JK atema mawaziri 60
Rais Kikwete
Dar es Salaam. Panga pangua ya saba ya
Baraza la Mawaziri iliyofanyika juzi imefikisha mawaziri 61 waliotemwa,
kujiuzulu au kufariki dunia tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani
mwaka 2005, huku mawaziri 16 wakihimili mawimbi hayo hadi sasa.
Katika
mabadiliko hayo saba yaliyofanywa katika kipindi cha miaka tisa, wako
waliobadilishwa wizara, kupandishwa kutoka naibu waziri kuwa waziri
kamili, huku sura mpya zikiingizwa.
Mabadiliko hayo
yalitokana na mawaziri kutakiwa kuwajibika kutokana na kashfa
mbalimbali, huku mengine yakitokana mawaziri kufariki na moja likitokana
na Waziri Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa.
Katika panga pangua hiyo, mawaziri 16
wamefanikiwa kudumu katika baraza hilo tangu Rais Kikwete aingie
madarakani ambao ni Sofia Simba, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wasira,
Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli.
Wengine ni
Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia, Dk Mary Nagu
na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye kabla ya kuteuliwa kushika nafasi
hiyo, alikuwa naibu waziri na baadaye waziri wa Tamisemi.
Mawaziri
wengine waliopo sasa ambao mwaka 2005 walikuwa manaibu mawaziri ni
Gaudencia Kabaka, Bernard Membe, Celina Kombani, Christopher Chiza na
Mathias Chikawe.
Naibu waziri pekee ambaye alikuwamo
katika baraza la mawaziri la kwanza la Rais Kikwete akiwa na wadhifa
huohuo ni Dk Makongoro Mahanga ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Kazi na
Ajira.
Waliotemwa
Mawaziri
waliotemwa au kujiuzulu tangu Rais Kikwete aingie madarakani, wakiwamo
wale walioshindwa katika kinyang’anyiro cha ubunge ni Edward Lowassa,
ambaye alijiuzulu, Antony Diallo, Dk Ibrahim Msabaha, Basil Mramba, John
Chiligati, Andrew Chenge, Joseph Mungai, Dk Emmanuel Nchimbi, Lawrence
Masha, Mustafa Mkulo, William Ngeleja, Dk Cyril Chami, Omary Nundu,
Bakari Mwapachu na Kingunge Ngoimbale-Mwiru.
Wengine ni
Ezekiel Maige, Dk Hadji Mponda, Teresa Huvisa, Shamsi Vuai Nahodha,
Nazir Karamagi, Dk Mathayo David, Khamis Kagasheki, Profesa Anna
Tibaijuka, Profesa Sospeter Muhongo, Dk Batilda Buriani, Joseph Mungai,
Diodorus Kamala, Mohamed Seif Khatib, Mwantumu Mahiza, Profesa Peter
Msola na Profesa David Mwakyusa, Philip Marmo na Juma Ngasongwa.
Naibu
mawaziri ni Dk Luca Siyame, Balozi Seif Ally Idd, Hezekiah Chibulunje,
Shamsa Mwangunga, Daniel Nsanzugwanko, Hezekiah Chibulunje, Rita Mlaki,
Dk Charles Mlingwa, Zabein Mhita, Athuman Mfutakamba, Dk Lucy Nkya,
Goodluck Ole Medeye, Benedict Ole Nangoro, Gregory Teu, Philipo Mulugo,
Mohamed Abood, Dk Aisha Kigoda, Omari Yusuf Mzee, Jeremiah Sumari, Dk
Maua Daftari, Zakia Meghji, Joel Bendera, Abdisalaam Issa Khatib na
James Wanyancha.
Pia, wapo ambao walifariki dunia ambao ni Salome Mbatia, Juma Akukweti, Jeremiah Sumari na William Mgimwa.
Badiliko la Kwanza
Katika
baraza lake la kwanza Rais Kikwete aliteua mawaziri na naibu mawaziri
60 Januari 2006 na ilipofika Oktoba 2006, Rais Kikwete alifanya
mabadiliko ya kwanza makubwa ya baraza lake la mawaziri kwa kuwahamisha
vituo vya kazi mawaziri 10 na naibu mawaziri wanane.
Mawaziri
waliohusika na mabadiliko hayo ni Diallo (Maliasili na Utalii) ambaye
alihamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Profesa Maghembe (Kazi,
Ajira na Maendeleo ya Vijana) kupelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Dk
Msabaha (Nishati na Madini) alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Karamagi (Viwanda na Biashara) alihamishiwa Wizara ya
Nishati na Madini, Mramba (Miundombinu) alihamishiwa Viwanda na Biashara
na Chiligati (Mambo ya Ndani) alihamishiwa Wizara Kazi, Ajira na
Vijana.
Mawaziri wengine ni Chenge (Ushirikiano Afrika
Mashariki) alihamishiwa Wizara ya Miundombinu, Dk Kawambwa (Maendeleo ya
Mifugo) alihamishiwa Wizara ya Maji, Wasira (Maji) alihamishiwa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Mungai (Kilimo, Chakula na Ushirika)
alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Naibu Mawaziri
waliohamishwa wizara zao na kupelekwa wizara nyingine ni Dk Nchimbi
(Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni) kwenda Wizara ya Kazi,
Nsanzugwanko (Kazi na Ajira) kwenda Wizara ya Habari, Michezo na
Utamaduni, Dk Mathayo (Biashara na Viwanda) kwenda Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika na Chibulunje (Kilimo, Chakula na Ushirika) kwenda
Wizara ya Viwanda na Biashara.
Wengine ni Dk Buriani
(Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) kuhamishiwa Wizara ya
Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Mbatia (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji)
kwenda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Masha (Nishati na
Madini) kwenda Mambo ya Ndani na Membe (Mambo ya Ndani) kuwa Naibu
Waziri wa Nishati na Madini.
Badiliko la Pili
Februari
2007, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa mawaziri wawili na naibu waziri
wawili baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa. Nafasi ya Migiro ilichukuliwa na Membe.
Dk
Buriani aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na
Uratibu) kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha Akukweti. Kabla
ya uteuzi huo Buriani alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mipango, Uchumi
na Uwekezaji.
William Ngeleja aliteuliwa kuwa Naibu
Waziri wa Nishati na Madini na Gaudence Kayombo aliteuliwa kuwa Naibu
Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji.
Badiliko la tatu
Februari
12, 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu
kutokana na kashfa ya Richmond, Kikwete alivunja Baraza la Mawaziri na
kuliunda upya.
Lowassa alijiuzulu sambamba na waliokuwa
mawaziri wawili Dk Msabaha na Karamagi ambao wote walikuwa wameiongoza
Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti. Nafasi zao zilizibwa na
William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Kamala (Afrika Mashariki), huku
Pinda akiteuliwa kuchukua nafasi ya Lowassa.
Badiliko la nne
Rais
Kikwete alifanya mabadiliko mara ya nne katika baraza lake Mei, 2008
baada ya Chenge, ambaye ni mbunge wa Bariadi, kujiuzulu kutokana na
kashfa ya ununuzi wa rada na nafasi yake kujazwa na mbunge wa Bagamoyo,
Dk Kawambwa huku Rais Kikwete pia akibadilisha mawaziri kadhaa.
Badiliko la tano
Mei
2012, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya tano katika baraza lake baada
ya kuwaondoa mawaziri sita baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa
Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwa walikiuka maadili ya utumishi wa
umma na kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia mali za umma.
Katika
mabadiliko hayo waliondolewa walikuwa ni Mkulo (Fedha), Ngeleja
(Nishati na Madini), Dk Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Maige
(Maliasili na Utalii), Nundu (Uchukuzi) na Dk Chami (Viwanda na
Biashara). Wengine waliotemwa ni Mfutakamba (Naibu, Uchukuzi) na Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Nkya.
Mawaziri
walioziba nafasi hizo ni William Mgimwa (Fedha), Kagasheki (Utalii), Dk
Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara),
Dk Mwinyi (Afya), Profesa Muhongo (Nishati na Madini), Dk Seif Rashid
(Naibu, Afya) na George Simbachawene (Naibu, Nishati na Madini).
Manaibu
wapya walioingia ni January Makamba (Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia), Dk Charles Tizeba (Uchukuzi) na Amos Makala (Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo). Wengine ni Dk Binilith Mahenge (Maji),
Stephen Masele (Nishati na Madini), Angela Kairuki (Katiba na Sheria),
Janet Mbene na Saada Mkuya Salum (Fedha).
Badiliko la sita
Januari
19, 2014, Rais Kikwete alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri
kwa kuteua mawaziri wapya wawili na manaibu mawaziri wapya wanane, huku
akiwapandisha vyeo manaibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.
Katika
mabadiliko hayo, Rais Kikwete aliwapumzisha Dk Terezya Huvisa, ambaye
alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Gregory Teu,
aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Philipo Mulugo
aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine
waliopumzishwa ni Benedict Ole-Nangoro aliyekuwa naibu waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Goodluck Ole-Medeye aliyekuwa naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mabadiliko
hayo yalikuwa yanalenga kujaza nafasi zilizoachwa na Balozi Khamis
Kagasheki (Maliasili na Utalii, Dk Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi),
Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk Mathayo (Maendeleo ya
Mifugo) waliotemwa Desemba 2013 kutokana na kashfa ya Operesheni
Tokomeza na nafasi ya Dk Mgimwa, aliyefariki dunia kutokana na maradhi.
Mawaziri
wapya walioteuliwa wakati huo ni Dk Asha-Rose Migiro (Katiba na
Sheria), Dk Titus Kamani kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Wengine
aliowateua kuwa naibu mawaziri ni Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa
Fedha, Dk Kebwe Stephen, Naibu Waziri, Afya na Ustawi wa Jamii na
Jenista Mhagama, naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Pia,
Dk Pindi Chana aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto na Kaika Telele, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi. Wengine ni Godfrey Zambi, naibu Waziri Kilimo, Chakula na
Ushirika, Juma Nkamia, Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
na Mahmoud Mgimwa, Naibu Waziri, Maliasili na Utalii.
Naibu
mawaziri waliopandishwa kuwa mawaziri ni Saada Mkuya (Waziri wa Fedha),
Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii) na Dk Seif Seleman Rashidi ( Afya
na Ustawi wa Jamii), Dk Binilith Mahenge alipandishwa kutoka Naibu
Waziri wa Maji na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira).
Dk Hussein Ali Mwinyi alihamishwa kutoka
Afya na Ustawi wa Jamii kwenda Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na
wengine kadhaa walihamishwa.
Badiliko la saba
Juzi,
Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya saba ambayo yanawezekana kuwa
yatakuwa ya mwisho kutokana na kusalia miezi sita kabla ya kuvunjwa kwa
Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.
Mabadiliko
hayo baada ya mawaziri wawili, Profesa Tibaijuka (kufutwa kazi) na
Profesa Sospeter kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Tegeta
Escrow.
Walioingia ni manaibu waziri wawili, Charles
Mwijage (Nishati na Madini) na Anna Malecela (Elimu na Ufundi). Wengine
walihamishwa ambao ni Wasira kutoka Ofisi ya Rais kwenye Kilimo na
Ushirika, Lukuvi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi.
Wengine ni Dk Nagu kwenda Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) na Jenister Mhagama (Waziri Mkuu, Uhusiano, Uratibu na Bunge).
Dk
Harrison Mwakyembe anahamia Afrika Mashariki (kutoka Uchukuzi) na
nafasi yake inachukuliwa na Sitta akitokea Wizara ya Afrika Mashariki.-