Urais 2015: Ukawa waanza safari
Dar es Salaam. Wakati CCM ikisubiri Februari kufanya tathmini kuona kama baadhi ya wagombea wake wa urais wametekeleza masharti ya adhabu zao, washindani wao wa Ukawa, Jumanne ijayo watakutana kujadili mambo mbalimbali, ukiwamo mchakato wa kuwapata wagombea wake wa urais, ubunge na udiwani, imefahamika.
Tangu
mwaka huu uanze zimekuwapo pilikapilika nyingi za kisiasa ndani ya
vyama vya siasa na Jumanne iliyopita CCM ilifanya kikao cha Kamati Kuu
mjini Zanzibar na kutoa maazimio yanayogusia mchakato huo lakini ikasita
kutaja ratiba rasmi ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM.
Wakati
hali ikiwa hivyo, habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya
viongozi wa Ukawa, umoja huo utakutana jijini Dar es Salaam Januari 20,
ukiwa na ajenda mbalimbali kuhusu ushirikiano wao, likiwamo suala la
kupata wagombea huku vikao vya ndani ya vyama vikitarajiwa mwishoni mwa
mwezi huu.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia
alithibitisha jana kuwapo kwa kikao hicho Jumanne akisema kutakuwa na
ajenda nyingine lakini: “Suala la kupata wagombea nalo huenda
likajadiliwa. Kuhusu suala la mgombea urais wa Ukawa, linaweza kuwa
sehemu ya mazungumzo lakini halipo kwenye ajenda.”
Ajenda
nyingine alizotaja ni mwongozo wa Ukawa, kura ya maoni ya Katiba,
changamoto za uandikishaji wa daftari la wapigakura, hali ya uchumi na
tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika Desemba mwaka
jana. Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi alisema
watajadili ajenda hizo ili kuhakikisha wanatafuta majibu ya changamoto
zilizopo kwa sasa.
Kiongozi huyo pia alithibitisha
taarifa kuwa kila chama ndani ya Ukawa kupitia vikao vyake kitateua
majina ya wagombea ambao watashindanishwa ndani ya umoja huo, akisema
kabla ya Machi, jina la mgombea urais ndani ya chama chake litakuwa
limeshapendekezwa.
Awali, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi,
Mosena Nyambabe alisema vikao vya chama hicho vinavyotarajiwa kufanyika
mwishoni mwa mwezi huu vitakuwa na ajenda ya uchaguzi vitakavyojadili
mwelekeo wa uchaguzi huo kama kalenda yake inavyosema.
“Nadhani
vikao hivyo ndiyo vitaanza kujadili ajenda ya uchaguzi ujao. Tulishatoa
nafasi ya watu kujitokeza kwenye nafasi mbalimbali. Tukishapendekeza
majina ya wagombea kwa baadaye ndiyo tutawapeleka ili kuchambuliwa kwa
pamoja na kamati ya Ukawa.
“Mpaka sasa kamati ya Ukawa
inaendelea na kazi yake tangu Oktoba mwaka jana ila inakuwa vigumu kwa
wajumbe kujua kazi zote zinazofanywa na kamati hiyo kutokana na msingi
wa majukumu yake.”
Nyambabe alisema kamati hiyo imekuwa
ikifanya kazi, ikijumuisha wajumbe wasiopungua watatu kutoka kila chama
ili kufanya tathimini, kuchambua na kuratibu shughuli zote za uchaguzi.
Kuhusu kupata mwongozo wa Ukawa, Nyambabe alisema:
“Namna ya kupata mgombea, ilani moja na mwelekeo, vinaweza kuonekana
kuanzia Februari baada ya vyama kukaa vikao vyake.”
Wakati
Nyambabe akisema hayo, kumekuwa na taarifa katika vyombo vya habari
kuwa CUF kimeshatangaza kumsimamisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwania
urais, ambazo hata hivyo, zimekanushwa na Naibu Katibu Mkuu wake Bara,
Magdalena Sakaya.
Alisema kikao cha hivi karibuni ndani
ya chama hicho kilikuwa na ajenda ya kutathimini Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa tu na hakukuwa na ajenda nyingine iliyojadiliwa. “Bado
hatujapendekeza jina lolote,” alisema Sakaya.
Hata
hivyo, Sakaya alisema kikao kijacho cha wenyeviti wa Ukawa hakitakuwa na
mamlaka yoyote ya kuamua au kupitisha jambo bila kupata baraka za
viongozi wa Baraza la Uongozi Taifa kutoka kila chama.
“Kikao
hicho sijafahamu ajenda yake lakini ifahamike tu kwamba, ndani ya Ukawa
kuna vikao vitatu; kikao cha maofisa, kikao cha makatibu na kikao cha
wenyeviti na hufanyika kwa kuzingatia ratiba zake,” alisema na kuongeza:
“Kwa
hivyo utaratibu wa mgombea hauwezi kupatikana kwa sasa kwani hakuna
chama ambacho kimejadili ajenda yoyote au kupitisha majina ya wagombea
wake.”
Sakaya alisema kabla ya kujadiliwa ndani ya
Ukawa, vikao vya mabaraza na kamati kuu za vyama husika vitakuwa
vimeshiriki kuchambua na kupitisha majina ya wagombea wake wanaokidhi
vigezo.
“Baada ya hapo ndipo majina yatafikishwa Ukawa
na kamati itachambua wanaoweza kusimama kwa niaba ya Ukawa kutokana na
tathimini yao watakayokuwa wameipata,” alisema na kuongeza:
“Kwa
upande wa CUF, kalenda yetu inaonyesha kuwa na vikao mwishoni mwa mwezi
huu. Nadhani kutakuwa na mwelekeo juu ya uchaguzi ujao.” Viongozi wa
juu wa Chadema jana hawakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Ofisa
Habari wake, Tumaini Makene alisema kwa sasa chama hicho hakijafikiria
kuwa na vikao vyenye ajenda ya kuangalia jina litakalopitishwa kwa ajili
ya kuingia Ukawa...
“Bado kabisa kuhusu suala la
kujadili mgombea urais wa Ukawa, hatujafikiria hilo ila kinachotuumiza
akili kwa sasa ni kero za daftari la wapigakura na kuwapo kwa tume
isiyokuwa huru ya uchaguzi. Ratiba ya ajenda hiyo ikitoka
tutajulishana,” alisema Makene.