Serikali yafungia gazeti la The EastAfrican
Gazeti la The EastAfrican limepigwa marufuku kusambazwa Tanzania, ikiwa ni miaka 20 baada ya
Dar es Salaam. Gazeti la The EastAfrican limepigwa marufuku
kusambazwa Tanzania, ikiwa ni miaka 20 baada ya kuanzishwa kwake kwa
ajili ya kuandika habari za ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa
mujibu wa barua iliyotumwa mwakilishi wa The EastAfrican nchini, uamuzi
huo umechukuliwa kwa sababu gazeti hilo “limekuwa likisambazwa nchini
bila ya kuwa na usajili, kinyume na kifungu cha 6 cha Sheria ya
Magazeti, Namba 3 ya mwaka 1976”.
Uongozi wa Nation
Media Group, ambao unamiliki gazeti la The EastAfrican, umeelezea hatua
hiyo kuwa ni ya kushangaza na isiyokubalika.
Barua hiyo
ya Januari 21, 2015 inaagiza kusimamishwa mara moja kwa uchapishaji na
usambazaji wa gazeti hilo nchini Tanzania ‘’hadi litakaposajiliwa rasmi
na Msajili wa Magazeti, Idara ya Habari’’.
Kabla ya
kutolewa kwa barua hiyo, mwakilishi wa gazeti hilo nchini, Christopher
Kidanka aliitwa Jumatano na kuhojiwa na mkurugenzi wa Idara ya Habari,
ambaye pia ni msemaji wa Serikali, Assa Mwambene.
Katika
mahojiano hayo, Serikali ilieleza kutofurahishwa na jinsi gazeti hilo
linavyoripoti habari na uchambuzi wake (zikiwamo safu za maoni).
Mwambene
alilituhumu gazeti hilo kwa kuwa na mtazamo hasi dhidi ya Tanzania.
Alitoa mfano wa maoni ya hivi karibuni ambayo yalikosoa msimamo wa
Serikali kuhusu waasi wa Rwanda, FDLR walioko nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama mfano wa mtazamo wa gazeti dhidi ya
nchi.
Mwambene pia alielezea katuni iliyotoka kwenye
toleo la wiki hii la The EastAfrican, kuwa ilionyesha kutozingatia
utamaduni na kwamba ilionyesha kutomuheshimu Rais.
Matokeo yake, The EastAfrican halitakuwa likisambazwa hadi masuala ya kisheria yatakapotatuliwa.
Akizungumzia
uamuzi huo wa Serikali, mwenyekiti wa Bodi ya NMG Group, Wilfred Kiboro
alisema sababu zilizotolewa na Serikali zinashangaza kwa sababu gazeti
hilo limekuwa likisambazwa tangu miaka 20 iliyopita.
“Kwa
hakika hawawezi kuamka leo na kututangaza kuwa hatuko kihalali. Kama
ingekuwa ni suala la kuweka sawa mafaili, hilo halihitaji hatua za
kikatili za kufungia gazeti,” alisema.
Alisema kwamba
sababu halisi “ziko sehemu nyingine “ na zinaweza tu kuhusishwa na
msimamo ambao gazeti hilo, na mengine ya kampuni NMG, limechukua katika
kuripoti rushwa, wizi wa mali za umma na utoaji duni wa huduma kwa watu
wa Afrika Mashariki.
“Mwaka jana, Serikali ilifungia gazeti letu la Mwananchi kwa wiki mbili kwa sababu ambazo hazijawahi kuwekwa bayana,” alisema.
Kiboro
aliongeza kuwa sera za habari za NMG ziko wazi kuhusu uhuru wa vyombo
vyake, kitu ambacho kitaendelea kuongoza magazeti yetu katika kuripoti
wakati wote.
“Tunajua kuwa kuna wakati tulifanya makosa
katika uamuzi na tumefanya haraka kuomba radhi, kama ilivyokuwa katika
suala la katuni inayozungumziwa. Makosa kama hayo, hata hivyo,
hayatakiwi kuhalalisha kufungia gazeti kwa sababu kufungia vyombo vya
habari kunafanywa na madikteta wasiowajibika,” alisema.
Alisema
kuwa ana matumaini Serikali ya Tanzania, kwa kuheshimu dhamira yake ya
uhuru wa vyombo vya habari na kuunga mkono demokrasia, itaharakisha
kuliruhusu gazeti la The EastAfrican kurejea sokoni.
Kampuni
ya NMG, kwa kupitia kampuni yake ya Mwananchi Communications Ltd, pia
inachapisha magazeti ya Mwananchi, the Citizen na Mwanaspoti ya
Tanzania.