Wanafunzi hatarini kupata magonjwa ya mlipuko Geita
Shule za msingi Ukombozi na Nyankumbu zilizopo mjini Geita
mkoani hapa, zipo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na
kukosa vyoo na msongamano mkubwa wa wanafunzi kwenye madarasa.
Hali hiyo ni kinyume na Sera ya Elimu ya Mwaka 2010 inayotaka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.
Shule
hizo zilizopo ndani ya eneo moja, zina zaidi ya wanafunzi 4,000, choo
kimoja chenye matundu 14 na madarasa 16, huku kila tundu likitumiwa na
zaidi ya wanafunzi 200.
Wakizungumza shuleni hapo
jana, wakuu wa shule hizo, Mwalimu Richard Rwengusi na Maxmilian Amos
walisema hali ni mbaya, kwani shule hazina vyoo na zinakabiliwa na
upungufu wa madarasa na madawati.
“Shule ya Ukombozi
pekee yake ina wanafunzi 1,792, madarasa manane, matundu ya vyoo 14,
ambayo hadi sasa yamejaa na madawati 176, hivyo wanafunzi 1,616 wanakaa
chini, huku Shule ya Nyankumbu ikiwa na wanafunzi 2,022 na madawati
180,” alisema Mwalimu Mkuu wa Ukombozi, Rwengusi.
“Hapa
hali ya usalama kwa watoto na walimu ipo hatarini, vyoo vimejaa na
vimebomoka upana wa madarasa ni mdogo, wanafunzi wanabanana na hewa
hakuna,” alisema Maximilian.
Walimu wanena
Walimu wa shule hizo
walisema wanapata shida kufundisha zaidi ya wanafunzi 300 kwenye darasa
moja kutokana na hewa nzito, kelele na vumbi.
Kamati za shule
Viongozi
wa kamati za shule hizo wanakiri uwapo wa hali hiyo na kwamba, suala
hilo tayari limefikishwa kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Geita.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Magreth Nakainga alikiri kuwapo tatizo,
lakini alisema wameshindwa kulitatua kutokana na ukosefu wa fedha.
“Kweli ni changamoto, hali ya madawati ni tatizo, madarasa na vyoo pia haviridhishi,” alisema Nakainga.