Okwi hatihati kuivaa Mbeya City
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Simba,
Emmanuel Okwi jana alilazimika kurudishwa tena Hospitali ya Taifa
Muhimbili kufanyiwa kipimo cha CT scan kujiridhisha iwapo ataweza
kucheza kesho mechi dhidi ya Mbeya City.
Okwi aliumia
dakika ya 62, na kupoteza fahamu wakati wa mchezo kati ya Simba dhidi ya
Azam juzi mechi iliyomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema
wamelazimika kufanya vipimo tena ili kujiridhisha kutokana na hali
aliyokuwa nayo uwanjani jana (juzi).
“Hali ya Okwi siyo
mbaya ingawa tunahitaji kujiridhisha kwa kumfanyia uchunguzi zaidi kama
kwa hali aliyonayo ataweza kucheza kwenye mechi ya Jumatano dhidi ya
Mbeya City au la,” alisema Daktari Gembe aliyeambatana na mchezaji huyo
Muhimbili jana asubuhi.
Kufuatia tukio hilo, uongozi wa Simba ulikutana na kujadili kitendo hicho huku ukijipanga kutoa tamko.
Katibu
mkuu wa timu hiyo, Steven Ally alisema kitendo alichofanyiwa mchezaji
wao kwenye mechi hiyo siyo cha kiungwana na kusisitiza kuwa, wakati
wowote kuanzia sasa uongozi utatoa tamko kuhusu tukio alilofanyiwa
mchezaji wao.
Gazeti hili lilifikia makao makuu ya
Simba, Kariakoo na kushuhudia mashabiki wa timu hiyo wakiwa vikundi
vikundi wakijadili kitendo alichofanyiwa Okwi na wakautaka uongozi
kutolifumbia macho suala hilo.
Wakati huohuo.
African Sports imejiweka katika mazingira mazuri ya kupanda Ligi Kuu
msimu ujao baada ya kuichapa Majimaji kwa bao 1-0 jana kwenye Uwanja wa
Mkwakwani, Tanga.
Bao pekee la African Sports lilifungwa dakika ya 70 na Ramadhani Msheli akiunganisha kwa umakini krosi ya James Mendi.