Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Segerea aapishwa na wakili binafsi
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa Migombani-Segera, Japhet Albert Kembo akiapishwa
leo jijini Dar es Salam. Picha na Immanuel Herman
Dar es Salaam. Baada ya kusubiri kwa muda wa wiki mbili ili
wajumbe serikali ya mtaa wa Migombani-Segerea waapishwe na mamlaka
husika bila mafanikio, wananchi wameamua kuwaapisha viongozi hao kwa
kutumia wakili binafsi.
Tukio hilo limetokea leo
asubuhi katika ofisi za Serikali za Mitaa zilizopo Segerea Mwisho ambalo
lilijumuisha kuapishwa kwa Mwenyekiti wa Mtaa, Japhet Albert Kembo
pamoja na wajumbe watatu ambao ni Rose Benard Mhagama, Nyangeto Flora
Justin na Ramadhan Rashid Seif.
Akizungumza baada ya
kuapishwa, mwenyekiti mpya wa mtaa huo amesema kuwa wananchi wamechoshwa
na danadana wanazopigwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala za
kutowaapisha viongozi waliowachagua ndiyo maana wamefikia hatua hiyo ili
kuwakumbusha kutekeleza majukumu yao kwa wakati.
“Wananchi
wanahitaji huduma kutoka kwa watu wanaowaamini lakini wanakosa imani
pale uongozi wa manispaa unaposhindwa kutekeleza majukumu yake kama
inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria. Wamemtafuta wakili ambaye amekuja
kulisimamia suala hili kisheria na ndiyo maana zoezi limefanywa
hadharani,” alisema Kembo.
Wananchi waliozungumza na
Mwananchi walisema kuwa hawaelewi kinachoendelea kwakuwa uchaguzi
ulifanyika kama kawaida pasipo dosari yoyote na matokeo yakatangwazwa
huku nafasi zote zikichukuliwa na wagombea kutoka Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema).
“Uchaguzi wetu haukuwa na
matatizo na ni miongoni mwa mitaa iliyotangaza matokeo muda mfupi baada
ya uchaguzi kufanyika lakini jambo la kushangaza ni kwamba viongozi wote
waliochaguliwa hawajaapishwa kama ilivyofanyika kwa wengine katika
manispaa hii wakati hakuna pingamizi lolote mahakamani linalozuia
uhalali wa waliochaguliwa,” alisema John Kandeo, mmoja wa wananchi
walioshuhudia kuapishwa kwa viongozi hao.
Akifafanua kuhusu matokeo ya uchaguzi uliofanyika
Desemba 14, mwaka jana, Kembo alisema kuwa walikuwa wagombea watatu
katika nafasi ya uenyekiti ambao ni yeye mwenyewe aliyepata jumla ya
kura 547, Uyeka Idd wa CCM aliyepata kura 273 na Erick Mchata wa
NCCR-Mageuzi aliyepata kura 205.
Zoezililivyokuwa
Muda
wa saa 05:00 asubuhi, wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya mawakili
ya Ame and Company, Idd Msawanga aliwasili katika ofisi za mtaa huo na
kupokelewa kwa kelele nyingi za wafuasi wa Chadema waliokuwa wakipaza
sauti zao kwa sauti kubwa za ‘Peoples…Power.’
Wakili
Msawanga alianza kwa kumuapisha mwenyekiti, peke yake, na baadaye
wajumbe hao watatu kwa pamoja na kuelezwa kuwa wajumbe wawili hawakuwepo
kutokana na matatizo ya kifamilia.
“Sheria ya uchaguzi
inaruhusu kufanya hivi na hata hao wajumbe wawili ambao hawapo kwa leo
watakaporudi nitawaapisha…ni suala la kutaarifiana tu,” alisema
Msawanga.