Mutabingwa wa Escrow apata dhamana
Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa, akisindikizwa na askari wa Magereza kuingia katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba
Leonard Mutabingwa anayekabiliwa na kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya
zaidi ya Sh 1.6 bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu ameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya
dhamana.
Hakimu Mkazi, Frank Moshi jana alimuachia huru
Mutabingwa baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwasilisha
fedha taslimu Sh 1bilioni ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani
ya kiasi hicho cha fedha.
Mutabingwa aliachiwa huru kwa
dhamana baada ya kuwasilisha hati tano za nyumba za watu mbalimbali
zenye thamani ya Sh 1.332 bilioni, wadhamini watatu ambao kati yao
wawili walikuwa wafanyakazi wa TRA na mmoja mjasiliamari.
Kila
mdhamini kati ya wadhamini hao, kila mmoja alisaini hati ya dhamana ya
maneno yenye thamani ya Sh340 milioni na mshtakiwa huyo aruhusiwi
kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama.
Baada
ya kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu Moshi alimuachia huru
mshtakiwa huyo na akaiahirisha kesi hadi Januari 29,2015 ambapo
mshtakiwa huyo atasomewa maelezo ya awali (PH).
Awali
akisomewa hati ya mashtaka inayomkabili mshtakiwa huyo alidaiwa kuwa
alitenda makosa ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15
(1)(a) cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Mwendesha
Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Leonard Swai akimsomea mashtaka hayo yanayomkabili mbele ya Hakimu
Mkazi, Janeth Kaluyenda kuwa Januari 27, 2014 katika Benki ya Mkombozi
wilaya ya Ilala , alipokea Sh1.6 bilioni kupitia akaunti namba
00110202613801.
Swai alidai kuwa mshtakiwa huyo akiwa
katika Benki ya Mkombozi alijipatia kiasi hicho cha fedha ambacho ni
sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba alizipokea kutoka
kwa James Burchard Rugemalira ambaye ni Mshauri huru wa Kitaalam,
Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL kama tuzo
kwa kuiwakilisha kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits ambayo ni
mali ya Rugemalira mahakamani kitu ambacho ni kinyume cha sheria.