Dk Slaa: Tanzania ni dhaifu kupambana na mihadarati
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa
Dk Slaa alisema hayo hivi karibuni alipomkaribisha
nyumbani kwake, Padri John Wootherspon kutoka Hong Kong aliyekuja
kuhimiza kampeni ya kuwazuia vijana kuacha kusafirisha dawa hizo katika
majimbo ya China ya Guangzhou, Macau na Hong Kong.
Padri
Wotherspon ambaye anawatembelea wafungwa katika magereza ya Hong Kong,
Macau na Guangzhou alisema kwa sasa kuna wafungwa wa Kitanzania zaidi ya
130 wanaotumikia vifungo kutokana na kusafirisha dawa za kulevya.
“Nitahakikisha
kuwa unafanyika utaratibu wa kuwaondoa Watanzania waliofungwa Hong Kong
warudishwe na kuhukumiwa nyumbani. Hilo jambo nitalipa kipaumbele kwa
nafasi yangu,” alisema Dk Slaa.
Kuhusu wajibu wa
Serikali katika kupambana na biashara hiyo, Dk Slaa alisema bado kuna
udhaifu mkubwa kwani hakuna mwamko wa dhati wa kuwahukumu kisheria
wanaosafirisha dawa za kulevya.
“Ikiwa Umoja wa Mataifa
umekubali na kuidhinisha kuwa wafungwa wanaokamatwa nje ya nchi
wahukumiwe katika nchi zao, iweje leo hapa nchini tusifanye mchakato wa
kuwarudisha nyumbani hao ndugu zetu?” alisema Dk Slaa.
Katika mkutano huo, Dk Slaa aliandika ujumbe mfupi wa
maneno kwa wafungwa hao akiwatakia maisha marefu na kuwaombea kumaliza
salama vifungo vyao.
“Wadogo zangu, ndugu, dada na kaka
zangu, kupitia Father John, nawaombea kwa Mungu awape ustahimilivu na
atawaokoa kwa uwezo wake. Tupo nanyi,” ulisema ujumbe wa Dk Slaa.
Dk Slaa pia alisoma barua za wafungwa hao zilizoandikwa kwa mkono.
Padri Wootherspon alisema kukutana na Dk Slaa ni sawa na kukutana na kiongozi kama; Nelson Mandela au Mwalimu Julius Nyerere.
“Kwa
dakika 90 nilizokaa pale na Dk Slaa nilijisikia kama nipo nyumbani kwa
Mandela au Nyerere. Ninachoomba ni kuwa kwa nafasi yake asaidie vijana
kuacha kusafirisha dawa za kulevya,” alisema.
Padri
Wootherspon ambaye ameondoka jana kuelekea Hong Kong alisema ataendelea
kufanya kila awezalo ili Tanzania isiwe kichochoro cha kusafirisha dawa
za kulevya.