Madiwani wataka mkurugenzi asimamishwe
Moshi. Baraza la Madiwani Halmashauri ya
Manispaa ya Moshi, limepitisha maazimio ya kumtaka Rais Jakaya Kikwete,
kumsimamisha kazi kwa muda mkurugenzi wa manispaa hiyo, Shaban Ntarambe.
Mbali
na kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi huyo, lakini baraza hilo limeunda
kamati ya madiwani wanne kuchunguza mchakato mzima wa kuhamisha miliki
ya kiwanja kinachodaiwa ni cha Umma. Maazimio hayo yaliyosomwa jana
alasiri baada ya kumalizika kwa kikao maalumu cha baraza hilo
kilichoitishwa mahsusi kujadili ajenda moja tu ya umiliki wa kiwanja
hicho kilichoibua mgogoro.
Wakati halmashauri ikidai
kukimiliki kiwanja hicho kilichopo ofisi za kata ya Mawenzi, Jumuiya ya
Wazazi ya CCM na Mawenzi Sports Club nazo kwa nyakati tofauti zimeibuka
na kudai ni wamiliki.
Akisoma maazimio hayo, ambayo
baadaye yalisahihishwa na Meya, Jaffar Michael na msoma maazimio, Sophia
Mshiu alisema theluthi moja ya madiwani ndiyo walioonyesha kutokuwa na
imani na Ntarambe.
Alisema madiwani hao ni wale
wanaotokana na Chadema na kwamba wamemtaka Rais kumsimamisha kazi
mkurugenzi huyo ili kupisha uchunguzi utakaofanywa na kamati ya madiwani
hao wanne.
Madiwani wanaounda kamati hiyo ni Dk
Charles Mmbando (Naibu Meya), ambaye atakuwa mwenyekiti na wajumbe
Priscus Tarimo, Raymond Mboya na Peter Kimaro.
Pia, kamati hiyo itawahusisha wataalamu watatu wa
halmashauri, ambao ni Erick Mapunda, Ofisa Utumishi, Anitha Bureta,
Afisa Ushirika na Peter Mbwambo, Ofisa Elimu.
Baraza
hilo pia limeiagiza ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kuweka zuio
la kisheria katika kiwanja hicho, ambacho zamani kilikuwa kikitumika
kama ofisi ya Shule ya Sekondari ya Kibo.
Baada ya
kusomwa kwa maazimio hayo, Meya alisema ni vyema kumbukumbu ikawekwa
sawa kuwa theluthi mbili ya madiwani wote ndiyo waliokosa imani na
mkurugenzi na wanne wa CCM walipinga.
Katibu wa
Madiwani wa CCM, Michael Mwita alisimama na kuungwa mkono na wenzake
kuwa wao hawakuunga mkono azimio la kuwamwajibisha mkurugenzi, kwa vile
halikufuata sheria.
Kabla ya kufungwa kwa kikao hicho,
mkurugenzi aliomba nyaraka zote alizoziwasilisha katika kikao hicho
zisichukuliwe kuwa ndio utetezi wake bali yalikuwa ni mawasiliano ya
wataalamu wa Serikali.
Akifunga kikao hicho, Meya
alisema amewaelewa madiwani hao na kusema moja ya hadidu za rejea za
kamati hiyo itakuwa kuchunguza mchakato mzima wa umiliki wa kiwanja
hicho.