Profesa Muhongo ajiuzuru, asema yeye ni mtu safi
Profesa Muhongo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kufuatia kuhusishwa na sakata la uchotwaji wa mabilioni ya
fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, Waziri wa Nishati na madini
Profesa Sospeter Muhongo ameamua kumuandikia barua Raisi ya kujiuzulu
wadhifa wake.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam, Profesa Muhongo ameelezea furaha yake ya
kupatikana kwa maendeleo ya haraka katika wizara yake kwa kipindi chake
akisema kuwa nidhamu na uwajibikaji vilikuwa dira ya maendeleo wizarani
hapo.
Profesa Muhongo amekwenda mbali zaidi na
kueleza kuwa anaamini kujiuzuru kwake kutaisaidia Serikali na Bunge
kutuliza malumbano ya Sakata hilo ambalo linazidi kurudisha nyuma
maendeleo ya nchi.
Amesema yeye si mwizi na hawezi kuuza utu wake kwa kupewa rushwa ili kuwakandamiza watanzania.
“Nimeamua
kujiuzuru kwa dhati kabisa bila kushinikizwa na mtu yeyeote, inaonekana
mimi ndiyo nitamaliza mjadala huu wa sakata la Escrow, tuna mambo mengi
ya kitaifa yanayotakiwa kujadiliwa lakini watu wamekazana na Escrow,
nimemuandikia Rais barua rasmi ya kujiuzuru wadhifa wangu, amesema
Profesa Muhongo.
Amesema pamoja na kujiuzuru anatarajia
mapema kuzungumza na watanzania ili kuwaeleza ukweli wa sakata la
Escrow na kujiuzuru kwake ili kuvunja majungu yanayoendelea kuitesa
Tanzania na watu wake.
Amesema yeye amelelewa katika
malezi yenye maadili mema na kwamba tokea alipomaliza masomo yake
aliaswa kutopokea ama kutotoa rushwa hivyo hawezi akapokea rushwa kwa
ajili ya kuutukana utu wa mtanzania hicho ndicho kinachomgharimu.
-