Madiwani walaani jaribio la kumuua mkurugenzi
Singida. Madiwani wa CCM wilayani Iramba
wamelaani vikali jaribio la kutaka kuuawa kwa bomu mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Mkurugenzi huyo,
Halima Hanjali Mpita alinusurika baada ya kitu kilichokuwa kwenye
bahasha kulipuka kitandani kwake wakati akijiandaa kutoka. Bahasha hiyo
alipewa na katibu muhtasi wake ikiwa na kadi ya pongezi iliyopelekwa
ofisini kwake na watu wasiojulikana.
Jana, madiwani hao
pamoja na kulaani kitendo hicho, wameomba Polisi kuwasaka na kuwakamata
wote waliohusika na njama hizo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya
sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, katibu
wa madiwani wa CCM ambaye anatoka Kata ya Urughu, Simon Tyosela alisema
umoja wao ulitoa tamko hilo kwenye kikao kilichofanyika Alhamisi
iliyopita.
“Kwa ujumla sisi madiwani wa CCM tupo pamoja
na mkurugenzi wetu Halima Mpita na vilevile watendaji wote. Kwa umoja
huo sote kwa pamoja tutaendeleza gurudumu la maendeleo ya wilaya ya
Iramba,” alisema.
Aidha, Tyosela ameiomba polisi pamoja
na kufanya uchunguzi wa jaribio hilo, ichunguze kwa kina ujumbe
aliopewa mkurugenzi huyo kwamba amedhulumu Sh90 milioni kutokana na
‘dili’ walilofanya pamoja ili ukweli ufahamike.
Katibu huyo alisema wananchi wanataka kufahamu kwa kina suala hilo.
na
hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa watakaokamatwa
kuhusika na jaribio hilo na juu ya ‘dili’ la shilingi 90 milioni.
Katika
hatua nyingine,Tyosela alisema madiwani wa chama tawala hawafurahishii
wala hawapendezwi na msuguano uliopo kwenye halmashauri hiyo wa
watendaji kwa watendaji na watendaji na mkurugenzi wao.
“Kuna
uvumi kwamba baadhi ya watendaji wanataka kuomba kuhama kwa madai
kwamba sisi madiwani hatuwapendi.Hapana sisi tunawapenda sana watendaji
wetu na hatupo radhi kuona mtendaji ye yote anahama kutokana na
misuguano ya ndani kwa ndani ambayo haina tija kwa wananchi wa wilaya ya
Iramba.