CCM kuwabana makada escrow
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Dar es Salaam. Kamati Ndogo ya Maadili ya
CCM leo inaketi kutoa hatima ya makada wa chama hicho waliotajwa
kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kikao
hicho kitakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM - Bara, Philip Mangula
kama ilivyoagizwa na Kamati ya CCM iliyokutana wiki iliyopita.
Walioitwa
katika kamati hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Mkuu
(NEC) na Kamati Kuu ya CCM (CC) pamoja na wajumbe wa NEC, Andrew Chenge
(Mbunge wa Bariadi Magharibi) na William Ngeleja (Sengerema).
Kwa
kuwa uamuzi wa CC unasisitiza utekelezaji wa maazimio ya Bunge, kwa
vyovyote unamlenga pia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo ambaye mpaka sasa amewekwa kiporo.
Kamati Kuu
iliyofanyika Januari 13, mwaka huu Zanzibar iliazimia kuwa hatua za
kimaadili zichukuliwe kwa wote waliohusika na ukiukwaji wa maadili
kwenye sakata la Escrow ambao wako kwenye vikao vya uamuzi vya CCM.
Pia
kikao hicho kiliitaka Serikali kuendelea kutekeleza maazimio ya Bunge
kuhusu sakata hilo ambalo lilikiweka chama hicho katika wakati mgumu
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika hivi karibuni.
Kutokana
na azimio hilo, Ngeleja, Profesa Tibaijuka na Chenge wanakabiliwa na
adhabu ya kuvuliwa nyadhifa walizonazo ndani ya vikao vya amuzi vya CCM.
Makada
hao walitajwa bungeni kuwa walipokea mamilioni ya shilingi kutoka
katika akaunti ya VIP Engineering inayomilikiwa na James Rugemalira.
Chenge na Profesa Tibaijuka walipokea Sh1.6 bilioni wakati Ngeleja
alipokea Sh40.4 milioni.
Hata hivyo, Ngeleja anayetajwa
kutaka kuwania urais anaweza kukumbwa na adhabu nyingine iwapo
atabainika kuwa alikwenda kinyume na adhabu aliyopewa pamoja na wenzake
watano ya kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka
kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo.
Adhabu
hiyo aliyopewa Ngeleja pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, January Makamba, Bernard Membe na
Stephen Wasira inamalizika Februari mwaka huu na baada ya hapo
itafanyika tathimini kuona kama walizingatia masharti ya adhabu zao.
Kwa mujibu wa taarifa ya CC, ambao hawakuzingatia masharti wataongezewa adhabu.
Tayari
uteuzi wa Profesa Tibaijuka umeshatenguliwa na sasa Rais Kikwete
anasubiriwa kumtangaza mrithi wake na kumalizia ‘kiporo’ cha Profesa
Muhongo.
Maazimio ya Bunge
Azimio
la pili la Bunge lilitaka Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua
uteuzi wao.
Kati ya hao wote, mtu pekee ambaye mpaka sasa bado hajachukuliwa hatua yoyote ni Profesa Muhongo.
Jaji
Frederick Werema ameshajiuzulu nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Eliakim Maswi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini alisimamishwa kazi na Bodi ya Tanesco imeshaundwa mpya.
Bunge
pia liliazimia kuwa Chenge na Ngeleja ambao walikuwa wenyeviti wa
kamati za Bajeti na ile ya Katiba, Sheria na Utawala, mtawalia, kuvuliwa
nyadhifa zao, jambo ambalo bado linasuasua.
Sakata la
Escrow pia linaweza kuwaathiri wanasiasa hao kwa upande mwingine kwa
kuwa wote bado wana nia ya kutetea nafasi zao za ubunge katika majimbo
yao.