DC awasimamisha kazi mgambo kwa kupokea rushwa
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, Amani Mwenegoha
amewasimamisha kazi mgambo wa Kata ya Igulwa baada ya kutuhumiwa kupokea
rushwa na kuwaachia wahalifu.
Mwenegoha alifanya
uamuzi huo baada ya Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya kubaini
kuwa, watuhumiwa walikiuka maadili na wamekuwa wakikamata watu bila
kibali.
Pia imebainika kuwa, wakiagizwa kukamata wahalifu huwaachia baada ya kupokea rushwa.
Aliwataja
mgambo waliosimamishwa kuwa ni Juma Makenzi, Kesi John, Bembenya Kumba
na Wilson Kapango ambao hawaruhusiwi kufanya kazi wilayani hapo.
Mkuu
huyo wa wilaya alisema adhabu hiyo ni fundisho kwa wengine wanaopenda
kukiuka maadili ya kazi na kuongeza kuwa, mgambo wanatambulika kama
askari halali na kuwataka wazingatie viapo vyao.
Aliwataka
mgambo wote kuhakikisha kuwa, kama askari wa akiba ni lazima wafanye
kazi kwa weledi kwa kulinda haki na mali za wananchi.
Pia,
Mwenegoha alitoa wito kwa wakazi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano na
ofisi yake pindi wanapoona watendaji wa Serikali wanakiuka maadili ya
kazi zao ili wachukuliwe hatua stahili.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mgambo waliosimamishwa kazi walikiri kupokea barua za kusimamishwa kufanya kazi.
Juma
Makenzi alisema uamuzi wa Kamati siyo sahihi kwani hawakuitwa kujitetea
na wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na watumishi wa Mahakama na
polisi.
Naye Bembenya Kumba alikana kupokea rushwa katika tukio alilodai walishiriki wenzake watatu bila yeye.
Kumba
alisema wenzake hao walipokea Sh1 milioni huku katika kesi nyingine ya
jinai walipokea Sh1 milioni na nyingine Sh200,000 katika kesi ya
uhamiaji.
Naye Ofisa Mtendaji Kata ya Igulwa, Amos Abed
alisema ametekeleza agizo la mkuu wa wilaya kwa kuwasimamisha kazi na
kuongeza kuwa, wamekuwa na tabia ya kukamata watu bila kuhusisha ofisi
yake na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi na watendaji wa
vijiji.
Mwisho