Mwigulu atii agizo la Kinana, asitisha ziara zake mikoani


Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesitisha ziara zake za mikoani ili kutii agizo alilopewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Nchemba ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, alisema jana kuwa anawajibika kutekeleza amri hiyo kutoka ndani ya chama.
Alisema agizo hilo halina lengo baya zaidi ya kukijenga chama ili kufikia malengo ikiwa ni pamoja na kuimarisha nidhamu miongoni mwa wanachama.
“Huwa ananituma, anaweza akaniambia nifanye au nisifanye jambo ambalo halina masilahi ya chama,” alisema Nchemba.
Utekelezaji huo umekuja baada ya Nchemba kuandikiwa barua na Kinana ambayo pia imezagaa katika mitandao ya kijamii ikimtaka kusitisha ziara anazozifanya maeneo mbalimbali kwa kuwa hazina baraka za chama hicho.
Katika barua hiyo iliyoandikwa Januari 18, ilieleza Nchemba amekuwa akifanya ziara nyingi katika mikoa na wilaya bila ya ushirikishwaji wa makao makuu, mikoa na wilaya na hasa kamati za siasa.
Powered by Blogger.