Utata mpya waibuka mauaji ya askari Kinapa
Moshi. Imedaiwa kuwa askari wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima
Kilimanjaro (Kinapa) alifariki dunia baada ya risasi zaidi ya 20 kutoka
katika bunduki ya SMG kufyatuka mfululizo na kumpata.
Taarifa
za awali zilieleza kuwa askari huyo, Mathayo Mkungu (35) aliuawa na
askari mwenzake Januari 21 katika Kitongoji cha Nduweni wilayani Rombo
wakati akiwa katika jitihada za kumkamata mtuhumiwa wa ujangili.
Ilidaiwa mtuhumiwa huyo alikaidi amri ya kujisalimisha, hivyo akatiwa mbaroni.
Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo aliwasha msumeno unaotumia mashine (Chainsaw), kwa lengo la kuwadhuru askari hao.
Askari
hao wa Kinapa walianza kurudi kinyumenyume ili kujihami na ndipo
mmojawao alianguka chini na bunduki yake ikafyatuka na kutoa risasi
mfululizo na moja ikampata marehemu Mkungu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nduweni, Gervas Shirima alidai tukio hilo lilitokea maeneo ya kijijini na siyo msituni
Alisema hajui mtuhumiwa iwapo alikuwa na kibali cha kutumia msumeno huo wa mashine.
Meneja
Uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete alikataa kueleza lolote kuhusu
tukio hilo akisema ni la kijinai na wenye mamlaka ya kulisemea ni
polisi.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela ilidai kuwa askari hao wa Kinapa
walikuwa katika haratati za kumkamata mtu aliyekuwa anakata miti kinyume
cha sheria.
Kamanda Kamwela alidai wakiwa katika
harakati hizo ndipo mmoja wa askari hao alianguka na bunduki yake
ikafyatuka risasi mfululizo na kumpata marehemu begani.
James Mmbando alidai kuwa kijana huyo alikuwa akipasua vipande vya mbao alivyoviokota katika Shamba la Misitu la Rongai.
“Alikuwa
anapasua mbao baada ya magogo kuvunwa, alikuwa kijijini kabisa siyo
hifadhini. Kutoka msituni hadi kijijini ni kilometa karibu 30,” alidai
Mmbando.