Kali ya Mwaka-1-Hoja ya Lipumba yajadiliwa Bungeni, Kauli ya ‘wapigwe tu’ yajirudia
Spika wa Bunge, Anna Makinda akifafanua jambo bungeni
Bunge la Jamhuri ya Muungano leo limejadili kitendo cha
uvunjifu wa amani uliotokea kwenye maandamano ya CUF yaliyoongozwa na
Profesa Ibrahimu Lipumba jijini Dar es Salaam
Katika
mjadala huo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mathias Chikawe aliomba
suala hilo kupewa muda wa kufanyiwa uchunguza yakinifu na vyombo husika,
wakati Mwanasheria Mkuu George Masaju akitaka suala hilo lisijadiliwe
bungeni kwa kuwa tayari limeshafikishwa Mahakamani.
Kabla
ya mjadala huo Waziri Chikawe alisoma taarifa yake ya kile kilichotokea
kwenye vurugu hizo huku akieleza kuwa taarifa za uchunguzi wa ndani
ndizo zililishawishi jeshi la Polisi kuwaomba Cuf kutofanya maandamano
yao.
Waziri Chikawe amelieleza Bunge kuwa baada ya
taarifa za polisi kutolewa wafuasi wa Chama hicho hawakutaka kutii amri
hiyo, hivyo ili kunusuru uvunjifu mkubwa wa Amani ambao ungeweza kutokea
walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi hao wa CUF waliokuwepo.
“Nchi
yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na kanuni, haitakuwa busara kila
mtu kujifanyia mambo yake anayotaka bila kuzingatia sheria, nimeagiza
vyombo husika kuchunguza suala hili, na ikibainika kuwa polisi walitumia
nguvu kubwa watawajibishwa kwa mujibu wa sheria. Amesema Chikawe.
Baada
ya kauli hiyo ndipo Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipolieleza bunge
kuwa tayari kesi hiyo imeshafikishwa mahakamani, hivyo kujadili suala
hilo bungeni ni kukiuka sheria ya mgawanyo wa madaraka katika mihimili
ya dola,jambo ambalo lilipingwa na idadi kubwa ya wabunge.
Pamoja na hayo Spika Anna Makinda alitoa muda wa dakika
10 kwa wabunge kujadili suala hilo huku mbunge Tundu lissu akilaani
vikali kutokea kwa vurugu hizo na akitaka kuwajibika kwa Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu pamoja na waziri Chikawe kwa kuwa
vitendo vinavyoendelea vinashabihiana kabisa na kauli yake ya ‘wapigwe
tu’.
Aidha wabunge wengi wa kambi ya upinzani
wakichangia hoja hiyo kwa jazba walionyesha kukerwa na kuzilaani vurugu
hizo, huku wabunge wa CCM wakitaka kusimamiwa kwa sheria bila kupendelea
mtu yeyote.
Pamoja na hayo mtoa hoja ambaye ni Mbunge
na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia amesema kuwa suala
la Amani ya nchi ni suala la kitaifa na halitakiwi kuingizwa kwenye
siasa, hivyo aliwasihi wabunge kuwa makini na suala hilo
“Amani
na usalama wa nchi yetu ni kitu muhimu sana katika ustawi wa taifa
letu, kila siku tunashuhudia kuendelea kuporomoka kwa amani na usalama,
ninawasihi wabunge wenzangu, tunapojadili suala kama hili lazima tuweke
kando itikadi zetu, lengo likiwa kuliponya taifa, Amesema Mbatia.
Naye
Spika Makinda alihitimisha kwa kusema kuwa anaiagiza Serikali kufanya
uchunguzi kupitia vyombo vyake, pia bunge litachunguza sheria ambazo
zinatoa mwanya wa vurugu ili kudhibiti vitendo hivyo.
-