FastJet yashindwa tena kutua Uwanja wa Songwe
Dar es Salaam. Kwa mara nyingine, hali ya
hewa mjini Mbeya jana ilisababisha ndege ya kampuni ya FastJet,
iliyokuwa na abiria 120, kushindwa kutua kwenye Uwanja Ndege wa
Kimataifa wa Songwe na kurejea Dar es Salaam.
Hii ni
mara ya pili katika kipindi cha takriban wiki mbili kwa tukio hilo
kujirudia baada ya ndege nyingine ya FastJet, iliyokuwa na abiria 131
Januari 12, kushindwa kutua uwanjani hapo kutokana na hali mbaya ya
hewa.
Kwa mujibu wa ratiba, ndege hiyo iliondoka Dar es
Salaam saa 3.05 asubuhi na kutakiwa kutua saa 4.30 asubuhi kwenye
uwanja huo wa Songwe, takribani mwendo wa saa moja na dakika ishirini.
Meneja
mkuu wa Fastjet Tanzania, James Kibati alisema ndege hiyo ilishindwa
kutua kutokana na hali mbaya ya hewa na kulazimika kurudi Dar es Salaam.
“Tunasubiri kibali cha watu wanaohusika na hali ya hewa hapa uwanjani, wakituruhusu tutaondoka tena leo (jana),” alisema Kibati.
Baadaye ndege hiyo iliruhusiwa kuondoka Dar es Salaam
saa 10.00 jioni na ilifika salama. Umbali kutoka Dar es Salaam hadi
Mbeya kwa njia ya anga ni kilomita 672 na kwa barabara ni kilomita 828.
Mmoja
wa abiria waliokuwamo kwenye ndege hiyo, Joseph Mbilinyi, ambaye ni
mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), alisema waliondoka Dar es Salaam saa
1.00 asubuhi na Mbeya walifika saa 2.15 asubuhi. Alisema kabla ya kutua
walikuta kuna ukungu mkubwa uliaombatana na mvua za rasharasha na
kufanya ndege hiyo kushindwa kutua.
“Wahudumu wa ndege
walitutangazia kwamba tusiwe na wasiwasi kwani mafuta ya kurudi Dar es
Salaam yapo ya kutosha. Tunawashukuru wahudumu wa ndege hiyo kwani
walijitahidi sana kutuondoa hofu.
“Hakuna
kilichoharibika tu zaidi ya ratiba kwani unapotoka huku unakwenda
umepanga kufanya jambo fulani lakini kwa dharura hii imeshindikana,”
alisema.
Kwa takriban wiki tatu sasa hali ya hewa ya
mkoani Mbeya imekuwa ya mvua na mawingu, hali ambayo siyo nzuri kwa
usafiri wa anga. Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa imeshatahadharisha
kuhusu mvua kubwa katika kipindi hiki.