Mwakyembe afunguka
Dk Harisson Mwakyembe
-
Arusha. Siku mbili baada kukabidhiwa ofisi
na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, waziri ambaye
ameteuliwa kushika nafasi hiyo, Dk Harisson Mwakyembe amewataka
Watanzania kuondoa hofu ya kuhamishwa kwake kutoka Wizara ya Uchukuzi,
huku akisisitiza kuwa hana nia ya kugombea urais.
Dk
Mwakyembe aliwataka wananchi kuondoa hofu kwa sababu utendaji
aliouonyesha akiwa Wizara ya Uchukuzi, atauhamishia wizara yake mpya.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na gazeti hili muda mfupi baada ya kuapishwa
na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Daniel Kidega, Mwakyembe
alisema utendaji aliouonyesha katika wizara aliyokuwamo awali zamani,
ndiyo uliomshawishi Rais Jakaya Kikwete kumhamishia Wizara ya Afrika
Mashariki ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa masuala ya jumuiya hiyo.
“Watanzania
wanapaswa kuondoa kasumba ya kutaka anayefanya vizuri katika nafasi
yake kuendelea kubaki hapo hapo. Hapana! Anayefanya vizuri sehemu moja
ni vyema akahamishiwa sehemu nyingine ili akafanye vizuri huko pia,”
alisema Mwakyembe na kuongeza:
“Ni utashi wa Mheshimiwa
Rais kuamua kuwapanga wasaidizi wake kwa namna anayoona inafaa. Naamini
utendaji wangu Wizara ya Uchukuzi ndiyo umesababisha nihamishiwe Afrika
Mashariki ili niuendeleze huku pia.”
Kauli ya Waziri
Mwakyembe inakuja siku chache baada ya kutolewa kwa maoni ya wananchi
yaliyoonyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Rais kumbadilisha kutoka Wizara
ya Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki akibadilishana na Sitta aliyekwenda
Wizara ya Uchukuzi.
Sina nia kugombea urais 2015
Akizungumzia
malengo yake kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Mwakyembe
alisema: “Akili na malengo yangu yote kwa sasa ni kutekeleza majukumu
yangu kama Waziri wa Afrika Mashariki. Sina nia ya kugombea urais katika
Uchaguzi Mkuu ujao. Hilo nawachia wenye nia hiyo,” alisema.
Tayari wanachama kadhaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wametangaza au kutajwa kwenye mbio hizo za urais.
Faida ya ushirikiano wa EAC
Akizungumzia
faida za EAC, Waziri Mwakyembe alisema muda umefika sasa umma wa Afrika
Mashariki uanze kupata faida ya moja kwa moja ya ushirikiano kati ya
nchi wanachama za Tanzania, Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda akitaja
nafuu ya gharama za usafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kuwa
miongoni mwa maeneo muhimu ya kuangaliwa.
“Miaka 15
sasa imepita tangu kufufuliwa kwa jumuiya hii, lakini bado ni ghali
kusafiri kwa ndege kati ya Dar es Salaam na Nairobi, Kampala, Bujumbura
na Kigali kulinganisha na Johannesburg, Afrika Kusini, India au Dubai,”
alisema. Mwakyembe.