Barua kumtaka Wasira aachie nyumba ya SBT yatua rasmi PAC


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akiwahoji wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jana wakati wa vikao vya kamati za Bunge vinavyoendelea kwenye Ofisi Ndogo za Bunge Dar es Salaam. Kushoto ni wajumbe wa kamati hiyo, Alhaji Ismail Aden Rage na Ester Matiku. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Agizo la kumwandikia barua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira ya kumtaka kurejesha nyumba ya bodi hiyo, limetekelezwa baada ya barua hiyo kuwasilishwa kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Agizo hilo lilitolewa na kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Zitto Kabwe kwa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) ikitaka Wasira arejeshe nyumba hiyo.
“Bodi tuliiagiza imwandikie barua Wasira na nakala ya barua hiyo watuletee leo (jana), tayari wameileta hivyo tunasubiri utekelezaji,” alisema Zitto na kuongeza: “PAC haina ugomvi na Wasira bali Serikali ambayo inatakiwa kumlipia kodi waziri wake na siyo kukaa katika nyumba ya umma bila kulipia kodi.”
Januari 16, mwaka huu, PAC ilikutana na Bodi ya SBT na iliieleza kamati kwamba tangu 2010, Wassira amekuwa akiishi katika nyumba hiyo iliyoko Masaki na wakimtaka kuirejesha hakukuwa na utekelezaji wowote.
Wasira alinukuliwa na gazeti hili juzi akisema, “Mimi ni waziri, nina haki zangu, PAC haihusiki na mtu binafsi wala siyo ofisa ya mahesabu.”
Wakati huohuo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alitolea ufafanuzi ukata unaozikabili halmashauri nchini na Serikali ikishutumiwa kutopeleka fedha.
Alisema halmashauri husika zinatakiwa kuboresha vyanzo vyake vya mapato badala ya kuitegemea Serikali Kuu.
“Kuna changamoto kama za wafadhili kutokutoa fedha lakini na halmashauri zenyewe zinatakiwa kuhakikisha zinaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na badala ya kutegemea kwa asilimia 100 fedha kutoka serikalini,” alisema Mkuya.
Akizungumzia mafanikio ya mfumo mpya wa ulipaji wa mishahara ya watumishi wa umma, alisema umefanikiwa kuwabaini watumishi hewa 12,000 na kuokoa zaidi ya Sh400 milioni.
Powered by Blogger.