Jaji Warioba: Rais ajaye anafahamika
Jaji Warioba
Dar es Salaam. Wakati Taifa zima likiwa
katika kitendawili cha kumjua kiongozi wa nchi atakayepatikana baada ya
Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rais ajaye
anafahamika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu jana,
Jaji Warioba alisema si kazi ngumu kwa Watanzania kumfahamu rais ajaye
kwa kuwa katika miaka 50 tangu tupate uhuru, Watanzania wanazijua sifa
za kiongozi bora.
Jaji Warioba alisema; “Tatizo la
kumjua rais afaaye tunalikwepa lakini linafahamika. Wanaotumia fedha na
lugha chafu katika kampeni na hao ndiyo wasiotakiwa.”
“Katika
miaka 50 tunazijua sifa za kiongozi bora. Hapa tunakwepa tatizo tu.
Tatizo ni matumizi ya fedha na lugha chafu katika kampeni,” alisema Jaji
Warioba ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu.
Hadi sasa
wanasiasa zaidi ya 20 wakiwamo wa CCM na upinzani wamekuwa ama wanatajwa
au wameonyesha nia ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu
ujao.
Ukiacha wale wanaotajwa, wanasiasa waliotangaza
nia hiyo kutoka CCM ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari
Makamba, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa
Nzega, Hamis Kigwangala na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku Mbunge wa
Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed akitangaza nia kupitia ADC.
Akifafanua
zaidi, Jaji Warioba alisema kila mtu anaweweseka kuhusu kiongozi
anayefaa ingawa ni kazi rahisi kumjua kutokana na ujuzi tulionao wa
miaka zaidi ya 50 ya uhuru.
Kadhalika, Jaji Warioba
alisema viongozi wa Serikali hawana budi kuangalia taswira ya uchaguzi
mkuu ujao kupitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao umeonekana kuwa na
kasoro zilizosababisha vurugu.
“Nchi hii ina amani na
tujitahidi kuilinda amani yetu. Katika uchaguzi huu tufanye kila
tuwezalo kuweka maandalizi yenye umakini,” alisema Warioba na kuongeza:
“Nasisitiza amani. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni funzo.”
Tetesi kuwania urais
Hivi
karibuni baadhi ya vyombo vya habari, likiwamo gazeti la chama tawala,
viliripoti tetesi kuwa Jaji Warioba anaandaliwa kuwania urais kupitia
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), tetesi ambazo kiongozi huyo
alizikanusha vikali.
Jaji Warioba alisema amelitumikia Taifa kwa muda mrefu na aling’atuka kwa mapenzi yake, hivyo hawezi kurudi tena katika siasa.
“Nimetukanwa
sana, nimebezwa, nimekejeliwa kwa mambo mengi lakini ukweli ni kuwa
nilifanya uamuzi wa kung’atuka katika siasa miaka 20 iliyopita na siwezi
kubadili uamuzi wangu,” alisema.
Akizungumzia baadhi
ya wanasiasa kutumia jina lake katika majukwaa na baadhi kumkashifu kwa
madai kuwa alimsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Jaji
Warioba aliwataka wanaofanya hivyo wasitumie jina lake kusafisha njia
zao katika siasa.
“Nimeitumikia nchi hii kwa miaka 30,
kuanzia mwaka 1966 hadi 1995 nikang’atuka. Niliufanya uamuzi huo miaka
20 iliyopita, nikabaki katika uongozi wa chama nako nikaachia ngazi
2002. Mjue kuwa nilifanya hayo kwa umakini mkubwa,” alisema.
Utata Kura ya Maoni
Katika
mahojiano hayo, pia Jaji Warioba alizungumzia mchakato wa kuboresha
Daftari la Wapigakura na Sheria ya Kura ya Maoni kuwa mwingiliano wake
hasa katika kipindi cha uchaguzi utaleta mkanganyiko.
Akizungumzia
mkanganyiko huo, Jaji Warioba alisema sheria inaweka utaratibu maalumu
wa mchakato wa kura ya maoni ambao alisema hautaendana na ratiba ya
uandikishwaji katika daftari hilo.
“Kwa utaratibu
uliowekwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itamaliza kazi Machi na
wakati huo kura ya maoni imepangwa kufanyika Aprili. Kwa hali hiyo
hatuna uhakika kama Tume itakamilisha kazi yake katika kipindi hicho,”
alisema.
Jaji Warioba alisema Sheria Kura ya Maoni Na. 3
ya mwaka 2014 inasema kuwa wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kura ya
maoni kwa kipindi cha miezi miwili na mwezi mmoja wa kampeni lakini hadi
sasa hakuna ratiba inayoeleweka, jambo ambalo linaleta mwingiliano.
“Hii
ni Januari, kama watafuata sheria na kuanza kutoa elimu kwa kipindi cha
miezi miwili, ina maana itakuwa ni Aprili na Mei, ukijumlisha mwezi
mmoja wa kampeni ambao ni Juni ina maana kura itapigwa Julai. Ikumbukwe
kuwa mwezi huo mbio za uchaguzi zitakuwa zimepamba moto,” alisema. Kura
hiyo ya maoni imepangwa kufanyika Aprili 30.
Jaji
Warioba alisema ni vyema kama mchakato wa Katiba mpya ukaenda kama
sheria inavyosema kwani kinyume na hapo mambo yataharibika na pengine
vurugu zinaweza kutokea katika uchaguzi mkuu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju hakupatikana kuzungumzia utata huo wa kisheria.
Kuhusu matumizi ya BVR
Kadhalika,
Jaji Warioba alisema kwa matumizi ya teknolojia BVR katika hatua ya
maboresho ya daftari la kudumu la wapigakura, kwa uzoefu alio nao, vifaa
hivyo vina utata mkubwa hivyo unahitajika umakini mkubwa.
“Nilikwenda
Malawi mwaka 2004 nikaona utaratibu wa BVR umeleta changamoto kwa
sababu tu ni teknolojia mpya. Inahitajika elimu ya kina kabla ya
matumizi yake,” alisema Jaji Warioba.
Alitoa mfano wa
utata wa BVR kuwa iwapo mpigakura atafanya udanganyifu na kujiandikisha
mara mbili au zaidi (hata kama atatumia majina tofauti), mashine itafuta
majina yaliyozidi na kubaki na taarifa zake katika kituo kimoja tu.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema tume hiyo
imeshazifanyia majaribio mashine hizo katika majimbo matatu na
zimeonyesha ubora na upungufu ulikuwa mdogo huku zile zenye kasoro
zikifanyiwa marekebisho.