kutaka wahusika walioko kwenye dhamana za
uteuzi wachukuliwe hatua stahili na mamlaka zao kuwawajibisha mara
moja.
Pia, Kamati ya Maadili ya CCM iliyokutana Dar es
Salaam mapema wiki hii, iliwajadili wanachama waliohusika kwenye kashfa
hiyo na kupeleka taarifa yake kwenye Kamati Kuu ya chama hicho kwa hatua
zaidi.
Wakati CCM ikisema hayo, wabunge wamekuwa
wakimkumbusha kiongozi huyo wa Serikali kuchukua hatua kabla ya kikao
cha Bunge. Wabunge wawili wa mkoani Arusha, Godbless Lema na Joshua
Nassari wote kupitia Chadema, wamediriki kusema kuwa watamwondoa Profesa
Muhongo kwa mabavu kwenye ukumbi wa chombo hicho cha kutunga sheria
iwapo Rais hatakuwa amemuondoa.
Pia, nchi wahisani
zilieleza mapema mwezi huu kuwa pamoja na kuruhusu kiasi cha fedha kwa
ajili ya miradi ya maendeleo, bado zinasubiri tamko la Serikali kuhusu
sakata hilo, ikiwa ni pamoja na hatua ilizochukua kuzuia kashfa kama
hiyo isitokee tena, ili Tanzania inufaike kwa misaada hiyo ya fedha
zinazotokana na walipakodi wa nchi zao.
Wapinzani
wanamlaumu Rais Kikwete kwa kuchelea kumwondoa Profesa Muhongo baada ya
kuahidi mwezi mmoja uliopita kuwa angelifanyia uamuzi suala lake katika
muda wa siku mbili au tatu tangu Desemba 22 mwaka jana.
Kuna
habari kwamba kuchelewa kutangazwa kwa mabadiliko hayo pengine
kunatokana na Rais Kikwete kusubiri ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya
Operesheni Tokomeza, ambayo habari zinasema inaweza kuwasafisha baadhi
ya mawaziri na hivyo kumpa mwanya wa kuwarejesha, hasa kutokana na muda
wa uhai wa baraza hilo kuwa mfupi, hivyo angehitaji watu ambao
ameshafanya nao kazi.
Kabla ya kutangaza hatua
alizochukua kwa mujibu wa maazimio ya Bunge, Rais Kikwete alikatisha
ziara ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyekuwa Arabuni, kitendo
kilichotafsiriwa kuwa alitaka ushauri kuhusu mawaziri waliohusika na
hatua za kuchukua, lakini akatangaza kumvua uwaziri Profesa Tibaijuka
pekee.
Awali, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
ilipendekeza kuwa Waziri Pinda naye awajibishwe kutokana na kushindwa
kushughulikia suala hilo akiwa mtendaji mkuu wa Serikali.
Aidha,
habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kuwa Rais Kikwete pia
alitaka kutumia fursa hiyo kuwaondoa mawaziri wote waliotangaza nia ya
kugombea urais kutokana na kusakamwa kuwa wanatumia nafasi zao vibaya,
huku wakivunja taratibu za CCM.
Hata hivyo, kutokana na
ukweli kuwa Pinda ni miongoni mwa waliotangaza nia, itakuwa vigumu
kwake kumuondoa mtendaji huyo mkuu kwa kuwa itamaanisha kuvunja
Serikali.
Katika sakata la Tegeta Escrow, zaidi ya
Sh306 bilioni zilichotwa kwenye akaunti hiyo iliyokuwa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) ambayo ilifunguliwa kwa pamoja na Tanesco na kampuni ya
IPTL, ambayo iliingia mkataba wa kuliuzia umeme shirika hilo la umma,
baada ya pande hizo mbili kuingia kwenye mgogoro wa viwango vya tozo na
hivyo kufungua kesi mahakamani.
Kesi hiyo iliisha kwa
jaji kuamua kuwa pande hizo mbili zikokotoe upya viwango vya tozo hiyo,
lakini fedha zote zilizokuwamo kwenye akaunti hiyo zikaondolewa mwishoni
mwa mwaka jana na kulipwa kwa Kampuni ya Pan African Power Solutions
(PAP), ambayo ilinunua hisa zote za umiliki wa IPTL.
Wakati
malipo hayo yanafanyika, kulikuwa na pingamizi la Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ambayo ilitaka kodi ambayo Tanesco ilitakiwa ilipe,
ikatwe kwanza kabla ya IPTL kulipwa fedha zake, huku ikihoji kodi
nyingine katika ununuzi wa hisa za kampuni nyingine iliyomiliki kwa muda
hisa za IPTL ya Piperlink ulioonekana kutawaliwa na udanganyifu.
Tayari
Jaji Frederick Werema, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
ameshajiuzulu wadhifa huo, wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Wenyeviti
watatu wa kamati za Bunge, William Ngeleja, Andrew Chenge na Victor
Mwambalaswa, wamejiuzulu nyadhifa zao, ikiwa ni sehemu ya maazimio ya
Bunge. Pia kuna mlolongo wa viongozi wa umma, vigogo wa zamani wa
Serikali na watumishi wa umma walioingiziwa fedha na mmiliki wa zamani
wa Kampuni ya IPTL, James Rugemarila ambazo zinahusishwa na kashfa hiyo
au kutotangaza masilahi binafsi katika vikao vilivyohusu sakata hilo.
Chenge,
aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni Mbunge wa
Bariadi, aliingiziwa Sh1.6 bilioni, Ngeleja, waziri wa zamani wa Nishati
na Madini na Mbunge wa Sengerema aliingiziwa Sh40.4 milioni, wakati
Mwambalaswa ameondolewa kutokana na kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nishati
na Madini wakati huohuo akiwa mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco
iliyotuhumiwa kushindwa kushughulikia vizuri sakata hilo.
Wakati
hayo yakiendelea, Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) imeshawafikisha mahakamani maofisa sita waandamizi wa TRA,
Tanesco na BoT kwa tuhuma za kuhusika kwa njia moja au nyingine kwenye
kashfa hiyo.
Kauli ya wasomi
Aliyekuwa
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Dk Charles Kitima alisema:
“Nchi lazima iundwe na Serikali imara na itakayoendeleza mikakati yake
ya maendeleo. Tunakwenda katika uchaguzi hivyo nchi inahitaji Serikali
yenye viongozi madhubuti.”
Huku akitolea mfano Uchaguzi
Mkuu utakaofanyika Oktoba na Kura ya Maoni kupitisha Katiba Mpya, Dk
Kitima alisema mambo hayo yanahitaji viongozi makini wa kuyasimamia.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema: “Nadhani mabadiliko
yanaweza kuwa makubwa kutokana na matukio yaliyopo mwaka huu. Yanaweza
kuwa ni mabadiliko ya kuhakikisha kuwa Serikali iliyopo madarakani
inaendelea kuwapo. Mabadiliko ya kuisaidia CCM kushinda.”
Aliungana
na Dk Kitima, kusisitiza kuwa sakata la escrow, Uchaguzi Mkuu na Kura
ya Maoni ni kati ya mambo yanayoweza kuchangia kufanyika kwa mabadiliko
makubwa