Hizi ni Stori kubwa zilizopewa Headlines kwenye Magazeti ya leo Tanzania January 21, 2015
MWANANCHI
Meneja Misamaha ya Kodi TRA, Kyabukoba Leonard anayekabiliwa
na kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh 1.6 bilioni kutoka
akaunti ya Tegeta Escrow katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
ameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Hakimu Mkazi, Frank Moshi jana alimuachia huru Mutabingwa
baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwasilisha fedha taslimu
sh. bil 1 ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho
cha fedha.
Mutabingwa
aliachiwa huru kwa dhamana baada ya kuwasilisha hati tano za nyumba za
watu mbalimbali zenye thamani ya Sh 1.332 bilioni, wadhamini watatu
ambao kati yao wawili walikuwa wafanyakazi wa TRA na mmoja mjasiriamali.
Kila mdhamini kati ya wadhamini hao
alisaini hati ya dhamana ya maneno yenye thamani ya sh. mil 340 na
mshtakiwa huyo haruhusiwi kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam bila ya
kuwa na kibali cha mahakama.
Baada ya kukamilisha masharti hayo ya dhamana, Hakimu Moshi
alimuachia huru mshtakiwa huyo na akaiahirisha kesi hadi January 29,
2015 ambapo mshtakiwa huyo atasomewa maelezo ya awali (PH).
MWANANCHI
Siku chache baada ya matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa
kuonyesha kuwa CCM imeporomoka, Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amewataka
wanachama wa chama hicho kujiandaa kisaikolojia kwa matokeo yoyote
yanayoweza kutokea katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
“Wana-CCM wanatakiwa kujiandaa
kisaikolojia kwani walizoea ushindi wa asilimia 90 au 80 (wa kishindo),
huu ulikuwa ushindi wa nyuma. Tusishangae tukipata ushindi wa asilimia
50, 60, 57 au 70 ni kitu cha kawaida kutokana na kukua kwa demokrasia
hususan ushindani wa vyama vingi vya siasa kuanza kuimarika:- Makamba
Kauli hiyo ya Makamba imekuja
wakati matokeo ya serikali za mitaa yakionyesha kuwa CCM imeporomoka
kutoka ushindi wa asilimia 91.7 mwaka 2009 hadi 79.8 katika uchaguzi wa
mwaka jana na upinzani ukipanda kutoka asilimia nane mwaka 2009 hadi
takriban 20 mwaka jana.
Akizungumza jana katika mahojiano na kipindi cha ‘Power Breakfast’
cha Radio ya Clouds na baadaye kufafanua alisema matokeo ya uchaguzi
huo ni ishara kwamba kwa umri wa miaka 22 sasa, mfumo wa vyama vingi vya
siasa umeanza kuimarika.
“Hata
ushindi wa asilimia 81 tulioupata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
bado ni mkubwa na hata kama tungepata asilimia 70 haupunguzi uhalali wa
uongozi. Kusema CCM itang’oka madarakani, hapana, bado wananchi
wanakiamini tena sana:- Makamba.
MWANANCHI
Ikulu imewataka Watanzania kuacha kulichukulia suala la kujiuzulu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo kama jambo la ‘kufa na kupona’, huku ikieleza kuwa waziri huyo mpaka sasa bado ni kiongozi wa Serikali.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema hatua zilizochukuliwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi haziwezi kuwa sawa na za Prof. Muhongo kwa sababu Maswi ni mtumishi wa Serikali na profesa huyo ni mwanasiasa.
Rweyemamu alitoa ufafanuzi huo baada ya kubanwa na wanahabari waliotaka kujua sababu za Prof. Muhongo licha ya kuwekwa kiporo na Rais Jakaya Kikwete
kutokana na kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa sh. bil 306 katika
akaunti ya Tegeta Escrow, bado anafanya shughuli mbalimbali za Serikali,
ikiwa ni pamoja na juzi kwenda kuhudhuria mkutano nchini Uswisi.
“Utaratibu wa kumwajibisha yeye
(Muhongo) ni tofauti na wa Maswi. Kama mtakumbuka Bunge lilitoa maazimio
yake ambayo bado yanaendelea kutekelezwa. Msilichukulie suala hili kama
la kufa na kupona:- Rweyemamu.
Akizungumzia kauli hiyo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema, “Kauli
hiyo ya Ikulu inadhihirisha udhaifu wa Rais. Rais alisema anamweka
kiporo kwa siku mbili, Ikulu inapaswa kueleza ni kwa nini Rais ameamua
kumuweka kiporo zaidi ya siku hizo mbili wakati alidai kuwa kuna
uchunguzi mdogo tu”
NIPASHE
Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA) limepoteza zaidi ya sh. bilioni 80 kwa kipindi cha mwaka 2011
hadi 2014, kutokana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutotangaza sheria
ya tozo ya wageni katika hoteli za kitalii kwenye Hifadhi za Taifa
kwenye Gazeti la Serikali (GN).
Mwenyekiti wa Kamati Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema
mwaka 2011 Bunge lilipitisha Sheria ya ongezeko la tozo kwa wageni
wanaofikia kwenye hoteli za kitalii hifadhini na Wizara kutakiwa
kutangaza kwenye GN ili ianze kutumika.
Alisema baada ya Bunge kupitisha
wafanyabiashara wa utalii mkoa wa Arusha walifungua kesi Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha, na Tanapa ilishinda katika hukumu iliyotolewa Septemba
14, mwaka jana na siku kumi baadaye waliiandikia Wizara juu ya amri ya
Mahakama ya kutaka tangazo kuwekwa kwenye GN.
“Miezi
minne sasa serikali haijatangaza, kila mwaka Tanapa ingepata mapato ya
Sh. bilioni 20 sawa na Sh. bilioni 1.5 kila mwezi, lakini kwa uzembe na
matakwa ya wachache haijatangazwa fedha zinapotea kwa wenye mahoteli
kutengeneza faida kubwa zaidi“:- Lembeli.
Lembeli
alisema kabla ya Bunge kupitisha sheria hiyo tozo la kila mgeni
lilikuwa ni dola za Marekani tano hadi nane kwa anayelala kwenye vyumba
vya dola 100 hadi 150 na hadi sasa inapata kiasi hicho huku bei ya
chumba kimoja ikiwa ni dola 600,000.
MTANZANIA
Kampeni ya tohara kwa wanaume Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika, inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani na Umoja wa Mataifa (UN) imeonyesha mafanikio licha ya kukosolewa.
Utafiti mpya unaonyesha Marekani sasa
inafikiria kubadili sera kwa kuruhusu fidia kulipwa kwa wanaume ambao
watalazimika kukosa kazini wakati wakiuguza majeraha yanayotokana na
tohara.
Profesa wa Sera ya Afya ya Usimamizi katika Chuo Kikuu cha North Carolina, Marekani
alisema Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo inafuatilia matokeo
kutokana na majaribio ya kitabibu ambayo yeye na watafiti wengine
waliyaendesha katika Jimbo la Nyanza, Kenya kati ya Juni, 2013 na
Februari, 2014.
Utafiti huo unaonyesha sehemu kubwa ya
wanaume 1,500 walioshiriki walieleza masikitiko yao makubwa kuhusu
tohara yalihusu upotevu wa ajira na mishahara wakati wakiuguza vidonda
kutokana na tohara.
“Motisha
ya kiasi cha Sh 700 au 1,200 za Kenya, iliongeza hamasa ya wanaume
kushiriki tohara mara nne hadi sita kulinganisha na makundi ambayo
hayakupewa kabisa au yalipewa motisha kidogo,” ulisema utafiti huo wa Profesa Thirumurthy ambao ulichapishwa Agosti 20, 2014 katika Jarida la Chama cha Utabibu Marekani.
MTANZANIA
Katika hali isiyo ya kawaida, zaidi ya wanafunzi 459 wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Saku iliyopo Chamazi, Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, wanasoma katika darasa moja.
Hali hiyo ya wanafunzi kusoma katika
darasa moja na wengine chini ya miti inayozunguka shule hiyo,
inachangiwa na upungufu wa majengo ya shule hiyo ambayo ina vyumba saba
vya madarasa huku ikiwa na zaidi ya wanafunzi 2,038.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Saku, Salome Munisi alisema
shule yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya uchache wa madarasa
pamoja na wingi wa wanafunzi kuliko uwezo wa vyumba vya madarasa
walivyonavyo.
Munisi alisema idadi ya wanafunzi
walioandikishwa darasa la kwanza mwaka huu ni kubwa kuliko darasa la
pili ambalo lina wanafunzi 436, wakiwamo wanaume 217 na wasichana 219.
“Kipindi
cha mitihani inabidi wanafunzi wafanye mtihani chini ya mti kwa sababu
wako wengi darasani, huwezi mwalimu kuwapa mtihani watatizamiana na
itakuwa ngumu kupima kiwango cha elimu kwa wanafunzi kwa sababu watajaza
majibu yote yanayofanana“:- Munisi.
HABARILEO
Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Mwauwasa imesema
taasisi za Serikali na vyombo vya dola ni changamoto kwenye ulipaji
wa ankara za maji ambapo zinadaiwa zaidi ya milioni 900 ikiwa ni
malimbikizo.
Mkurugenzi wa Mwauwasa, Anthony Sanga alisema
sambamba na taasisi hizo, pia wanakabiliwa na changamoto ya ukuaji wa
mji kwa kasi ya uwezo wa Mamlaka kujenga miradi ya maji katika maeneo
ambayo yanaendelea kujengwa pamoja na wananchi kujenga juu ya matanki
ya maji.
Kukosekana kwa mfumo wa uondoshaji wa
majitaka katika maeneo ya milimani kunasababisha baadhi ya wananchi
wanaoishi maeneo hayo, kuchimba vyoo vyenye vina vifupi na kuwa chanzo
cha uchafuzi wa mazingira na hatimaye kwenda ziwa Victoria.
Sanga
alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imechukua mkopo
wa masharti nafuu wa jumla ya Euro milioni 90 kutoka benki ya uwekezaji
ya Ulaya na Shirika la maendeleo la Ufaransa ili kujenga miradi
mbalimbali ya maji na usafi wa mazingira.