PAC yaagiza Wasira aondolewe kwenye nyumba anayoishi
Zitto Kabwe akisema jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
imeiagiza Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) kumwondoa katika nyumba ya bodi
hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen
Wasira kutokana na kuishi katika nyumba hiyo kinyume na taratibu.
Wasira
akiwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika alikuwa akiishi katika
nyumba hiyo inayomilikiwa na SBT iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa SBT, Henry Semwaza aliieleza Kamati ya PAC jana katika
kikao kilichofanyika kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam,
kuwa wamekuwa wakifanya jitihada za kuwasiliana na Wasira kuhusu
kuirejesha nyumba hiyo, lakini hakuna utekelezaji wowote unaofanyika.
“Mara
ya mwisho tulimwandikia barua mwaka 2012 kuhusu kuirejesha nyumba hiyo,
lakini bado hajairejesha na anaendelea kuishi katika nyumba hiyo,”
alisema Semwaza.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe akitoa
azimio la Kamati hiyo alisema, “Hapa hakuna msukumo mnaoufanya yaani
tangu mwaka 2012 mlipomwandikia barua mpaka sasa kimya. Tunaiagiza SBT
kumwandikia barua Wasira mkimtaka arejeshe nyumba na nakala ya barua
hiyo tuipate Jumatatu (Januari 19 mwaka huu).”
Alisema
kutokana na kuwapo kwa harakati za kutaka kubadili hati ya umiliki ya
nyumba hiyo, Zitto alisema, “Msajili wa Hazina kamati inakuagiza
uhakikishe umiliki wa nyumba hiyo unabaki kwa bodi ya sukari na si
vinginevyo.”
Zitto pia alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma amwandikie barua Katibu
Mkuu Kiongozi kuhusu uamuzi huo wa Kamati.
Pia, PAC
imeishauri Wizara ya Kilimo kuandaa sheria itakayounda Bodi ya Sukari
isiyokuwa na mgongano wa kimaslahi ili kutoa fursa ya kufanya uamuzi
tofauti na ilivyo sasa.