Ufisadi mpya kutikisa Bunge
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe
Kashfa
nyingine zinazotarajiwa kuibuliwa kesho ni, ufisadi katika gharama za
ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na uuzaji wa nyumba ya Bodi ya
Korosho.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana na
kuthibitishwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe zilisema kuwa, tayari
kamati hiyo imepokea ripoti ya ukaguzi huo ambayo inaonyesha ufisadi wa
kutisha katika maeneo hayo matatu na mengineyo.
Masuala
hayo matatu pia yaliibuka wakati wa vikao vya kamati za Bunge
vilivyomalizika Dar es Salaam wiki iliyopita, huku bodi ya korosho
ikibanwa kuhusu nyumba yake aliyouziwa Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM),
Silvestry Koka.
Kwa mujibu wa habari hizo, ripoti hiyo
inayoonyesha jinsi ufisadi wa kutisha ulivyofanywa katika ujenzi wa
jengo la (VIP Lounge) na Serikali inadai ilitumia Sh12 bilioni
kulijenga, lakini mthamini wa majengo ya Serikali ameeleza kuwa jengo
hilo lina thamani ya Sh3 bilioni.
Katika suala la
misamaha ya kodi, PAC imepokea taarifa kutoka kwa CAG ikionyesha kuwa
misamaha hiyo iliyokuwa imefikia Sh1.5 trilioni mpaka Juni 2013, lakini
baada ya mwaka moja misamaha hiyo imeongezeka hadi Sh1.8 trilioni mpaka
Juni 2014.
“Kwa mwaka moja tu, misamaha ya kodi
imeongezeka kwa zaidi ya Sh300 bilioni. Kiasi hiki ni kama escrow fulani
(Fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, Sh306 bilioni),” chanzo cha habari
kilidokeza.
Katika vikao vya kamati hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilieleza kuwa misamaha ya kodi imepanda kutoka Sh1.4 trilioni mwaka 2012/13 hadi Sh1.8 trilioni mwaka 2013/14, chanzo kikiwa ni misamaha ya kodi katika miradi mikubwa. Ilisema kati ya misamaha hiyo, Sh676 bilioni zinatokana na misamaha ya kodi inayotokana na Ongezeko la Thamani (VAT) na kuwa hali hiyo itapungua iwapo nchi itaanza kutumia Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia,
TRA ilifafanua kuwa mpaka sasa wafanyabiashara na kampuni kubwa
zimefungua kesi katika mahakama ya rufaa wakipinga kulipa kodi ambayo
inafikia Sh1.7 trilioni.
Mvutano mwingine unaotarajiwa kuibuliwa katika ripoti hiyo ni uwasilishwaji wa utata wa uuzwaji wa nyumba ya Bodi ya Korosho.
Awali,
hati ya nyumba hiyo ilikuwa ya Taasisi ya Kilimo Tanzania ambayo
ilifutwa mwaka 1963, kabla ya mtu mwingine kuibadilisha hati na kuiuza
kwa Koka mwaka 2011.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mudhihir Mudhihir alisema Koka aliuziwa nyumba na taasisi hiyo ambayo haikuwa mmiliki halali.
Alisema
nyumba hiyo iliuzwa kwa Sh300 milioni na katika juhudi za bodi
kufuatilia taratibu za kuirudisha, ikagundulika kuwa hati
imeshabadilishwa, kusisitiza kuwa uuzwaji wa nyumba hiyo ulifanyika
kimakosa bila kufuata sheria na taratibu.
Juzi Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alikaririwa akiwataka wananchi kutoa
taarifa kuhusu makusudio ya kuuza nyumba za Serikali na mashirika ya
umma, kutokana na madeni mbalimbali ili ziweze kukombolewa kabla ya
kuuzwa.