Muhongo aachia ngazi
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akitangaza kujiuzuru nafasi yake ya Uwaziri, kutokana na kasha ya uchotwaji wa fedha katika akauti ya Tegeta escrow, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam, jana. Picha na Emmanuel Herman
Dar es Salaam. Dakika 50 zilimtosha Profesa
Sospeter Muhongo kujieleza kwa urefu wakati akitangaza uamuzi wake wa
kujiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini akisema “anataka nchi isonge
mbele” baada ya kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta
Escrow kutikisa Taifa.
Muhongo, ambaye aliteuliwa na
Rais Jakaya Kikwete kuwa mbunge Mei 3, 2012 na siku nne baadaye
kuteuliwa kuwa waziri, alitangaza uamuzi huo jana saa chache kabla ya
kutangazwa Baraza la Mawaziri lenye mabadiliko 13, ikiwa ni kuziba
nafasi za mawaziri wawili- mwingine ni Profesa Anna Tibaijuka-
waliotajwa kwenye kashfa hiyo. Mawaziri hao waliapishwa jana baada ya
kutangazwa.
“Sasa ni lazima kila kitu kiwe na tamati,
na ninadhani mimi ninaweza kuwa sehemu ya suluhisho la malumbano
yasiyokuwa na mwisho,” alisema Profesa Muhongo mbele ya waandishi wa
habari waliojaa kwenye chumba cha mikutano cha Wizara ya Nishati na
Madini na ambao walimsubiri kwa takriban saa moja na nusu.
Profesa
Muhongo aliingia kwenye chumba hicho na kabla hata hajakaa vizuri
akasema utaratibu wa kujitambulisha hautakuwapo kutokana na idadi ya
watu waliopo.
“Sasa ndugu zangu waandishi wa habari na
wageni waalikwa nadhani kwa muda mrefu sana hamjanisikia naongea jambo
lolote kuhusu mambo ya escrow baada ya kutoka bungeni,” alisema.
Kama
ambavyo amekuwa akijieleza kwa staili ya kusifia kazi aliyofanya kwa
mafanikio, Profesa Muhongo alianza hotuba yake ya kutangaza kujizulu kwa
kuzungumzia mafanikio yake kwa muda wa miaka miwili na nusu aliyokaa
kwenye wizara hiyo, ambayo sasa imepoteza mawaziri wanne katika Serikali
ya awamu ya nne.
Akizungumzia uamuzi wake wa
kujiuzulu, mbunge huyo wa kuteuliwa alisema ameamua kuchukua uamuzi huo
ili kuipa nafasi Serikali iwatumikie wananchi badala ya kushinda kwenye
vikao visivyokuwa na mwisho kujadili sakata hilo.
“Chama
changu cha Mapinduzi ni lazima kiendelee kuwatumika wananchi hasa wale
walio maskini kuliko kila siku CCM kukaa kwenye vikao wanaongelea suala
la escrow,” alisema.
Alisema hata Bunge haliwezi
kuendelea kuongea kitu ambacho hakina mwisho kwa sababu alipozungumza
bungeni alitoa tamko la Serikali.
Alisema hakutaka
kulizungumzia suala la escrow baada ya vikao vya Bunge kwa kuwa alidhani
siyo busara kuendelea kulumbana wakati Watanzania wanataka kupumzika.
Aliongeza kuwa baada ya Rais Kikwete kuzungumzia suala hilo, alidhani
kuwa ingekuwa mwisho, lakini ameona mjadala unaendelea.
“Na
leo navyotaka kuliongea hili, nadhani kama tunalipenda Taifa letu na
kama tunataka kufuta umaskini basi mjadala wa escrow tutakuwa tumeiachia
mahakama au watu wengine wanaohusika,” alisema.
Alieleza
kuwa mkataba wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na escrow ulikuwa
Mei, 1995 wakati huo alikuwa akifanya kazi ya utafiti nchini Ujerumani.
“Akaunti
ya escrow imefunguliwa mwaka 2006, ndugu zangu mwaka huo sikuwa nchini
nilikuwa Pretoria nina majukumu ya kusimamia maendeleo ya sayansi kwenye
bara la Afrika. Kwa hiyo kuanzishwa kwa IPTL nchini sikuwapo,
kuanzishwa kwa escrow sikuwapo, lakini nikapewa majukumu ambayo
yananifanya nisogelee IPTL na escrow,” alisema Profesa Muhongo.
Bunge
halikumtuhumu Profesa Muhongo kuwa alichukua rushwa, lakini alitumia
muda mwingi jana kueleza kuwa hajawahi kupokea na hawezi kupokea rushwa.
Alisema
aliisoma mara nne ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikalia
(CAG) iliyochunguza sakata la escrow na aliona hakuna sehemu yoyote
anahusika au ana hatia.
Alifafanua kuwa hata baada ya
watu kugawana fedha za escrow kutoka kwenye mabenki yanayotajwa, hakuwa
na nyaraka zozote zinazoonyesha kuwa alipewa fedha hizo.
“Nendeni
kwenye benki ambazo zinahisiwa zilichukua fedha za escrow, msichukue
maelezo ya mitandaoni ambako mtu anaandika akaunti feki tu anasema sijui
mtu fulani, hapana nendeni benki. Sijachukua senti popote,” alisema.
“Na
isitoshe ndugu zangu Watanzania haiwezekani uanze kuiba kwenye umri
kama wa kwangu hivi, nadhani mwizi anaanza zamani,” alisema Profesa
Muhongo mwenye umri wa miaka 61 huku akiacha kicheko ukumbini.
Alieleza
kuwa hata katika nchi za Ujerumani, Ufaransa ambako alitunukiwa nishani
ya Napoleon na China hakuna hata siku moja alikopa au kuiba fedha za
utafiti.
“Sijawahi kuiba hela mahali popote pale na
wote waliofanya kazi na mimi wananielewa mimi siingiliki kwa rushwa.
Haiwezekani unipatie rushwa na kama kuna Mtanzania amenipatia rushwa
ajitokeze kama yupo,” alisema.
“Na siyo rahisi wewe kunipatia rushwa, haiwezekani. Huenda watu wengine hali kama hiyo hawaipendi.”
Bunge
lilimuingiza Profesa Muhongo kwenye kashfa hiyo kwa kumtuhumu kuwa
alishindwa kushughulikia vizuri sakata la escrow kwa makusudi au uzembe
na kusababisha Taifa kupoteza fedha kutokana na kodi. Pia, alidaiwa
kushindwa kuhakiki ununuzi wa hisa za IPTL kwa kuwa nyaraka zilizotumika
kuuza hisa kutoka Mechmar Corporation na Piper Links zilikuwa za
kughushi, uhakiki ambao Bunge liliambiwa kuwa unatakiwa ufanywe na
waziri husika.
Kuhusu tuhuma kwamba waziri huyo ndiye
aliwakutanisha watu waliochota fedha za escrow, Profesa Muhongo alisema
kama ingekuwa ni kweli yeye ndiye angekuwa wa kwanza kupewa fedha za
shukrani.
Katika sakata hilo, zaidi ya Sh306 bilioni
zilichotwa kwenye akaunti hiyo iliyofunguliwa Benki Kuu (BoT) kuhifadhi
fedha ambazo Tanesco ilitakiwa kuilipa IPTL baada ya pande hizo mbili
kuingia kwenye mzozo wa kiwango cha tozo ya umeme unaozalishwa na IPTL
na kufungua kesi.
Uamuzi wa kesi hiyo ulitaka pande
hizo mbili zikokotea upya viwango hivyo, lakini fedha hizo ikachotwa
mwishoni mwa mwaka juzi na kulipwa kwa Kampuni ya Pan African Power
Solutions ambayo ilinunua hisa zote za IPTL na baadaye baadhi ya fedha
hizo kugawanywa kwa vigogo wa Serikali, mawaziri wa zamani, watendaji
waandamizi wa Serikali na viongozi wa kidini.
Kabla ya
kuchotwa kwa fedha hizo, Mamlaka ya Mapato (TRA) iliiandikia BoT kutaka
isifanye malipo hadi ikate kodi ambayo Tanesco ilitakiwa ilipe, lakini
Mwanasheria Mkuu wa wakati huo, Frederick Werema alishauri fedha hizo
zisikatwe. TRA pia ilibaini kuwapo wa udanganyifu wa kiwango cha kodi
kilichotozwa wakati wa kuuza hisa za IPTL kwa kampuni ya PAP na hivyo
kulikosesha Taifa mapato.
Tayari Anna Tibaijuka,
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amevuliwa
madaraka hayo wakati Werema amejiuzulu wadhifa wake wa Mwanasheria Mkuu,
huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi
amesimamishwa kwa uchunguzi. Maofisa waandamizi watano wa Tanesco, TRA
na BoT wamefikishwa mahakama kwa tuhuma za kupokea rushwa inayofikia
jumla ya Sh1.9 bilioni.
Pia wenyeviti wanne wa kamati za Bunge, Andrew Chenge,
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, William Ngeleja, aliyekuwa Waziri wa Nishati
na Victor Mwambalaswa aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini na wakati huohuo mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
Tanesco, wamejiuzulu.
Kuhusu kuitwa kwake kuja kuwa
mbunge na baadaye waziri, Profesa Muhongo alisema alilazimika kuiacha
kazi aliyokuwa anaifanya mjini Pretoria, Afrika Kusini.
“Nilijua
ninaitwa kuja kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa hili ya 2025
inayosema kuwa ukifika mwaka huo umaskini uwe umetoweka nchini, alisema.
Kiini kashfa ya escrow
Profesa
Muhongo alisema hoja ya escrow imebeba mambo mengi ndani yake, ambapo
sasa imeibuka mivutano ya kisiasa isiyokuwa na mwisho huku wananchi
wakionekana kuchoshwa na hali hiyo.
Alikumbusha kuwa
mwaka 1969 wakati mtu wa kwanza kutua mwezini, Mwasisi wa Taifa, Julius
Nyerere alisema wakati wengine wanatua mwezini, sisi twende vijijini.
“Mimi nilikuwa natekeleza wazo la Nyerere,” alisema.
Alisema
kwa muda wote aliokuwa wizarani hapo alitumia muda mwingi kupeleka
umeme vijijini na kwamba ifikapo Juni mwaka huu vijiji 1,5000 vitakuwa
na umeme.
“Ndiyo kazi niliyoisimamia kwa miaka miwili na nusu niliyokaa hapa wizarani,” alisema.
Aliongeza
kuwa wakati nchi za Afrika zinapata uhuru, baadhi ya viongozi walitaka
kujenga barabara zitakazounganisha Afrika nzima, lakini yeye amejenga
barabara za umeme.
“Kuna watu wana mambo yao binafsi,
Watanzania wamechoka, Serikali imechoka, CCM imechoka na hata mimi
nimechoka… ndani ya escrow kuna wivu, kuna chuki, kuna fitina. Kama
kweli dira yetu ya maendeleo miaka 10 ijayo tunataka Tanzania lisiwe
taifa la umasikini, hatuwezi kuendelea kwa kuendeleza vitu hivi vinne
ambavyo ni siasa, biashara, ubinafsi, wizi, chuki na fitina lazima
tufike mwisho,” alisema.
“Ambaye anaweza kuwa suluhisho
la kufika mwisho ni mimi hapa. Tunalumbana na mambo ya escrow, lakini
mimi ninayezunguka mikoani kukagua miradi ya maendeleo, nilikuwa Tabora,
Shinyanga, Simiyu na Mara, sikuulizwa kuhusu escrow.
“Baada
ya kutafakari na kujadiliana na wakubwa zangu, lazima taifa langu liwe
juu ya kazi niliyopewa, lazima maslahi ya taifa hili yawe ni muhimu
zaidi kuliko cheo cha mtu mmoja kwa maneno mengine ndugu zangu walioko
vijijini wanataka umaskni uwatoke.
“Viwanda vinataka
kupata umeme, vijana wanataka kupata ajira na ndiyo maana nimejiona ni
sehemu ya suluhisho na ndiyo maana nimemwaomba rais niachane na nafasi
ya uwaziri ili taifa lisonge mbele hakuna sababu ya kuendelea kulumbana.
Tunapoteza muda na rasilimali zetu.”
Aliongeza kusema:
“Uamuzi nimeufanya kwa sabahu nataka Serikali ibaki inashughulikia
matatizo ya wananchi badala ya Serikali kuu kushughulikia escrow.
Naachia ngazi ya uwaziri kwa sababu nataka chama changu CCM kiendelee
kutatua kero za wananchi badala ya kukaa vikao kujadili suala la escrow,
nataka bungeni niwe mbunge wa kawaida na hii itatoa fursa kwa Bunge
letu kutumia muda vizuri na rasilimali.
“Naachia hii
kwa sababu Watanzania wamechoka, escrow haifuti umaskini na ninyi
waandishi wa habari leo anzeni kuwapatia habari zao na mimi nina familia
familia yangu haiwezi kuamka inakuta escrow, escrow kuna watu wanasoma
watashindwa kusoma.”
Zitto na Kafulila
Akizungumzia
uamuzi wa kujiuzulu, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema: “PAC
tulichokuwa tunakitaka ni kuona utekelezaji tu wa maazimio ya Bunge na
wala hatuna chuki na mtu yeyote… na PAC tukifika Dodoma tutapokea
taarifa rasmi ya utekelezaji wa maazimio hayo.”
Aliongeza:
“Tumeshuhudia watu wamefikishwa mahakamani, lakini bado ni vidagaa,
tunataka wakubwa wapelekwe mahakamani. Hiyo ni busara aliyochukua ambayo
ninaamini itasaidia harakati za kujenga demokrasia yenye uwajibikaji na
kulinda heshima ya Bunge na maazimio yake.”
Zitto,
ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema: “Muhongo si
mmoja tu kati ya waliotajwa kwani tumeona Tibaijuka, Werema na sasa
Muhongo hivyo kama kamati tutakaa na kujadili utekelezaji wa maazimio
hayo manane ya Bunge. Hata Ngeleja, Chenge Spika (Anne Makinda)
tumesikia amekwishawaandikia barua ya kamati zao kufanya uchaguzi.”
Mwasisi
wa sakata hilo bungeni, David Kafulila alisema: “Kujiuzulu ni jambo la
busara na kwa kiongozi inaonyesha uwajibikaji na ni heshima lakini
Profesa Muhongo alichelewa sana hivyo kuwapo kwa taswira tofauti kwa
taifa na wananchi.”
“Hakuna serikali duniani
iliyoshindana na Bunge na Serikali ikashinda. Hii ni changamoto kwa
watendaji kuwa Bunge halishindani na Serikali hata siku moja, Muhongo
alikuwa anapima mabavu ya Bunge sasa ameshindwa.”
Kafulila
alisema alibainisha mambo matatu ambayo yalitakiwa kufanyika kuwa;
waliohusika kujiuzulu au kufukuzwa kazi, kurudisha fedha kama ilivyokuwa
katika kashfa ya Akaunti ya Benki ya Madeni ya Nje (EPA) pamoja na
kufikishwa mahakamani.
Wasomi
Mtaalamu
wa Maendeleo na Utawala wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Emmanuel
Mallya alisema: “Ni uamuzi mzuri na wakati mwingine unawajibika hata
kama hukukosea wewe.”
“Amefanya jambo la busara kwani
watu walikuwa wameanza kupoteza imani naye na amechelewa kuchukua uamuzi
huo na hii ni hulka ya jamii yetu tunayotoka.”
Profesa
George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema: “Amechukua uamuzi
sahihi lakini amechelewa. Viongozi wetu wanatakiwa kuiga dhana ya
uwajibikaji, siyo hadi maneno yanasemwa hadi yasiyotakiwa.”