Ripoti ya wizara yazidi kuiweka pabaya IMTU
Dar es Salaam. Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii imesema Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na
Teknolojia (IMTU) hakitafunguliwa mpaka pale upungufu ulioainishwa
utakapofanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati
Maalumu ya Ukaguzi iliyoundwa na wizara hiyo, IMTU iliyofungiwa Julai
mwaka jana, haitaweza kuendelea na huduma kutokana na ukaguzi
uliofanyika Desemba 19 kubaini kwamba bado ina upungufu kwa asilimia 50
licha ya kufanyiwa ukarabati.
Ripoti hiyo ilibainisha
pia kuwa, licha ya kupewa muda wa kufanya marekebisho, bado sehemu
nyingi za kutolea huduma zinakosa nafasi ya kutosha, mazingira yasiyo
rafiki kwa watu wenye mahitaji maalumu pamoja na mfumo wa maji kuwa
mbovu huku majengo yakiwa bado na nyufa.
Ilithibitishwa
kwamba, hakuna mfamasia aliyeajiriwa kwa mkataba wa kudumu huku idadi
ya wauguzi 16 waliopo ni wachache na kwamba haikidhi mahitaji ya
hospitali.
Pia taarifa hiyo ilieleza kwamba kuna
watumishi waliopewa majukumu bila sifa stahiki na wengine kupatiwa
mafunzo kazini na upungufu katika wodi za upasuaji.
“Licha
ya kukosekana kwa uboreshaji wa huduma za afya hospitalini hapo, timu
haikuona mpango mkakati wala mpango wa utekelezaji wa mwaka na
ilibainika kwamba, miongozo hii muhimu ni siri ya wachache,” ilisema
sehemu ya ripoti hiyo.
Mkurugenzi wa Hospitali ya IMTU,
Profesa Yasini Mgonda alisema wameshakamilisha ukarabati wa kituo
hicho, lakini bado hawajaweza kufungua hadi watakapopata tamko kutoka
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Profesa Mngoda alisema kasoro
zilizoainishwa zimeshatekelezwa na wanachosubiri ni ruhusa kutoka
wizarani.