Watu 300 wahofiwa kula sumu Bulyanhulu
Shinyanga. Zaidi ya watu 323 wakazi wa
Kijiji cha namba 9 katika Kata ya Bulyanhulu wilayani Kahama mkoani
Shinyanga, wanahofiwa kula sumu kali aina ya sodium cyanide inayotumiwa
katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia.
Hali
hiyo imetokana na mvua kubwa kunyesha na kubomoa bwawa kubwa la ndani
ya mgodi huo wa Bulyanhulu, ambalo hutunza sumu hiyo na kusababisha maji
hayo kutiririkia kwenye bwawa la nje linalotumiwa na wananchi.
Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Acacia, Necta Foya alisema jana kuwa, maji hayo yalibomoa pia bwawa la nje na kwenda vijijini.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya
alisema baada ya maji hayo yanayosadikiwa kuwa na sumu kubomoa bwawa la
nje yalisambaa pia kwenye mashamba ya watu.
Mpesya,
ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, alisema katika eneo hilo
takriban hekta 15 za mpunga zimeathiriwa na sumu hiyo, zikiwamo bustani
za nyanya.
Mpesya alisema ili kunusuru maisha ya
wananchi hao, huduma zote za maji ya kunywa mifugo na binadamu kwenye
visima na mabwawa zimefungwa na tayari mgodi huo umevuta kwa muda maji
ya bomba ambayo sasa wananchi hao wanayatumia.
Hata hivyo, Mpesya alisema tayari watalaamu wa afya na
mazingira wamechukua sampuli ya maji hayo pamoja na nyanya kwenye
bustani inayodhaniwa kunyonya maji yenye sumu hiyo na kupeleka Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali
Pamoja na hali hiyo, jana
wananchi wote wanaoishi eneo hilo walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya
Kahama kupimwa afya zao, zoezi ambalo hadi tunakwenda mitamboni lilikuwa
likiendelea kufanywa na madaktari wote kutoka halmashauri tatu za
Wilaya ya Kahama.
Alisema uamuzi huo wa kuwapima wananchi unatokana kuhisi kuwa wametumia maji yaliyochanganyika na sumu hiyo.
Pia,
Mpesya alisema kamati yake ilikubaliana watu hao wapimwe wakati hatua
nyingine zikiendelea kufanywa ikiwa ni pamoja na kusubiri majibu kutoka
kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kujua sumu hiyo imeingia kwenye eneo
hilo kwa kiasi gani.
“Tumeliona hilo tukasimamisha
shughuli zote katika eneo hilo zikiwamo za kilimo na baada ya kupata
hali halisi ya madhara yaliyojitokeza kwenye eneo hilo, ndiyo hatua ya
kuwalipa fidia wanachi hao zitafuata,” alisema Mpesya.