CUF wamtaka Waziri Chikawe afute kesi


Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe akifafanua jambo bungeni mjini Dodoma. 
Dar es Salaam. Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF) imemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe kufuta kesi zote zilizofungliwa kutokana na tukio lililotokea mapema wiki hii la viongozi wa chama hicho na wafuasi kupigwa na kukamatwa na polisi.
Jumuiya hiyo, pia imesema kuwa itaandaa maandamano nchi nzima kulaani vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na askari wa Jeshi la Polisi vya kuwapiga wafuasi wa vyama vya upinzani na kuwafungulia mashtaka.
Wakati jumuiya hiyo ikitoa tamko hilo, kituo cha Haki za Binadamu kimelaani vikali kitendo cha polisi kupiga viongozi hao na wafuasi wa CUF, kikisema kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba Jeshi la Polisi linaonyesha upendeleo kwa chama tawala CCM ambacho kinaruhusiwa kufanya mikutano yake wakati wapinzani wanawekewa mizengwe.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jana, mwenyekiti wa JUVICUF, Hamidu Bobali alisema kabla ya kufanya maandamano hayo, wanamtaka Waziri Chikawe ajiuzulu na Serikali ifute kesi zote zinazotokana na tukio hilo.
“Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu asikubali kuliacha jeshi hilo lionekane ni la watu waliokosa nguvu ya kujenga hoja mbele ya umma. Hoja ya kuibiwa silaha kutoka Kituo cha Polisi cha Ikwiriri haikuwa na uhusiano na maandamano ya CUF, hivyo ni vema akakanusha hoja hiyo na tunaiita ya kitoto na isiyo na mashiko, “alisema Bobali.
Profesa Lipumba na wafuasi 30 wa CUF wamefunguliwa mashtaka ya kula njama, kukukusanyika na kuandamana bila ya kibali na tayari kiongozi huyo alipata dhamana juzi, huku wafuasi hao wakipata dhamana jana.
Mapema wiki hii, viongozi na wafuasi wa CUF walipigwa na kukamatwa na polisi kwa madai ya kuandamana bila kibali wakati wakiadhimisha mauaji ya wenzao waliouawa na polisi mwaka 2001. Wafuasi hao walikuwa wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 2000. Katika machafuko hayo, watu kadhaa wa kisiwani Unguja walikimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya kuepuka vurugu hizo.
Kuhusu maandamano, Bobali alisema pamoja na kupigwa, jumuiya hiyo inaandaa maandamano mengine kulaani vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyofanywa na Jeshi la Polisi.
Bobali alisema wameazimia kuandaa maandamano nchi nzima kupinga vitendo alivyoviita vya kinyama baada ya viongozi wao kwa kupigwa eneo la Mtoni Mtongani.
Alisema kilichofanyika ni unyama na uhuni kwa sababu suala la wao kuandamana kwa ajili ya kuwakumbuka wanachama wenzao hufanyika kila mwaka na huu ni mwaka wa 13 haijawahi kutokea kama walivyofanyiwa mwaka huu.
Katika hatua nyingine, mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho cha haki za binadamu, Helen Kijo-Bisimba alisema kitendo cha kuwafyatulia mabomu ya machozi na kuwajeruhi wananchi waliotii amri ya kutawanyika, ni uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na polisi.
Alisema Polisi wanapaswa kujitathmini upya kwa sababu CCM imekuwa ikiruhusiwa kufanya mikutano wakati vyama vya upinzani vinawekewa mizengwe kuwa mikutano yao inaweza kutumiwa na magaidi.
“Polisi wanasema mikutano ya vyama vya upinzani inaweza kusababisha matukio ya kigaidi, mbona CCM inaendelea na mikutano. Je, matukio ya kigaidi hayawezi kutokea kwenye mikutano ya chama tawala,” alihoji Bisimba katika taarifa yake.
Bisimba alisema kituo hicho kinalaani sababu za kiintelijensia zisizotajwa ambazo zimekuwa zikitumiwa na polisi kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani.
“Kituo kinaitaka Polisi kuhakikisha kuwa wanazielewa na kuzitii sheria zinazowaongoza katika kazi zao kwani kwa kufanya hivyo wataepusha matumizi ya nguvu dhidi ya raia ambayo husababisha majeruhi na maafa.
Wakati huohuo, wafuasi 30 wa CUF wanaokabiliwa na mashtaka ya kula njama na kukaidi amri halali ya polisi na kufanya maandamano, wameachiwa baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Emillius Mchauru jana aliwaachia huru washtakiwa hao baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika na kila mdhamini asaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh100,000.
Baada ya washtakwia hao kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 12 kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika.
Sakata la kupigwa kwa wafuasi hao lilisababisha kikao cha Bunge cha Jumatano kuvurugika baada ya mbunge wa kuteuliwa na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kutaka chombo hicho kisitishe shughuli zake kwa ajili ya kujadili jambo la “dharura kwa maslahi mapana ya Taifa”.
Lakini Spika Anne Makinda alisema suala hilo lingejadiliwa siku inayofuata, maelezo ambayo yalipingwa na wabunge, hasa kutoka vyama vya upinzani, ambao waliamua kusimama na kupiga kelele na kusababisha Spika ashindwe kuendelea na kikao hicho na hivyo kuahirisha hadi Jumatano.
Katika kikao cha Jumatano, ulizuka utata wa mgongano wa mihimili mitatu ya nchi baada ya Mwanasheria Mkuu, George Masaju kuwataka wabunge wasijadili suala hilo kwa kuwa ni kuingilia mahakama, lakini Spika akaruhusu mjadala huo, ambao ulitawaliwa na shutuma nyingi dhidi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri Chikawe.
Powered by Blogger.