Mawaziri wa escrow hawatuhusu-Hoseah
Dar es Salaam. Wakati wananchi wakisubiri vigogo wa serikalini
na mawaziri wanaotuhumiwa kuhusika kwenye kashfa ya uchotaji fedha
kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow kufikishwa mbele ya vyombo vya umma, ni
watumishi watano tu wa umma waliofikishwa mahakamani, lakini Mkurugenzi
wa Takukuru, Dk Edward Hoseah ana jibu la suala hilo; kazi yao ni
kufikisha mahakamani ‘vidagaa’.
Katika kashfa hiyo ya
Sh306 bilioni, mawaziri wa sasa na zamani pamoja na makatibu wakuu wa
wizara, wanatuhumiwa kwa njia moja au nyingine kuhusika kwenye
kufanikisha kwa makusudi au uzembe uchotwaji wa fedha hizo, kuikosesha
mapato Serikali na kupokea mgawo wa fedha hizo, lakini hadi sasa ni
watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Wizara ya Nishati na Madini,
Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Tanesco na Benki Kuu (BoT) pekee
waliofikishwa mahakamani.
Wote watano, ambao ni vigogo
kwenye taasisi zao, wameshtakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa
ili kufanikisha mkakati huo ulioibuliwa na gazeti la The Citizen na
baadaye Bunge kulidaka na kufikia maazimio ya kutaka wahusika wote
wawajibishwe na mamlaka zinazowahusu.
Juzi, mkurugenzi
huyo wa Takukuru aliliambia gazeti hili kuwa taasisi yake itaendelea
kuchunguza watu wote waliohusika katika kashfa ya escrow bila ya
ubaguzi, lakini akabainisha kuwa kazi ya kuwapeleka mahakamani mawaziri
na vigogo inatakiwa ifanywe na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Dk
Hoseah, ambaye aliwahi kuingia kwenye mzozo wa DPP wa zamani kutokana
na madai yake kuwa mafaili mengi ya kesi za rushwa hayafanyiwi kazi,
alisema sheria haiwaruhusu kuwapeleka mahakamani mawaziri iwapo
watabainika kuhusika kwenye vitendo vya rushwa.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 57 cha Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa ya Mwaka 2007, endapo vigogo na mawaziri watabainika kuhusishwa
na vitendo vya rushwa, jalada la uchunguzi wao litakabidhiwa kwa DPP ili
achukue hatua ya kuwapeleka mahakamani.
Dk Hoseah
alisema kwa sasa Takukuru inaendelea na uchunguzi wake mpaka
itakapojihakikishia ushahidi wa kutosha dhidi ya vigogo hao.
“Bunge
lilitoa maazimio yake na likaagiza kuchukuliwa hatua…Takukuru
tulishaanza na tunaendelea na uchunguzi. Taratibu zote zikishakamilika
kisha ushahidi ukapatikana kwa vielelezo vyote, basi watafikishwa
mahakamani wala hakuna tatizo lolote,” alisema.
“Lakini
watafikishwa mahakamani baada ya sisi kuwasilisha jalada letu la
uchunguzi kwa DPP ambaye ndiye mamlaka ya kuwafikisha mahakamani kama
sheria inavyotuagiza.”
Udhaifu huo wa sheria pia
ulizungumziwa na Bunge wakati wa kujadili kashfa ya escrow na kuazimia
kuwa sheria inayounda Takukuru ifanyiwe kazi ili iwe na mamlaka hayo ya
kufikisha mahakamani vigogo wa rushwa kubwa.
Waliohusishwa na rushwa
Mawaziri
waliotajwa kwenye sakata hilo ni Profesa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ambaye aliingiziwa
Sh1.6 bilioni na mwanahisa wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James
Rugemarila. Tibaijuka alivuliwa wadhifa huo kutokana na sakata hilo.
Wengine
ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye Rais
Jakaya Kikwete alisema amemuweka kiporo baada ya Bunge kumuona kuwa
hakushughulikia vizuri suala hilo na kuisababishia Serikali kukosa
mapato.
Wengine ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Bajeti na ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge, ambaye
aliingiziwa pia Sh1.6 bilioni kwenye akaunti yake na Rugemarila; waziri
wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja, aliyeingiziwa Sh40.4
milioni; aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4
milioni), mbunge wa zamani wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4
milioni) na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7
milioni).
Vigogo waliotajwa kwenye sakata hilo ni
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi, ambaye
amesimamishwa, Fredrick Werema, ambaye alijiuzulu kwa maelezo kuwa
ushauri wake kuhusu suala la kodi kwenye fedha hizo haukueleweka na
ulisababisha tafrani.
Awali, Dk Hoseah aliliambia
gazeti dada la The Citizen kwamba katika uchunguzi wake, hakuna kiongozi
wala kigogo yeyote ambaye atapona.
“Yeyote yule ambaye
atabainika katika uchunguzi wetu, lazima afikishwe mbele ya sheria,
hakuna kigogo wala kiongozi yeyote ataweza kukwepa endapo ushahidi
utaonekana wazi,” alisema.
Alipoulizwa kama uchunguzi
huo unamjumuisha Profesa Tibaijuka, mkurugenzi huyo alisema hawezi
kutaja jina la mtu kwa kuwa ni kinyume cha sheria kutaja jina au taarifa
ambazo ziko kwenye uchunguzi.”
Waliofikishwa mahakama
ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi sasa ni Mhandisi Mkuu wa Mradi
wa Umeme Vijijini (Rea), Theophillo Bwakea na Mkurugenzi wa Huduma za
Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa
Mujunangoma, ambao kwa pamoja wanadaiwa kupokea rushwa ya Sh485.1
milioni.
Wengine ni Meneja Misamaha ya Kodi wa TRA,
Kyabukoba Leonard Mutabingwa, Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven
Roman Urassa na Mkurugenzi wa Fedha BoT, Julius Rutta Angello
wanaokabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya jumla ya
Sh1.923 bilioni.
Maoni ya wasomi
Akizungumzia
suala hilo, Profesa Gaudence Mpangalla kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha
alihoji sababu za Serikali kushindwa kuchukua hatua za haraka kuijengea
uwezo Takukuru ili iweze kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa aina hiyo.
“Kama
tunavyoona hivi sasa inawapandisha kizimbani watumishi wengine, sasa
kuna tofauti gani na waziri atakayebainika kukutwa na kosa kama hilo?
Sioni tofauti yoyote kwa wakosaji hao,” alisema.
“Udhaifu
huo unaweza kujenga imani kwamba Serikali inawabeba mafisadi kwa mgongo
wa ofisi ya DPP kwa sababu mashtaka mengi hayafanyiwi kazi katika ofisi
hiyo.”
Mara kadhaa Dk Hoseah amekuwa akitoa kauli
zinazoonyesha kuwa ameshawasilisha majalada mengi ofisi ya DPP, lakini
amekuwa akiyakalia au kuyarudisha kutaka uchunguzi ukamilike.
Hata hivyo, Profesa Chris Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anaona hilo halitafanyika kwa hivi sasa.
“Kwa
jinsi sakata hilo lilivyoibuliwa na ushahidi kuwekwa wazi na Rais
akaonyesha hisia zake, lazima DPP ajaribu kuwa makini sana na mawaziri
au vigogo watakaofikishwa mbele yake,” alisema.
“Inamlazimu
achukue hatua za haraka. Hili suala siyo sawa na mashtaka mengine…
lakini tusubiri kwa sababu ni kiongozi mpya aliyeingia ofisi hiyo
hatujui itakuwaje.”