Polisi yaua majambazi wawili Dar

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wamefanikiwa kukamata silaha moja aina ya SMG namba BA172288 na risasi 10 wakati wa mapambano makali ya ana kwa ana kati ya polisi na majambazi.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alisema kwenye tukio hilo majambazi wawili waliuawa kwa risasi walipojaribu kuwashambulia askari.
“Tukio hilo lilitokea eneo la Kariakoo Mtaa wa Mkunguni na Livingstone, juzi saa 3.00 usiku na kwamba wakati wa tukio hilo umeme ulikatika,” alisema Kova.
Alisema baada ya kuanza tukio la uporaji, wasamaria wema waliwajulisha polisi ndipo kikosi maalumu cha kupamba na majambazi kilipofika na kupambana nao.
Majambazi hao, walishtuka na kuanza kuwarushia risasi askari waliokuwa katika gari ya polisi na ndipo kukawa na mapambano ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili.
Aliwataja majambazi hao wawili waliuawa kuwa ni pamoja na Allan Ocheng maarufu kama Onyango (24), raia wa Kenya na Yussuph Hamis maarufu kama Twalib (46) mshiraz mkazi wa Kariakoo huku majambazi wengine wakitoroka baada ya tukio hilo na polisi inaendelea na msako wa kuwatafuta.
Pamoja na kuuawa kwa majambazi hao na kukamatwa kwa silaha, pia zimekamatwa pikipiki mbili moja ni Sunlg yenye namba za usajili T 249 CMC rangi nyekundu na nyingine aina ya Boxer namba za usajli MC 350 AM rangi nyeusi na kwamba zilitumiwa na majambazi hao katika tukio.
Katika tukio jingine, Kova alisema majambazi sugu tisa wamekamatwa katika msako mkali unaondelea jijini Dar es Salaam, wakijihusisha na matukio ya uhalifu ya unyang’anyi wa kutumia silaha na makosa ya kuvunja nyumba usiku na kuiba.
Powered by Blogger.