Sitta aanza kwa mkwara mzito


Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta akikagua Stesheni ya Reli Dar es Salaam jana alipotembelea mashirika na mamlaka zinazotoa huduma za uchukuzi . Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la (TRL), Elias Mshana. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta ameagiza kukamatwa na kufikishwa mahakamani mara moja kwa watumishi wa uwanja wa ndege ambao dawa za kulevya zitapita wakiwa kwenye zamu.
Waziri Sitta ameanza rasmi majukumu mapya kwa kupiga mkwara watumishi wa mashirika na taasisi zilizo chini ya wizara yake na kutoa onyo kwa wahujumu na wezi wa rasilimali za umma.
Waziri Sitta alitangaza msimamo huo jana, alipofanya ziara katika baadhi ya mashirika na kampuni zilizo chini ya wizara yake, kwa lengo la kufahamu baadhi ya changamoto pamoja na kuwahakikishia wafanyakazi utatuzi wa matatizo yao.
Waziri Sitta alitembelea na kuzungumza na watendaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Mamlaka ya Reli ya Tazara, Kampuni ya Reli (TRL) na pia akakutana na maofisa wa Kampuni ya Ndege (ATCL) na aliwaeleza nia na hatua za Serikali kushughulikia changamoto zinazowakabili kwa pamoja.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo mafupi na watendaji wa TRL, Waziri Sitta alisema kazi zote alizozianza mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe ataziendeleza tena kwa ukali zaidi na kusema si sahihi wezi wa kuku wakachomwa moto huku wahujumu na wabadhirifu wakiachwa huru.
Powered by Blogger.