Profesa Lipumba avuruga Bunge
Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi,
Kisutu, Dar es Salaam jana baada ya kusomewa shtaka la kuhamasisha
wafuasi wa chama hicho kutenda kosa la jinai. Juu kulia- Spika wa Bunge
Anne Makinda akizungumza baada ya wabunge wa upinzani (kushoto),
kusimama mfululizo wakipinga kuahirishwa kwa hoja ya kujadili suala la
Profesa Lipumba kukamatwa. Picha na Edwin Mjwahuzi na Anthony Siame.
Dodoma. Kwa mara ya pili, Spika Anne
Makinda jana alilazimika kuahirisha kwa muda shughuli za Bunge la
Jamhuri ya Muungano baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kukataa
kukaa, wakishinikiza kitendo cha polisi kumpiga na baadaye kumkamata
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kijadiliwe kwa masilahi ya
Taifa.
Profesa Lipumba, ambaye pamoja na wanachama
wengine 32 walikamatwa juzi eneo la Mtoni Mtongani wakati alipokuwa
akielekea Zakhem, Mbagala jijini Dar es Salaam kuwataka wafuasi wa CUF
kutawanyika kwa amani baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano, jana
alikamatwa tena akiwa nje ya Kituo Kikuu cha Polisi muda mfupi baada ya
kuachiwa kwa dhamana, akidaiwa kuongea na waandishi wa habari wakati
akiwa mtuhumiwa.
Wakati akiwa mbaroni, Profesa Lipumba
alijisikia vibaya na hivyo kupelekwa hospitali kabla ya kufikishwa
Mahakama ya Kisutu jioni, akishtakiwa kwa kufanya maandamano bila ya
kibali.
Jana bungeni, Spika Makinda alijikuta
akipambana na nguvu ya wabunge wachache wa upinzani ya kuzuia kuendelea
kwa shughuli za Bunge kama ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka jana wakati
walipotumia staili hiyo ya kusimama wakati wote kushinikiza Bunge
kusikiliza matakwa yao kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya wahusika kwenye
sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati
huo ilibidi Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi, Sera na
Utaratibu wa Bunge, William Lukuvi kumfuata mkuu wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe kuzungumza naye kabla ya Bunge kuahirishwa.
Tafrani
ya jana iliyodumu kwa dakika 12 na sekunde 8 ilianza baada ya
kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu. Baada ya kumalizika kwa
kipindi hicho, wabunge zaidi ya watano wa upinzani walisimama kutaka
kutoa hoja na Spika Makinda alimpa nafasi ya kwanza James Mbatia, ambaye
ni mbunge wa kuteuliwa, aliyeomba mwongozo akitumia Kanuni ya 47
inayohusu kuahirishwa kwa shughuli za Bunge ili kujadili jambo la
dharura.
Mbatia, ambaye aliisoma kanuni yote ya 47
yenye vipengele vinne, aliomba kutoa hoja ya kutaka kitendo cha kupigwa
kwa Profesa Lipumba wakati akiwa katika mkutano wa hadhara, kijadiliwe.
Mbatia
alisema: “Jana (juzi) tarehe 27 mwezi Januari mwaka huu wilayani Temeke
jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba alikuwa na
ratiba ya kufanya mkutano wa hadhara pamoja na maandamano na walifuata
taratibu zote za kisheria na za kikatiba za kujumuika, kuandamana na
kuweza kubadilishana mawazo.
“Cha kushangaza, dakika za
mwisho polisi walikataza jambo hilo lisiendelee na Profesa Lipumba
akaonyesha ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoendelea na jambo
hilo, lakini Jeshi la Polisi likafika baadaye kidogo kuamua kutumia
nguvu dhidi ya raia ambao hawafanyi fujo yoyote, raia ambao wameonyesha
ushirikiano na utii kwa Jeshi la Polisi.”
Mbatia
alisema pamoja na ushirikiano huo polisi waliamua kumpiga Profesa
Lipumba na raia wengine wa Tanzania hata watoto wadogo chini ya umri wa
miaka mitano, kauli ambayo ilifanya wabunge wampigie makofi mwenyekiti
huyo wa Chama cha NCCR-Mageuzi.
Aliendelea kusema waandishi wa habari walipigwa virungu na kudhalilishwa, jambo ambalo alisema linaondoa utulivu, amani nchini.
“Mimi
binafsi nilisikitika sana baada ya vyombo vya habari kuonyesha moja kwa
moja. Nilichukua hatua ya kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa
kuwa mambo ya aina hii yalipokuwa yakitokea huko nyuma, sisi vyama vya
siasa tuliwahi kumuhusisha hata Rais.”
Alifafanua kuwa
walimhusisha “Rais na Jeshi la Polisi na IGP mstaafu, (Said)
alituhakikishia kushirikiana na sisi kwa maazimio na Rais akatoa kauli
yake, mawaziri wakashiriki. Sasa jana polisi ilitoa kauli kwamba wana
maagizo kutoka juu na kuongeza:
“Sasa Spika, tusipoziba ufa, tutakuja kujenga ukuta.”
Huku
wabunge wa upinzani wakipiga makofi, Mbatia aliendelea kusema: “Mwaka
juzi waandishi wa habari waliuawa, Jeshi la Polisi likawa linaua raia,
raia wanaua polisi, viongozi wa dini wakaingizwa huko kuuawa nchi
ikafikia hali ya sintofahamu na sasa imeanza kujirudia tena kwa kasi
kubwa, kwa dharau kubwa na kwa kudhalilishwa.”
Huku
akipigiwa makofi, Mbatia alibainisha kuwa Profesa Lipumba ni mwenyekiti
wa chama chenye wabunge wengi bungeni ambao ni zaidi ya 35 pia ni
mwenyekiti wa chama ambacho kinaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Zanzibar, hivyo kama anaweza kudhalilishwa kiasi hicho basi haijulikani
raia wengine wa kawaida wanaweza kudhalilishwa namna gani.
Jambo
hilo likiachiwa liendelee, litasababisha matatizo hivyo kwa kuwa Jeshi
la Polisi lilisema limepata maagizo kutoka juu katika tukio hilo, ni
muhimu hilo agizo likajulikana limetoka kwa nani, kwa sababu gani na
masilahi gani, alisema huku akipigiwa makofi na wabunge wenzake.
“Nilimuuliza
waziri jana aniambie ni agizo kutoka juu kwa nani na kwa malengo gani,”
alisema Mbatia na kuongeza: “Kwa nini tusiwekeze kwenye amani na
utulivu wa taifa letu wakati tulishakubaliana viongozi wote wa (Kituo
cha Demokrasia Tanzania) TCD na Rais alishiriki mwaka juzi tarehe 9 na
10 mwezi wa saba, sasa leo hii naona limeanza kujirudia na tunaona giza
mbele ya safari.
“Sasa, Spika naomba kutoa hoja
tuahirishe shughuli za Bunge ili tujadili (suala hili) kwa maslahi
mapana ya Taifa letu, tulijadili jambo hili ili tuweze kupata majibu
sahihi na tuhakikishe kwamba jambo hili halitajitokeza tena.”
Baada
ya kutoa hoja hiyo wabunge wote wa kambi ya upinzani kwa ujumla
walisimama kama ishara ya kuunga mkono, lakini Spika Makinda alisimama
na kusema: “ Naomba mkae, naomba mkae. Hoja hii haiungwagi mkono
(wabunge wakaguna aah aah aah). Jamani eeh mimi siyo kangaroo court,
ninachosema hoja namna hii huwa haiungwagi mkono someni kanuni.”
Spika
Makinda aliendelea kusema: “Someni kanuni na ameisoma vizuri mheshimiwa
na nimefurahi ameisoma sehemu ya kanuni hiyo inasemaje, inasema hiyo
kanuni ya 47(4) inasema Spika atakavyoona kwa kuzingatia mazingira ya
suala lililojadiliwa.
“Kwa mazingira hayo naiagiza
Serikali kesho (leo)… mimi ni Spika naomba tuelewane kesho (leo) itoe
kauli kamili ambayo sisi tutaelewana halafu kesho (leo) nitaruhusu
mjadala, lakini siyo leo (jana).”
Baada ya hapo Spika
aliruhusu kuendelea kwa shughuli za Bunge, lakini wabunge wa upinzani
walisimama na kusababisha Spika kusimama tena.
“Nimesema
kesho ndiyo tutajadili na kama mnataka nendeni (kelele zikaaanza kutoka
upinzani) jamani muwe na busara,” alisema huku wabunge wa vyama vya
upinzani wakipiga kelele na kufanya hali ya kuelewana kupungua.
Kelele
zikaendelea huku Spika akisema “hatuwezi kuanza kutukanana hapa kama
mnataka kufanya mnachotaka kufanya, fanyeni… watu wazima tumieni busara
mnachotaka kufanya, fanyeni lakini hamtumii busara.”
Zogo
likiwa linaendelea, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Muhagama
walisogea kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kujadiliana. Spika aliendelea
kusisitiza kuwa Mbatia alisema vizuri kwamba suala hilo linataka amani
na mshikamano. Pamoja na Spika kusema hivyo, wabunge wa upinzani
walionekana kuwa wakali na muda wote wakiwa wamesimama.
Spika
Makinda bila kujali kusimama kwa wabunge wa upinzani, alitangaza
kuendelea kwa shughuli za Bunge kwa kumtaka katibu kusoma kinachofuatia,
lakini ilishindikana kwani alipotaja hoja za Serikali hasa ya Kamati ya
Hesabu za Serikali, mwenyekiti wake hakutokea huku wabunge wakiwa
wameendelea kusimama na Spika akawaonya kwamba huo siyo mtindo wa
kanuni.
Tafrani iliendelea huku wabunge wakisema;
“Haiwezekani, haiwezekani, lazima jambo hilo lijadiliwe.” Hata hivyo,
Spika alikataa kwa maelezo kuwa siyo utaratibu wa Bunge. Hali ya
kutoelewana na kelele bungeni iliendelea na kila mbunge wa upinzani
akisema chake huku wakiwa wamesimama.
Spika Makinda
alisimama na kuwaambia tena, “Mnajua tatizo mlilonalo ninyi ni dogo
sana, jambo hili ni kubwa sana,” alisema na kuamsha kelele wa wabunge
wakisema, “Ndiyo maana tunataka lijadiliwe, ndiyo maana tunataka
lijadiliwe.”
Spika Makinda alisisitiza akisema:
“Ninachosema jambo hili ni kubwa sana na kama ni kubwa sana, hatuwezi
kuzungumza kama mnavyozungumza sasa ni vizuri wabunge wote wakaelewa na
kwamba mimi ndiye niliyeruhusu hoja hii ije baada ya kujadiliana na
Mbatia, Tundu Lissu na Mohamed Mnyaa.”
Kelele
ziliendelea na kusababisha Spika kuahirisha shughuli za Bunge hadi leo
lakini akabadili na kusema tena hadi jana saa 10:00 jioni.
Akizungumzia
kitendo hicho nje ya Bunge, Mbatia alisema alitegemea baada ya kutoa
hoja yake Spika angeruhusu mjadala na Serikali kutoa majibu, lakini
haikuwa hivyo.
“Niletegemea Waziri Mkuu asimame kutoa majibu ya Serikali, lakini haikuwa hivyo sasa hatuna jinsi (ya kufanya),” alisema Mbatia.