Kingunge: Katiba mbovu inadumaza maendeleo


Mwanasiasa mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombare Mwiru akizungumza na wanahabari. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Uchumi wa Tanzania utaendelea kudumaa kama itaendelea kung’ang’ania Katiba isiyokuwa na misingi bora ya maendeleo ya uchumi. Hayo yalisemwa jana na mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru mjini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) .
Wakati kiongozi huyo akisema hayo, mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed amesema kama siyo Muungano, Zanzibar ingekuwa imeshapinduliwa zaidi ya mara 10.
Kingunge, aliyekuwa mjumbe wa Bunge la Katiba, alisema licha ya Tanzania kuonekana inapiga hatua, asilimia kubwa ya uchumi wake bado ni tegemezi hivyo inahitaji kuwa na katiba bora itakayoweka misingi ya maendeleo ya uchumi .
 “Tatizo hili liko katika nchi nyingi za Afrika na hasa za Waafrika weusi, uchumi wake bado ni tegemezi,” alisema Kingunge.
Alisema historia inaonyesha Waafrika pamoja na kujikomboa kutoka katika mikono ya wakoloni, bado ni wanyonge kwa sababu ya kushindwa kujijengea uchumi imara usiotegemea nchi nyingine.
Alisema kama Waafrika wataendelea kuridhika na mwendo wa kutumia vitu vinavyotengenezwa na nchi nyingine, ipo siku ukoloni utarejea katika nchi hizo.
“Na hili wala msifikiri kuwa ni njozi ya Kingunge. Kama tunataka kutumia kweli gesi ambayo inapatikana nchini kwetu lakini wataalamu wanatoka nje, ipo siku tutalia zaidi,” alionya Kingunge.
Alisema lazima ifike wakati kama walivyofanya waasisi wa nchi ambao waliamua kupambana na wakoloni ili kuiweka nchi huru, “Huu ni wakati wa kizazi cha sasa nacho kujiuliza, hivi na sisi tunastahili kuwa katika hali hii? Tujifunze kutoka kwao ili tuvuke hapa tulipo.”
Mkongwe huyo alisema viongozi wengi wa Afrika wamechelewa kuitambua nguvu ya nchi za Magharibi kwenye suala zima la maendeleo katika nyanja ya uchumi ambalo linasimamiwa kwa mujibu wa katiba ya nchi zao.
Alisema asilimia kubwa wamewekeza katika teknolojia za kisasa za uchumi ambazo kwa nchi kama Tanzania, bado hawajaliona hilo ama kwa bahati mbaya, au kwa makusudi ya kung’ang’ania Katiba mbovu.
Alisema Tanzania imepata uhuru wa siasa na siyo wa kiuchumi kwa kuwa Watanzania wengi bado ni maskini waliojaa ujinga na wanakubali kukandamizwa bila kutafuta njia mbadala ya kujinasua.
Alisema ni ajabu kuona nchi iliyopata uhuru kwa zaidi ya miaka 50 bado watu wake wanategemea vifaa kutoka nje kwa ajili ya matumizi mbalimbali badala ya kuvitengeneza wenyewe.
Alisema suala hilo linahitaji tafakari ya kina. “Wote hapa tumeletwa na magari, vipaza sauti hivi na hata nguo tulizovaa zote zinatengenezwa nje ya nchi licha ya sisi kulima pamba,” alisema.
Kingunge alisema majibu ya hayo yote ni kuwa na Katiba bora itakayokuwa inajali uchumi wa nchi na mustakabi mzima wa maisha ya Watanzania kuelekea katika maendeleo ya kweli.
Alisema Katiba Mpya inayopendekezwa kwa mara ya kwanza imetoa mwelekeo wa kuitoa Tanzania hapa ilipo na kuipeleka mbele.
Hata hivyo, alisema Katiba hiyo iliyopendekezwa siyo Msahafu wala Biblia, kwa kuwa inaweza kubadilika kwa kufanyiwa marekebisho. “Kama kuna vitu alivyoviumba Mungu, binadamu wanavijadili na kuvikosoa, kwanini isiwe kwa Katiba,” alihoji Kingunge.
Hamad Rashid na Muungano
Akizungumzia Muungano wa Tanzania, mbunge Hamad Rashid alisema haukuja kinadharia bali ulikuwa na makusudi yake na wanaotaka uvunjike, hawaijui historia.
Alisema Zanzibar ina historia na uzoefu mkubwa wa mfumo wa vyama vingi kuliko Bara kwa kuwa imepitia katika mikono mingi ya watawala wa nchi tofauti.
“Na kama isingekuwa imeungana na Tanganyika, ni dhahiri ingekuwa imeshapinduliwa zaidi ya mara kumi na hili si mzaha nalisema kwa kufuata historia na viashiria vyake,” alisema Rashid.
Alisema ili kuepuka hilo lisitokee, Watanzania waisome kwa makini Katiba Inayopendekezwa ili wafanye uamuzi sahihi itakapofika siku ya kuipigia kura, Aprili 30, mwaka huu.
Alivitaka vyombo vya habari kuendelea kuuelimisha umma nini kilichomo ndani ya katiba hiyo.
Wakati huo huo, mbunge huyo alisema nguvu ya kuiondoa Serikali ya CCM madarakani ni Katiba na siyo mikutano ya hadhara wala maandamano.
“CCM haiwezi kung’olewa madarakani kwa maandamano wala mikutano ya hadhara ya Kibandamaiti na Jangwani,” alisema.
“Na hata Katiba Inayopendekezwa haiwezi kupingwa kwa mikutano ya hadhara inayofanyika Jangwani na Kibandamaiti,” alisema Rashid.
Powered by Blogger.