Zitto awavaa TRA, akerwa na Misamaha ya kodi
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema misamaha ya kodi imepanda kutoka Sh1.4 trilioni mwaka 2012/13 hadi Sh1.8 trilioni mwaka 2013/14, kueleza kuwa chanzo ni misamaha ya kodi katika miradi mikubwa.
Imesema kati ya
misamaha hiyo, Sh 676 bilioni zinatokana na misamaha ya kodi
inayotokana na Ongezeko la Thamani (VAT) na kufafanua kuwa hali hiyo
itapungua iwapo nchi itaanza kutumia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT).
Pia, imefafanua kuwa mpaka sasa
wafanyabiashara na kampuni kubwa zimefungua kesi katika mahakama ya
rufaa wakipinga kulipa kodi ambayo inafikia Sh1.7 trilioni.
Akizungumza
katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika ofisi ndogo za Bunge
jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa Mapato, Richard Bade
alisema, “Kuna ongezeko la Sh400 bilioni. Kuongezeka kwa misamaha hii
kunatuathiri kwa kiasi kikubwa.”
Alisema chanzo cha
kuongezeka kwa kiwango hicho kunachangiwa na misamaha ya kodi katika
miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara, miradi ya gesi na mafuta na
ujenzi wa daraja la Kigamboni.
“Katika miradi hiyo kuna
misamaha ya zaidi ya Sh300 bilioni. Pia katika Sh1.8 trilioni kuna
misamaha ya VAT ya Sh 676 bilioni na suala hili limefanyiwa kazi katika
sheria mpya ya VAT,” alisema.
Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Zitto Kabwe alishangazwa na kitendo cha sheria hiyo kutotumika
licha ya kuwa ilipitishwa na Bunge, jambo ambalo linasababisha Serikali
kukosa mapato.
“Kamati ya PAC italiwasilisha suala hili
kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kwa ajili ya hatua zaidi. Nadhani
kutotumika kwa sheria hii kuna watu nyuma yake ambao wananufaika na
misamaha hii,” alisema Zitto.