Escrow yapangua mawaziri 13
Dar es Salaam. Hatimaye Rais Jakaya Kikwete amefanya
mabadiliko 13 kwenye Baraza la Mawaziri yaliyohusisha mawaziri nane,
manaibu watano, wakiwamo wapya wawili, ikiwa ni siku mbili kabla ya
kuanza kwa Bunge, na ndani ya saa 48 kama gazeti hili lilivyoripoti
Ijumaa iliyopita.
Rais pia aliwaapisha mawaziri wote 13
akiwamo waziri mpya wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe ambaye
alisababisha hafla hiyo kuchelewa kwa kuwa alikuwa akitokea Davos,
Uswisi.
Mabadiliko hayo, yanayoweza kuwa ya mwisho kwa
Rais Kikwete, yamefanyika ikiwa imesalia miezi sita kabla ya kuvunjwa
kwa Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.
Rais
amelazimika kufanya mabadiliko hayo baada ya mawaziri wawili, Profesa
Anna Tibaijuka na Profesa Sospeter Muhongo, kuondoka kutokana na
kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow,
ambayo pia imesababisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Eliackim Maswi kusimamishwa kazi, huku waziri wa zamani wa wizara hiyo,
William Ngeleja akivuliwa uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria.
Kwa
mujibu wa mabadiliko hayo, Kikwete amewaondoa mawaziri wawili wazoefu
kutoka Ofisi ya Rais, Steven wasira na Ofisi ya Waziri Mkuu, William
Lukuvi, kuwapangia wizara nyingine, huku akimhamishia Dk Mary Nagu
kwenye Ofisi ya Rais na Jenister Mhagama (Waziri Mkuu).
Akitangaza
mabadiliko hayo jana, Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue alisema mbunge
wa Kibakwe, George Simbachawene, ambaye alikuwa naibu wa wizara ya
Nishati na Madini kuanzia mwaka 2012 hadi 2014 na ambaye hadi jana
alikuwa naibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
ameteuliwa kumrithi Profesa Muhongo kwenye wizara hiyo tata ya Nishati
na Madini.
Simbachawene anakuwa waziri wa nne kushika
wizara hiyo tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani na anaingia
wakati Steven Masele, aliyekuwa naibu Waziri wa Nishati na Madini,
akiwa amehamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano). Nafasi ya Masele
imechukuliwa na mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage ambaye
ameteuliwa kwa mara ya kwanza.
Sefue alisema mbunge wa
Ismani, William Lukuvi, ambaye tangu mwaka 2010 amekuwa Waziri wa Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na Bunge), ameteuliwa kuziba nafasi ya
Profesa Tibaijuka ya uwaziri wa Kazi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Sura
nyingine ngeni kwenye baraza hilo, kwa mujibu wa Sefue, ni ya mbunge wa
Same, Anne Kilango Malecela, mmoja wa wazungumzaji wakubwa bungeni,
ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu.
Alisema
aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama
amepanda kuwa Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, nafasi iliyokuwa
ikishikiliwa na Lukuvi.
Nagu amehamia Uhusiano na Uratibu (Uwekezaji na Uwezeshaji) na Dk Harrison Mwakyembe anayehamia Afrika Mashariki (Uchukuzi).
Wengine
ni mwanasiasa mkongwe, Steven Wasira aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo
akitokea Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, wakati Samuel Sitta
anakwenda Uchukuzi akitokea Wizara ya Afrika Mashariki.
Manaibu
waziri wengine waliohamishwa ni Angella Kairuki, ambaye anakwenda
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akitokea Katiba na Sheria.
Ummy Mwalimu anakuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria akitokea Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).
Mabadiliko
hayo yamekuja ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio manane ya
Bunge, kutaka uteuzi wa Profesa Muhongo na Profesa Tibaijuka kutokana na
kuhusishwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Bunge
liliagiza mamlaka ya uteuzi kutengua nyadhifa hizo pamoja na wenyeviti
wa Kamati za Bunge, Nishati na Madini iliyokuwa chini ya Victor
Mwambalaswa.
Wengine waliotakiwa kuvuliwa nyadhifa za
Kamati kutokana na kashfa hiyo ni Andrew Chenge (Bajeti) na Kamati ya
Sheria na Katiba iliyokuwa chini ya William Ngeleja.
Akizungumzia
uteuzi huo, Kilango alisema: “Ninayajua matatizo ya walimu wenzangu na
kwa kushirikiana na wenzangu tutaweza kuyatatua, kikubwa ni
kushirikiana.”
Alisema kuwa kwa kushirikiana na Waziri wa Wizara hiyo watakuja na mipango na mikakati itakayolenga kuboresha sekta ya elimu.
Kwa
upande wake, Lukuvi alisema kuwa anafahamu changamoto zinazoikabili
wizara hiyo na atashirikiana na wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi.
“Ninachoomba
ni ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa kuwa ni imani yangu kuwa
tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja kazi itafanyika vizuri”alisema
Lukuvi
Naye Waziri wa Nishati na Madini George
Simbachawene alisema anatambua fika kuwa uchumi wa nchi yeyote
unategemea nishati hivyo atahakikisha sekta hiyo inawaletea manufaa
watanzania wote.
Simbachawene alisifu kazi ya Profesa Muhongo ana akasema atahakikisha anaikamilisha kwa kufikisha umeme kote vijijini.
Dk Slaa alonga
Akizungumzia
mabadiliko hayo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema:
“Hakuna jipya katika hayo mabadiliko, kwani tatizo lililopo ni mfumo na
si viongozi, Watanzania wasitegemee lolote kutoka kwao.
“Kitendo hiki cha watu wanafanya makosa halafu wanaachiwa wanajiuzulu na kubaki na sifa zao.
Kama taifa hatuwezi kusonga mbele. Tunahitaji kuwashughulikia wanaorudisha nyuma maendeleo ya nchi.”
Katibu
huyo aliongeza kusema: “Wahalifu bado wanapata fursa ya kukaa na
kujadiliana na rais, hii haikubaliki. Washabainika wamefanya makosa kwa
nini wasiwajibishwe mapema?”
TBC yawa kero
Shirika
la Habari Tanzania (TBC) jana liliwakera Watanzania waliokuwa
wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya mabadiliko madogo ya Baraza
la Mawaziri.
Mabadiliko hayo yalikuwa yakitangazwa na
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kutoka Ikulu jijini Dar es
Salaam ambapo yalihusisha mawaziri na manaibu mawaziri.
Matangazo
hayo yalikuwa yakikatika mara kwa mara na wakati mwingine yakionyesha
picha bila sauti jambo lililokuwa kero kwa watazamaji.
Hata
hivyo, mkurugenzi mtendaji wa TBC, Clement Mshana alipotafutwa
kuzungumzia matatizo yaliyojitokeza, alisema kwa kifupi “mimi sijui na
nipo mkoani ninaendelea kufuatilia matangazo ya mabadiliko hayo” na
kukata simu.
Katika hatua ya uapishwaji wa mawaziri na
manaibu mawaziri hao ulioanza Saa 12.14 jana jioni muda mfupi baada ya
kumalizwa kutangazwa matangazo yaliendelea vizuri.
Hali
hiyo si ya kwanza kutokea kwani katika mijadala kadhaa ya mikutano ya
Bunge matangazo yamekuwa yakikatika jambo lililokuwa likilalamikiwa na
baadhi ya wabunge na wananchi kwa kukoseshwa fursa ya kutazama muhimili
huo wa ukiendelea na shughuli zake.
Imeandikwa na; Goodluck Eliona, Ibrahim Yamola na Elizabeth Edward.