Watayarishaji filamu nao waibuka
Chiki Mchoma
Dar es Salaam. Lile sakata la kushushwa kwa
bei za filamu, limeingia katika sura mpya baada ya watayarishaji wa
filamu nchini kujitokeza na kutoa malalamiko yao kwa Bodi ya Filamu,
kuhusu kutoshirikishwa katika vikao vinavyoendelea.
Bodi
ya Filamu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na
Michezo, Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda na Biashara, TRA, TBS,
imekuwa ikifanya vikao vya ndani zaidi ya viwili sasa na wasambazaji wa
filamu ili kuzungumzia suala ya bei ya filamu.
Mtayarishaji
wa filamu Mike Sangu aliliambia Mwananchi kuwa kitendo cha bodi hiyo
kuendesha kikao pasipo wao kushirikishwa, kimewaumiza na kwamba
wanahitaji haki itendeke ili biashara ya filamu isonge mbele kwa
manufaa.
“Tunaiomba serikali kupitia vyombo vyake vyote
vinavyoshiriki haya masuala ya filamu, kusifanyike mkutano wa aina
yoyote ile kuzungumzia bei ya filamu bila kushirikisha maprodyuza, sisi
ndiyo wenye filamu na ndiyo tunaotengeneza sasa iweje tusishirikishwe,”
alisema Sangu na kuongeza:
“Inashangaza ikiwa
msambazaji atapanga yeye bei, badala ya sisi ambao ndiyo wazalishaji,
kwa sababu tungeweza kusambaza wenyewe, lakini tunawauzia wao ili
wafanye biashara, hivyo lazima na sisi tujue nini kinaendelea, kikao cha
pili tulipata taarifa juu juu kupitia watu tuliamua kuhudhuria ili
kujua bei wanazopanga na sisi tuwauzie kwa bei gani, badala yake
tulifukuzwa na kikao kikavunjika.”
Mwongozaji na
mtayarishaji filamu Chiki Mchoma naye alisema kumekuwa na upotoshaji
kwamba msambazaji mkubwa ndiye aliyeamua kushusha bei ya filamu, lakini
wao ndiyo waliomtaka afanye hivyo.
“Kuna mkanganyiko wa bei kutoka kwa msambazaji mpaka kwa
mlaji ndiyo umesababisha migogoro hii, ilianzia kwetu baada ya kuona
hali halisi ya mfumo wa bei ya filamu bado haukui, soko linazidi kuyumba
tuligundua kwamba wizi wa filamu umekuwa ndiyo mtihani wetu, tukaona
kuna kila sababu ya kuhakikisha tunaudhibiti, tulimuomba msambazaji mkuu
ambaye ni Steps Entertainment kuhakikisha kwamba anatafuta mbinu
mbadala,” alisema Mchoma.
Alipoulizwa kuhusu sakata
hilo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu na Ukaguzi wa Michezo ya Kuigiza
Tanzania, Joyce Fisoo alisema hawajawatenga watayarishaji, bali
walizingatia upande mmoja kwanza kwa kukaa na wasambazaji ili maamuzi
yatakayofikiwa wayatangaze kwa wasanii wote kwa ujumla.
“Tunapoendesha
vikao vinavyohusu masuala ya filamu, huwa tunafanya kwa makundi, sasa
suala linalowahusu wasambazaji, hatuwezi kukaa na watayarishaji lazima
tutashindwa kufikia muafaka, sisi hatubagui mtu bali kila mwana tasnia
huwa tunakutana naye na kuzungumza naye,” alisema Joyce.
Alisema
suala la kibiashara limewafanya wazungumze na wafanya biashara ambao ni
wasambazaji, bali watayarishaji nao wangeshirikishwa baadaye.
“Kikao
cha wiki jana tulikaa na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Wizara
ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, TBS, TRA, Cosota na wengineo
ili kufikia muafaka. Kikao cha juzi hakikuwa cha kupanga bei bali
kilihusu maadhimio ya kikao kilichofanyika Desemba 30 mwaka jana,”
alisema Joyce.
Alisisitiza kuwa watayarishaji bado wana
nafasi yao na wataitwa ili kutoa ushauri wa nini kifanyike kuhusu
sakata hilo, kwani serikali ilihitaji kupata taarifa kutoka upande wa
wasambazaji kwanza.