Wingu zito Kura ya Maoni ya Katiba
Tundu Lisu
Dar es Salaam. Mchakato wa Katiba Mpya, hatua ya Kura ya Maoni umegubikwa na wingu zito kutokana na kuibuka utata na ukiukwaji wa sheria.
Wakati
hali ikiwa hivyo, jana Ofisi ya Rais, Ikulu iliibuka na kutoa ufafanuzi
kuwa Rais Jakaya Kikwete hajakiuka Sheria ya Kura ya Maoni kama
ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni.
Juzi,
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba alisema kuna mwingiliano unaoleta mkanganyiko katika mchakato wa
kuboresha Daftari la Wapigakura na Sheria ya Kura ya Maoni.
Jaji
Warioba alisema sheria inaweka utaratibu maalumu wa mchakato wa kura ya
maoni ambao hautaendana na ratiba ya uandikishwaji katika daftari hilo.
Alisema
Sheria Kura ya Maoni Na. 3 ya mwaka 2014 inasema wananchi wanatakiwa
kupewa elimu ya kura ya maoni kwa miezi miwili na mwezi mmoja wa kampeni
lakini hadi sasa, hakuna ratiba inayoeleweka, jambo ambalo alisema
linaleta mwingiliano.
“Hii ni Januari, kama watafuata
sheria na kuanza kutoa elimu kwa kipindi cha miezi miwili, ina maana
itakuwa ni Aprili na Mei, ukijumlisha mwezi mmoja wa kampeni ambao ni
Juni ina maana kura itapigwa Julai. Ikumbukwe kuwa mwezi huo mbio za
uchaguzi zitakuwa zimepamba moto,” alisema.
Mkanganyiko
huo umeibua maswali kutoka kwa wanasiasa, wanasheria na wanaharakati
wakisema hali hiyo inaweza kuathiri kura ya maoni ambayo imepangwa
kufanyika Aprili 30.
Kwa upande mwingine, Mbunge wa
Ubungo (Chadema), John Mnyika amewasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu
udhaifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili ijadiliwe na kutoa
maazimio kutokana na kutokuwapo uwezekano wa kufanyika kura ya maoni
Aprili 30.
Kauli ya Ikulu
Mkurugenzi
wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu alisema katika mchakato huo,
Rais Kikwete alifuata taratibu zote zilizopo katika sheria hiyo, ikiwa
ni pamoja na kutangaza katika Gazeti la Serikali tarehe ya kuanza kwa
upigaji wa kura hiyo.
“Sheria inasema Rais atatangaza
tarehe hiyo wiki mbili baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa na
alitekeleza hilo na baadaye alieleza jinsi ambavyo Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) itakavyosimamia suala hilo,” alisema.
Katika
hotuba yake kwa wazee wa Dodoma Novemba mwaka jana, Rais Kikwete
alisema, “Ninaomba Watanzania wenzangu tuzingatie mamlaka ya Sheria ya
Kura ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri lini kura ya maoni itapigwa, lini
kampeni zitafanyika na lini wadau watatoa elimu, naomba tuwe na subira.
Tukizingatia sheria hii hakuna ugomvi,” alisema Rais Kikwete.
Alisema
licha ya sheria kuruhusu kampeni kufanyika ndani ya siku 60 kabla ya
kura za maoni, kwa mamlaka yake ya kiuongozi, kura na kampeni
vitafanyika ndani ya siku 30 tu.
“Kampeni zitaanza
Machi 30 na kumalizika Aprili 29 ikiwa ni siku moja kabla ya kupiga kura
ya maoni. Muda huo ndiyo utakuwa wa kufanya hivyo,” alisema Rais
Kikwete.
Hoja ya Mnyika
Mbunge huyo wa
Ubungo alisema mpaka sasa Nec ilitakiwa iwe imetangaza ratiba ya
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura lakini haijafanya hivyo,
pia Sheria ya Kura ya Maoni inasema kabla ya kufanyika kwa kura hiyo
kutakuwa na miezi miwili ya kutoa elimu ambayo haitatosha.
“Hakuna
haja ya kuuharakisha mchakato huu kwani unaweza kufanyika baada ya
Uchaguzi Mkuu, unajua baada ya mjadala, Bunge litakuja na maazimio
ambayo yatakuwa suluhisho la mchakato huu unaoharakishwa na chama
tawala.”
Mnyika ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema (Bara) alisema; “Hata Rais Kikwete anatakiwa kutengua kauli yake
kuwa kura ya maoni itafanyika Aprili 30 kwani hali ilivyo hakuna
uwezekano wa kufanyika.”
Akifafanua baadaye, Mnyika
alisema anazo taarifa za ndani ya Nec kuwa vifaa vinavyotakiwa
havijakamilika na Serikali haijatoa fedha za kutosha na ndiyo sababu
haijatangaza ratiba ya uboreshaji daftari.
Alisema kwa
muda uliotangazwa kati ya Februari 15 na Machi 15 kufanya uboreshaji
huo, hauwezekani kwa kuwa hakutakuwa na muda wa kuhakiki daftari hilo
kabla ya kura ya maoni.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Nec, Julius Malaba alipoulizwa alisema atazungumzia suala hilo leo.
Msimamo wa Makamba
Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba
akizungumzia suala hilo alisema; “Kama tukijipanga vizuri kwa Tume na
Serikali tunaweza kufanikiwa na hakuna sababu ya kuharakisha kitu.
Katiba itapata uhalali kama mchakato wa kuipitisha utakuwa halali.”
Wanasheria waponda
Wanasheria
mbalimbali wamesema Sheria ya Kura ya Maoni 2013, ina upungufu mkubwa
na inaweza kuathiri Wazanzibari wengi kutoshiriki katika upigaji kura ya
maoni.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
alisema miongoni mwa udhaifu wa sheria ni pamoja na mwingiliano wa
Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013 na Sheria ya Kura ya Maoni ya 2010 ya
Zanzibar.
Alisema katika utaratibu wa kupatikana wapigakura, kila upande wa Muungano utatumia daftari lake kuwasajili.
“Kwa
upande wa Bara kuna daftari linaloandaliwa lakini kwa upande wa sheria
ya kura ya Zanzibar ya 2010, ili Mzanzibari atambuliwe na kusajiliwa
kwenye daftari la wapigakura ni lazima awe ni mkazi aliyeishi Zanzibar
kwa miaka isiyopungua mitatu,” alisema na kuongeza:
“Kutokana
na sheria hiyo, kuna Wazanzibari wengi ambao wanaishi Bara kwa muda
mrefu ambao hawatakuwa na sifa za kuandikishwa kwenye daftari hilo.
Nilitoa hoja hiyo bungeni lakini wabunge wa CCM walikataa kwa kuhofia
Wazanzibari wakipata nafasi ya kuandikishwa, wataikataa Katiba hiyo.”
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema mbali ya
udhaifu huo alioutaja Lissu, mpaka sasa hakuna dalili zozote za
kufanyika kura ya maoni kutokana na muda uliobakia.
Alisema
katika tathmini yake, hatua zote za maandalizi ya tukio hilo
zitakamilika Mei, kinyume na tarehe iliyopangwa na Serikali.
“Mpaka
sasa haijulikani daftari kama litakamilika kutokana na muda uliopangwa
na ukosefu wa fedha kwa Tume, Pili hatua ya kampeni na maandalizi
mengine yanaweza kukamilika Mei,” alisema Kibamba.
Awali, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema Nec haitaweza kukamilisha uandikishaji kabla ya Aprili 30.
“Tulikutana
kwenye kikao cha TDC ambacho kilihusisha viongozi wote wa vyama na Jaji
Lubuva alikuwapo, aliahidi kutimiza ahadi hiyo lakini mpaka sasa
hajapata fedha za kununulia vifaa vingine vilivyobakia,” alisema
Nyambabe.
Mashine za BVR zinazohitajika ni 7,750 na
zilizopatikana ni 250 tu, vituo vya kuandikishia viko 40,500 nchi nzima
na Watanzania wanaotarajiwa ni milioni 23, kwa hivyo hakuna uwezekano wa
kufanikiwa shughuli hiyo kwa mwaka huu.”
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na Kelvin Matandiko.