Wamchangia Jaji Warioba nauli akatoe somo la Katiba
Jaji Warioba
Moshi. Wananchi wa Jimbo la Vunjo mkoani
Kilimanjaro wamechanga Sh200,000 za nauli ya Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili aweze kufika jimboni humo
kutoa somo la Katiba.
Fedha hizo zilitolewa juzi na
kukabidhiwa kwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia wakati
akihutubia mikutano ya hadhara kwa nyakati tofauti katika miji ya Himo
na Moshi Mjini kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kuwaamini wagombea
wa Ukawa na kuwapa ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano ya fedha hizo, Katibu wa Umoja wa Wanawake wa
NCCR-Mageuzi, Getrude Pwila alisema kama hazitatosha kwa nauli ya Jaji
Warioba, wako tayari kuchangishana kuongeza.
“Tunataka
tuelimishwe hii Katiba Inayopendekezwa kwa sababu hatuko tayari kuipigia
kura kwa sababu hatuielewi, hatujaiona wala kuisoma na kuielewa,”
alisema Pwila kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo.
Katibu
huyo, alimwomba Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa, amwombe Jaji
Warioba kwenda katika jimbo hilo kuendesha kongamano kama alivyofanya
katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam na wao wako tayari kumgharimia.
“Leo
tunayo nusu ya nauli (Sh200,000) akikubali tuko tayari kuchangia na
kujazia Sh200,000 nyingine na tunakukabidhi shati la kitenge kama
alilokuwa anavaa Mandela (Nelson) ili ukamkabidhi,” alisema.
Pwila alisema wananchi wa Vunjo wanamchukulia Jaji Warioba kama Mandela wa Tanzania, ndiyo maana wamempatia shati hilo.
Jaji Warioba alipoulizwa kuhusu maombi hayo, alisema hajayapokea na hajui lolote.
Katika
mkutano huo, pia wananchi walimkabidhi Mbatia suti mpya ambayo wanataka
aivae atakapokwenda bungeni kuapishwa akiwa mbunge wa jimbo hilo.
Mbatia awasha moto
Kwa
upande wake, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alimtaka
Rais Jakaya Kikwete kutekeleza masuala aliyokubaliana na viongozi wa
vyama vya siasa kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) mwaka jana.
Mbatia
alisema moja ya makubaliano hayo yalikuwa ni kufanya mabadiliko ya
Katiba ya sasa ili kuruhusu kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi ili
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba uwe wa huru na wa haki.
Vilevile,
mabadiliko hayo yangeruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi, matokeo ya
uchaguzi wa rais kuhojiwa mahakamani, mshindi wa urais kupata zaidi ya
asilimia 50 ya kura na kuahirisha kura ya maoni hadi mwaka 2016.
Akihutubia
mkutano katika Mji mdogo wa Himo, Mbatia alisema mwaka huu hawako
tayari kuona Uchaguzi Mkuu unavurugwa na wasimamizi wanaopokea maelekezo
ya Serikali. “Ninamwomba Rais asimamie maridhiano haya kwa masilahi
mapana kwake na kwa nchi yetu kabla miezi yake hii minane aliyobakia
nayo haijawa michungu kwake,” alisema.
Mbatia alisema
makubaliano hayo yalikuwa ni ya utu na kwamba kwa utafiti alioufanya
anaona giza mbele na hakuna uwezekano wa kupitishwa kwa Katiba
Inayopendekezwa kwa vile haina maridhiano. “Naomba kama inawezekana wote
tuseme Katiba Inayopendekezwa hapana, hapana, hapana! Badala ya
kulumbana tuangalie kesho, hatutaki uchaguzi mkuu wa kumwaga damu,”
alisisitiza Mbatia.
Mwanasiasa huyo aliyetangaza nia ya
kuwania ubunge katika Jimbo la Vunjo, aliishauri Serikali
iwakukutanishe haraka viongozi wa vyama vya siasa kutafuta maridhiano ya
kitaifa kwa kuwa Ukawa hawako tayari kuigeuza nchi kuwa ya machafuko.