Hospitali ya Mbeya yateuliwa kupima ebola
Jengo la Hospitali ya Rufaa mkoani Mbeya. Picha na Maktaba
Mbeya. Hospitali ya Rufaa Mbeya (MRH), imeteuliwa rasmi
kuwa na maabara maalumu ya kuwapima watu watakaohisiwa kuwa na virusi
vya ugonjwa wa ebola.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali
hiyo, Mpoki Ulisubisya alisema hayo jana jioni alipozungumza mambo
mbalimbali kuhusu changamoto zinazoikabili hospitali yake.
"Ni
kweli Serikali imeiteua maabara yetu ya hospitali kuwa maabara maalumu
ya kupima virusi vya ebola nchini na kwa sasa maandalizi yote
yanakamilishwa na tutaanza kazi mwishoni mwa mwezi huu au mapema
Februari’’ alisema.
Kwa kipindi cha miaka mitano sasa,
Maabara ya Hospitali ya Rufaa Mbeya ni maabara ambayo imethibitishwa
kimataifa kwa ubora na kwamba vipimo vikitolewa kwenye maabara hiyo
vinakubalika hata nchi za Marekani na Uingereza.
Akizungumzia uboreshaji wa utendaji kazi amesema wafanyakazi kupitia kwa viongozi wao kwa sasa wameimarisha utendaji kazi.
Kuhusu
chumba cha kuhifadhi maiti kwenye Hospitali hiyo, Ulisubisya amesema
Serikali imempata mtu atakayejenga jengo kubwa la kuhifadhi maiti na
kuliboresha ili kuendeshwa kwa ubia katika hali ya usafi na kisasa
zaidi.
‘’Bila shaka unakumbuka , mfanyakazi wa chumba
cha maiti aliwahi kumweleza Waziri kwamba ukifariki dunia ukiwa Mbeya
maiti yako italazwa chini. Sasa Serikali imeamua kuchukua hatua ili
kuboresha nyumba hizo ingawa wahusika watatakiwa kutoa mchango
kidogo’’alisema.
Mapema mwaka jana, Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii Dk Seif Rashid wakati huo akiwa Naibu Waziri
alitembelea hospitali hiyo ambapo mfanyakazi wa Chumba cha maiti,
Vuruga P Vuruga alimweleza kiongozi huyo kwamba maiti zinalazwa mbili
mbili kwenye chumba chenye uwezo wa kuhifadhi watu sita.
Vuruga
amesema kutokana na kasi ya kufa, hivi sasa maiti zinalazwa chini na
kwamba hata Naibu Waziri angefariki akiwa Mbeya ajue maiti yake
ingelazwa chini.