Spika Anna Makinda achachamaa
Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Anne Makinda amezitaka kamati
tatu za Bunge ambazo wenyeviti wake walitakiwa kuwajibika kutokana na
kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, kufanya uchaguzi wa wenyeviti
wengine kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 18 wa Bunge, Januari 27 mwaka huu
mjini Dodoma.
Uamuzi huo wa Spika Makinda umekuja
baada ya wenyeviti wa kamati hizo waliotakiwa kuwajibika, William
Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala), Victor Mwabalaswa (Nishati na
Madini) na Andrew Chenge (Bajeti) kujitambulisha kuwa bado ni wenyeviti,
huku Ngeleja akiendelea kuongoza vikao hadi juzi.
Siku
mbili zilizopita Spika Makinda alikaririwa akisema wenyeviti hao
wameshajiuzulu, lakini wajumbe wake waliibuka siku moja baadaye na
kusema hawatafanya uchaguzi hadi watakapopata maelekezo kutoka Ofisi ya
Spika.
Katika Azimio lake la tatu kuhusu kashfa hiyo,
kati ya maazimio manane, Bunge liliazimia: “Kamati husika za Kudumu za
Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa
18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za
kudumu za Bunge.”
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na
kuthibitishwa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah zilieleza kuwa
Spika Makinda ametoa agizo hilo jana mchana.
Awali,
wajumbe wa kamati hizo tatu walilithibitishia gazeti hili kuwa walipokea
maelekezo kutoka ofisi ya Spika wakiwataka kufanya uchaguzi huo kabla
ya Januari 27.
“Binafsi sisi Kamati ya Nishati na
Madini tutafanya uchaguzi wetu mjini Dodoma Jumatatu ijayo. Tumepewa
maelekezo hayo leo (jana).