Watafiti UDSM kusafisha majitaka kuwa ya kunywa
Dar Es Salaam. Kitengo cha Utafiti cha Idara ya Uhandisi,
Teknolojia na Madini (COET) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
kipo katika mchakato wa kusafisha majitaka yanayotokana na kinyesi na
kuyarejeleza kuwa safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Mkuu
wa COET, Profesa Jamidu Katima alisema hayo jana katika mkutano wa
wanasayansi ulioandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).
Alisema
idara hiyo inatarajia kukamilisha utafiti huo siku zijazo baada ya
kufanikisha teknolojia hiyo ambayo maji yake pia yatafaa kwa umwagiliaji
na mifugo.
Hivi karibuni kampuni ya nishati ya Marekani ya Janicki Bioenergy, ilizindua maji ya kunywa yaliyozalishwa kwa kutumia majitaka.
Akizungumzia
teknolojia hiyo, mkurugenzi wa Costech, Dk Hassan Mshinda alisema huu
ni wakati wa Taifa kutumia sayansi katika kukuza uchumi wa kilimo na
viwanda.
“Huu ni mradi muhimu sana kwa sababu
teknolojia hii inasaidia siyo tu kupata maji masafi yanayofaa kwa
matumizi mengine, pia yanasafisha mazingira,” alisema.
Dk Mshinda alisema majitaka ya viwandani yanaharibu mazingira na iwapo yatasafishwa yataepusha mambo mengi ikiwemo maradhi.
Alisema
Costech inajivunia kufanya kazi za kisayansi kwa kushirikiana na sekta
binafsi na Serikali na kusisitiza kutumia tafiti za wanasayansi.
“Ufike
wakati tafiti zinazofanywa na wanasayansi wazawa zisitumike kuibua hoja
bungeni tu, bali matokeo ya tafiti hizo yatumike kutunga sera na
sheria,” alisema.
Wanasayansi wa COET walitumia teknolojia hiyo katika kiwanda cha mvinyo cha Banana.
Walirejeleza majitaka ya ndizi zilizokamuliwa na kuwa majisafi yaliyofaa katika umwagiliaji, mbolea, kunywesha mifugo na kuoga.
Kabla ya mtambo wa kusafisha kujengwa, kiwanda hicho kilikuwa kikizalisha lita 80,000 za majitaka kwa wiki.